Sunday, August 12, 2012

Chadema yatupia jicho Urais 2015


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema Chadema imedhamiria kuingia madarakani 2015 bila maandamano na kwamba kipaumbele chake kikubwa kitakuwa ni elimu.
Mbowe alitoa kauli hiyo juzi jijini Dar es Salaam katika harambee ya kuchangisha fedha za maendeleo ya chama chao kuleta vuguvugu la mabadiliko (M4C) iliyoandaliwa na vijana wa chama mkoani Dar es Salaam juzi usiku na kuhudhuriwa na wapenzi na wanachama zaidi ya 500 na kuwezesha kukusanya fedha taslimu Sh. milioni 270 na ahadi zikiwa ni Sh. milioni 253
Mbowe alisema chama hicho kitachukua nchi kupitia M4C iliyoshika kasi na kuwataka Watanzania kuondoa woga katika kuendeleza vuguvugu la mabadiliko ili Chadema iweze kupata ushindi katika uchaguzi mkuu ujao.
"Tukichukua nchi kipaumbele chetu ni elimu hii inatokana na Watanzania wengi kukosa haki hii na wamekuwa masikini na kushindwa kusimamia rasilimali zao," alisema.
Alisema wakati uliopo ni wa vitendo na si kulalamika na kwamba kinachotakiwa chama kupata wabunge wa kuchaguliwa wasiopungua 186 katika uchaguzi wa 2015.
Mbowe ambaye ni mbunge wa Siha alisema kufanya mapinduzi kwenye elimu kutawezesha vijana wengi kusimamia rasilimali zao hasa zilizopo majini na madini ambazo nyingi zinaongozwa na wageni kwa zaidi ya asilimia 95.
Alisema chama chake kipo salama pamoja na propaganda chafu zinazoenezwa na wapinzani kuwa kinaudini na ukabila madai aliyosema si kweli.
"Harakati za vuguvugu la maendeleo nchi nzima zitaendelea bila woga wala hofu kwa sababu chama chetu kilizianzisha mwaka 1991 huku tukipitia katika mazingira magumu" alikumbusha.

Nipashe

No comments:

Post a Comment