Tuesday, July 17, 2012

Waghushi waraka kuhusisha Chadema na migomo


Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Slaa, ameeleza kuwa wapinzani wa kisiasa wa chama hicho wameghushi waraka wenye sahihi yake ambao unakihusisha chama hicho na migomo inayoendelea nchini.

Akizungumza na NIPASHE jana kwa njia ya simu, Dk. Slaa alisema inashangaza watu kughushi waraka wa namna hiyo wakati ambao nchi inakabiliwa na changamoto nyingi hususani za kuwakwamua wananchi na lindi la umaskini.

Alisema chama hicho kitaendelea kutekeleza wajibu na majukumu yake kama chama cha siasa ikiwemo kuuelimisha umma juu ya haki za msingi pamoja na umuhimu wa kushiriki kwenye shughuli za maendeleo ya nchi.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa shirikisho la Chama Cha Mapinduzi katika Vyuo Vikuu vya Mkoa wa Dar es Salaam, Asenga Abubakar, alisambaza waraka unaodaiwa kutolewa na Dk. Slaa kwa viongozi wa Chadema kuwataka washinikize migomo nchini hususani wa walimu.

Akizungumza na NIPASHE jana, Asenga alisema waraka huo umesambazwa kwenye mitandano ya kijamii na kwamba yeye (Asenga), alitoa nakala na kuzisambaza kwa vyombo vya habari kwa nia njema ya kukemea maelekezo hayo.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment