KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amemtaka mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete kuwafundisha viongozi walio chini yake mambo ya kuongea ili wasiendelee kulidhalilisha taifa.
Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jana wakati akihutubia mikutano mbalimbali na kugusia madai yaliyotolewa juzi na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nauye, kuwa CHADEMA inatumia mgongo wa kuficha fedha za wafadhili wao wa nje kwa kujifanya inakusanya michango ya wananchi kuendeshea shughuli zao.
Alisema kuwa CCM ndio wenye serikali, vyombo vya upelelezi na hata mamlaka ya kukamata, hivyo akashangaa ni kwanini wageuke kuwa walalamishi kwa matukio ambayo wanaona ni hatari kwa usalama wa taifa.
Alisema, kama kauli aliyotoa Nape ina ruhusa ya mwenyekiti wake, basi nchi itakuwa imepoteza umakini wake kwa kuwa, kauli hiyo inazidi kuivua nguo serikali ya CCM na viongozi wake.
Aliongeza kusema kuwa, alichofanya Nape hakina tofauti na kauli aliyowahi kuitoa Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, wakati wa uchaguzi mdogo wa Igunga kuwa CHADEMA kilikuwa kimeingiza nchini makomandoo kutoka nje ya nchi, zikiwemo Afghanistan, Israel na kwingineko na alipotakiwa kuthibitisha kauli hiyo alishindwa.
Alisema, kauli za CCM si propaganda tena bali ni ujinga ambao unaivua nguo serikali ya Kikwete na chama chake kuwa kimeshindwa kuwadhibiti watu wanaodaiwa kuingiza fedha chafu kutoka nje ya nchi.
“Kama kweli tunaweza kufanya yote haya na serikali ipo, basi wanapaswa kutuvulia kofia, kutupigia saluti. Sasa wanasubiri nini, kina Nape na kina Mkama wanasaidia kutangaza kuwa serikali hii imeshindwa,” alisema Dk. Slaa.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment