Thursday, July 26, 2012

Zitto Kabwe aug’ang’ania urais 2015


NA THOBIAS MWANAKATWE
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, ameung’ang’ania urais kwa kusema kama urais upo utakuja tu na kwamba hana mashaka na uwezo, uadilifu, uzalendo wake pamoja na kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, ametoa kauli hiyo siku chache, baada gazeti moja  (siyo NIPASHE) kuandika kuwa wabunge wawili wa Chadema wamemsafishia njia ya kugombea kiti hicho katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Hata hivyo, juzi ikiwa ni siku moja baada ya kuchapishwa kwa habari hiyo, wabunge hao ambao ni Joshua Nassari (Arumeru Mashariki na Halima Mdee (Kawe) walitoa taarifa katika vyombo vya habari za kutoa kauli za kukanusha na kujiweka mbali na mpango wa kumpigia debe Zitto.

Zitto alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akichangia makadiro ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2012/13. 

“Ndugu zangu wasanii, najua kuwa suala la tamasha la Kigoma limeleta maneno maneno kidogo ya kisiasa, lakini hayo ni maneno yatapita kwa sababu kama urais upo utakuja tu, kama haupo hautakuja, hata mtu afanye nini,” alisema na kuongeza:

“Muhimu ni kuhakikisha kuwa tunafanya kazi ya ziada kuitetea nchi yetu na jambo moja tu ambalo sina mashaka nalo hata kidogo ni uwezo, uadilifu, uzalendo wa kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa nchi yetu. Hili sina mashaka nalo hata kidogo na kama nina mashaka labda  mambo mengine, lakini kwa hili sina mashaka hata kidogo Mheshimiwa Mwenyekiti.”

Kabla ya kuchangia makadirio hayo bungeni jana, Zitto, alisambaza taarifa katika vyombo vya habari na kuweka bayana kwamba mwanachama wa Chadema atakayekubalika kwa wajumbe wa mkutano wa uteuzi wa chama chake na jamii ndiye atakuwa mgombea wa urais kupitia chama hicho.

Zitto pia alitoa ufafanuzi kuhusiana na mambo yaliyojitokeza katika tamasha la vijana lililofanyika wiki iliyopita mjini Kigoma, ambako ilidaiwa kuwa wabunge hao na Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM) walitoa kauli za kumpigia debe.

“Nisingependa kuhusishwa kwa njia yeyote ile na matamshi yao, habari iliyowanukuu na hata makanusho yao. Maana mwisho wa siku ukweli ndio utasimama,” alisema katika taarifa hiyo.

Zitto alisema: “Suala la urais lisitupotezee muda kwani kuna mambo mengi sana ya kujadili kuhusu nchi, taharuki wanazopata watu masuala ya urais yanapotajwa zinashangaza sana.”

Alisema ifahamike kuwa Chadema bado hakijatangaza rasmi mchakato wa kupata mgombea urais, ambapo mchakato utakapotangazwa wanachama wataruhusiwa kuomba kupeperusha bendera ya chama.

“Mwanachama wa chama chetu (Chadema) atakaye kubalika na jamii na wajumbe wa mkutano wa uteuzi ndiye atakuwa mgombea wetu, kwa sasa hayupo na hivyo tusipoteze muda kujadili jambo hili,” alisema.

Zitto alinukuu wosia wa mmoja wa waasisi wa Afro Shiraz Party (ASP), Hayati  Sheikh Thabiti Kombo, kuwa tunapokuwa tunazungumza kuwa: “Weka akiba” sio akiba ya fedha, bali ya akiba ya maneno. Tuweke akiba ya maneno. Tusimalize yote.”

Akifafanua zaidi kuhusu tamasha hilo, alisema wabunge wote walioalikwa waliambiwa hii ni shughuli ya muziki na wala hakufanya mazungumzo na yeyote awali au kuwaambia au kukubaliana nini cha kuzungumza katika tamasha hilo.

“Tamasha lilikuwa la muziki na halikuhusika kabisa na siasa. Ni bahati mbaya sana kuwa kuna matamshi ya kisiasa yalitamkwa katika shughuli ile,” alisema Zitto katika taarifa yake.

Alisema katika tamasha hilo wabunge wote walipewa nafasi ya kusalimia na wote walizungumza ambapo waliozungumza kwa muda mrefu kidogo ni Mdee, Nassari, Filikunjombe na Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola.

Alisema hotuba za wabunge wote zilirekodiwa kwenye video neno kwa neno na kwamba video hizo zitawekwa wazi kwenye blogu yake (Zitto) kama sehemu ya ‘documentary’ ya tamasha hilo la kihistoria.

Zitto alisema hakuhusika kwa namna yeyote ile na kuandikwa kwa habari iliyowanukuu wabunge wanaodaiwa kumsafishia njia ya urais iliyozusha mjadala.

“Wala sikujua kama habari hii ingeandikwa, maana katika ziara ile sikuita mwandishi hata mmoja maana nilitaka liwe tukio la Kigoma tu, mimi kama mlezi wa Kigoma All Stars na vijana wenyewe tulijikita katika ‘shukrani Kigoma’ kwa watu wa Kigoma,” alisema Zitto.

Aliongeza kuwa, kama mwandishi kaandika mambo  ambayo wabunge hawakuyasema itaonekana kwenye video hizo na wabunge wenyewe wanajua kwenye nafsi zao nini walisema Kigoma na kipi kiliwasukuma kusema walioyasema Kigoma.

Alisema tangu habari hiyo ilipoandikwa katika hilo imeleta mjadala mara baada ya kutoka na kusomwa ambapo mjadala umekuzwa zaidi baada ya wabunge Mdee na Nassari kukanusha maneno waliyonukuliwa kuyasema.

Juzi Nasari na Mdee walisambaza taarifa kwa vyombo vya habari kukanusha kwamba hajawahi kutamka wala hawatarajii kutamka maneno ya kumsafishia njia ya urais Zitto.

Nassari alisema akiwa kama Mtanzania ambaye ni mwanachama wa Chadema kinachoamini kuwa suala la urais si kipaumbele, bali muhimu kwa wakati huu ni kushughulika kujua mizizi au vyanzo vya matatizo yanayowakabili Watanzania ikiwemo umaskini, ujinga, maradhi, ufisadi na utawala mbovu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Naye Mdee alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa habari iliyoandikwa na kumnukuu yeye ni ya uongo na imesigina misingi ya uandishi na hususani katika kufuata maadili ya taaluma ya uandishi wa habari kwa kiwango cha kufanya moja ya dhambi kubwa ya kukilisha maneno chanzo cha habari.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment