Monday, August 20, 2012

Chadema yasambaratisha mkutano wa DC

CHAMA cha Demokrasia na Maendendeleo (Chadema), kimevunja mkutano wa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Elius Tarimo baada ya mikutano hiyo kugongana, huku wa mkuu wa wilaya ukilazimika kuvunjika kutokana na kukosa watu.

Tukio hilo lilitokea Kata ya Lumuma,Tarafa ya Kidete, wilayani humo wakati ratiba ya mkutano wa Chadema na mkutano wa mkuu wa wilaya wa kuhamasisha wananchi kushiriki sensa ilipogongana.

Viongozi wa Chadema waliwasili katika kata hiyo saa 9.00 mchana na kuamua kufanya mkutano wao stendi ya mabasi,umbali wa mita takribani 500 kutoka sehemu ulipoandaliwa mkutano wa mkuu wa wilaya hiyo.

Kufuatia hali hiyo,baadhi ya watu ambao walikataa kujitambulisha majina yao wakiwamo waliovalia sare za CCM, walianza kuzozana na Mkuu wa Operesheni wa Chadema, Singo Benson huku wakikitaka Chadema kusitisha mkutano wake ili kupisha mkuu wa wilaya.

Saa moja baada ya Chadema kuanza mkutano wake,ujumbe wa mkuu wa wilaya uliwasili kwenye eneo la mkutano na Ofisa mtendaji wa kata hiyo,Deo Lisanga akiwa ameambatana na mwakilishi wa Kamanda wa Polisi Wilaya (OCD), walipovamia mkutano huo na kutaka usitishwe kwa madai haukuwa halali.

Benson alimweleza mwakilishi wa OCD, Antony Mkwawa kuwa mkutano wao ni halali na una baraka zote kutoka kwa kamanda wa polisi wa wilaya, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro na Mkuu wa Polisi nchini (IGP), Said Mwema.

Baada ya kuelezwa hivyo waliondoka eneo hilo na kwenda kuahirisha mkutano wa mkuu wa wilaya.
Kwa upande wake,kada wa Chadema, Ally Bananga aliwaeleza wakazi wa kijiji hicho kuwa chama hicho kimeanzisha mpango wa kuwa na serikali mbadala katika kila kijiji na kata,ili wananchi wenye kero zao waziwasilishe kwa uongozi huo na Chadema makao makuu itafute ufumbuzi.


Mwananchi

No comments:

Post a Comment