WAKATI wabunge wakitoa tuhuma nzito dhidi ya wenzao wanaodaiwa kujihusisha na ufisadi ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), imebainishwa kuwa wabunge wenye tabia hiyo ni watano, watatu kutoka chama tawala CCM na wawili upinzani.
Habari zilizopatikana jana mjini Dodoma zimeeleza kuwa baadhi ya wabunge hao wanatoka katika Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, huku wengine wakitoka Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, wabunge hao wamedaiwa kuwa wamekuwa wakitumia nafasi zao za ubunge na ujumbe wa kamati kufanya biashara na Tanesco na kutetea mafisadi ndani ya shirika hilo la umma.
Gazeti hili limefanikiwa kupata majina ya wabunge hao, ambayo leo hatutayataja kwa sababu za kitaaluma.
Baadhi ya wabunge waliochangia hoja hiyo bungeni juzi na jana walisema kuwa, wanawafahamu wabunge hao kwa majina, lakini hawapendi kuwataja kwa kuwa siyo wakati mwafaka.
Moto wa kutaka kutajwa kwa majina ya wabunge hao ulikolezwa jana na Mbunge Vita Kawawa wa Namtumbo(CCM) aliyeomba Mwongozo wa Spika, akitaka jambo hili lijadiliwe na Bunge na kupendekeza kuwa, Kamati za Bunge zinazotuhumiwa kwa rushwa zivunjwe.
“Waheshimiwa wabunge wamejadili suala hili kwenye wizara, lakini kwa mujibu wa kifungu cha 55 (3)f mbunge au waziri anaweza kutoa hoja ili jambo fulani lijadiliwe. Sasa naomba kutoa hoja ya kujadili suala hilo," Kawawa alisema.
Aliliomba pia Bunge likubali kuivunja na kuiunda upya Kamati ya Nishati na Madini na kamati nyingine zilizolalamikiwa kwa rushwa. Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge.
Baada ya hoja hiyo kuungwa mkono Spika wa Bunge, Anne Makinda alisimama na kukubali hoja hiyo ya Kawawa na kutangaza kuivunja Kamati ya Nishati na Madini.
Spika Makinda alisema ameiagiza Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge kutengeneza kanuni za kuwadhibiti wabunge wenye tabia hiyo ya kupokea rushwa kutoka kwa watu mbalimbali ili kutimiza matakwa yao binafsi.
"Ninakubali kuivunja Kamati ya Nishati na Madini na zingine ambazo zitatajwa kwenye tuhuma hizo. Nalipeleka pia suala hilo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, halafu kama ni kutajwa (wabunge hao), basi tutapata mwongozo wa kamati hiyo." alisema Spika Makinda na kuongeza:
"Nasema kwa dhati kabisa, kitendo hiki hakikubaliki ndani ya Bunge hili. Wabunge mkae vizuri. Kama kuna baadhi yetu wanaenda huku na huku kujitafutia masilahi binafsi, tutawezaje kuisimamia Serikali?"
Mbunge Zedi
Baada ya Spika kutangaza kuvunja Kamati ya Nishati na Madini, Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Seleman Zedi alisema kuwa ameshtushwa na uamuzi huo na anasubiri uamuzi wa Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge.
"Nimeshtushwa sana na uamuzi huo, lakini tusubiri Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge," alisema Zedi.
Waziri Muhongo
Akihitimisha hoja ya wizara yake bungeni jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema kuwa baadhi ya wabunge ambao wanashiriki kwenye vikao vya uamuzi vya Tanesco kama wajumbe, wamekuwa wakilihujumu shirika hilo kwa njia mbalimbali ikiwamo kufanya nalo biashara.
"Shirika liliwahi kulipa Pauni za Uingereza 50,000 kwa ajili ya kununua vipuri, lakini kilicholetwa nchini ni masanduku ya misumari,” alisema Profesa Muhongo na kuongeza;
“Hata katika nguzo za umeme kuna biashara inaendelea. Tunajua kuwa nguzo hizo zinazalishwa Iringa na kupelekwa Mombasa kisha kurudishwa nchini kwa maelezo kwamba zimetoka Afrika Kusini."
Waziri Muhongo alisema kuwa mbali na ufisadi huo, baadhi ya wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini wamewahi kuliuzia shirika hilo matairi ya magari kwa bei kubwa, bidhaa ambayo hata hivyo alisema haina ubora unaokubalika.
"Baadhi ya wabunge wanafanya biashara na Tanesco; niseme tu kuwa, hii siyo sahihi. Lakini niombe kwamba mjadala huu tuufunge kwa sababu, tayari tumekabidhi suala hilo kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)" alisema Waziri Muhongo.
Waziri Muhongo pia alizungumzia jinsi baadhi ya watu na kampuni zinavyoiibia Tanesco kupitia mita za Luku ambapo aliwataja watu hao kuwa ni pamoja na Shule za St. Mary's zinazodaiwa Sh10.5 milioni, Access Bank, Tawi la Tabata Matumbi Sh13.8 milioni na Hoteli ya Akudo Paradaise ya Kariakoo inayodaiwa Sh25.5 milioni.
Alisema kuwa baada ya kubainika kwa wadaiwa hao hutumia umeme kinyume na utaratibu,wahusika wote walikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi baada ya kufanyika kwa uchunguzi.
“Baada ya kufanya uchunguzi na kubaini kuwapo kwa watu wanaotumia umeme bila kulipia na kuisababishia Tanesco hasara, tumeamua kuwachukulia hatua ikiwamo kuwafikisha polisi,” alisema Profesa Muhongo na kuongeza:
“Inaonyesha wazi kwamba wizi wa umeme wa Luku umekuwa ukifanyika mara kwa mara na kwamba baada ya kuwakamata hawa, uchunguzi utaendelea na wengine watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.”
Jenista Mhagama
Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama alisema kuwa, amepokea kwa masikitiko taarifa hizo za wabunge wa CCM kuingia katika tuhuma hizo, lakini akasema namna nzuri ya kushughulikia tatizo hilo ni vyombo vya dola kufanya uchunguzi makini ili kujiridhisha na kisha hatua za kisheria kufuatwa.
"Ni taarifa mbaya kwa kweli, lakini mimi niiombe Serikali itusaidie kufanya uchunguzi ili ukweli ubainike na hatua zichukuliwe," alisema Mhagama.
Mbunge Silinde
Naye Katibu wa Wabunge wa Chadema, David Silinde alisema: "Kwa kuwa tumesikia, kama kambi tutafanya uchunguzi juu ya tuhuma hizo. Tutakaa kikao cha kuamua nini cha kufanya. Pia tutatoa tamko juu ya mwenendo mzima wa hizi tuhuma na Bunge kwa ujumla.”
Zitto
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mashirika ya Umma ambayo imeunganishwa kwenye tuhuma hizo, Zitto Kabwe, alisema tuhuma hizo anazisikia, lakini anaziona kama siasa za majitaka kwa sababu zinarushwa bila ushahidi wowote.
"Hakuna hata mbunge mmoja aliyesimama kusema nani amehongwa nini. Mimi binafsi sijahongwa na mtu yeyote wala mimi sijamtetea mtu isipokuwa natetea taratibu kufuatwa," alisema.
Zitto alibainisha kuwa anaamini tuhuma hizo zimetokana na hasira za yeye kupinga posho za wabunge na sasa wameona hilo ndilo eneo la kumkomoa.
"Kwa kuwa ‘my conscious is clear’, (dhamira yangu safi) sina mashaka, uzushi, uongo na siasa za majitaka hizi zitaumbuliwa na ukweli. Hata hivyo, kwa kuwa tuhuma hizo zinasemwa juu juu tu, tutataka vyombo vya dola vichunguze na ikithibitika hatua zichukuliwe," alisema na kuongeza:
"Kwangu mimi naona hizi ni siasa za urais na hasira za posho. Wenye kutaka urais wa vyama vyote na wapambe wao, wameungana kunichafulia heshima yangu. Wabunge wenye njaa ya posho, wameungana kunikomoa. Ukweli una tabia ya kutopenda kupuuzwa. Mwalimu Nyerere (Julius) alisema katika andiko lake la 'Tujisahihishe'.”
Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini(Chadema) alishauri pia Spika wa Bunge kutumia Kamati ya Maadili kuchunguza tuhuma hizo kwa kuwa hazipaswi kuachwa zikapita hivihivi.
John Cheyo
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali, John Cheyo alisema anasikitika kuona Bunge ambalo kimsingi ni kitovu cha uadilifu limeanza kuvamiwa na mafisadi.
"Very unfortunate, (bahati mbaya sana) Bunge ambalo ni kilele cha uadilifu, nyumba ya waheshimiwa, ambako kunatarajiwa high level of intergrity (uadilifu wa hali ya juu), kuanza kutumika kama perpets (vibaraka) wa mafisadi," alisema.
Cheyo aliongeza: "Ninalaani sana kitendo hicho, lakini niwaambie viongozi wapya wa Wizara ya Nishati na Madini kuwa, waendelee kufanya kazi kwa uadilifu na nguvu yao ni wabunge wengi wema, ambao watawaunga mkono. Wasikate tama," alisema.
Mjadala ya wabunge
Mbunge wa Maswa Magharibi (Chadema), John Shibuda aliliomba Bunge kufanya uchunguzi ili kuwabaini wabunge wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.
Alisema baadhi ya wabunge wanatumia nafasi zao vibaya kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa ili kuiyumbisha Serikali.
“Namwomba Spika na timu yake yote ikaona kuna haja ya kufanya uchunguzi kwa wabunge ili kuweza kuwabaini wanaotumia nafasi zao vibaya kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa ilikuiyumbisha Serikali ,” alisema Shibuda
Mbuge Kangi
Naye Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugora alitaka Waziri wa Nishati na Madini awataje wabunge aliowatuhumu ili kuonyesha usawa hasa baada ya kuwataja kwa majina watuhumiwa wengine katika ufisadi wa Tanesco na wale wanaoliibia umeme shirika hilo la umma.
"Tunaomba waziri asema kwa nini asiwataje hao wengine wakati tayari ametutajia kina Freddy na Veronica William Mhando na taasisi za St Mary? " alihoji.
Hoja hiyo ya Lugora ilitupwa na Spika wa Bunge Anne Makinda aliyesema kuwa jambo hilo lina taratibu zake.
Kamata
Vicky Kimata (Viti Maalumu) nusura amwage machozi bungeni juzi jioni, alipozungumza kwa uchungu kupinga hatua ya wabunge hao kujihusisha na ufisadi, huku akieleza kuwa nchi imefika pabaya.
'Watanzania tumefikia hapo! Watu wanatengeneza mgawo wa umeme ili kujipatia hela, Jamani...jamani.. Hammwogopi hata Mungu!"
Said Mussa Zuberi alipendekeza itungwe sheria ya kuwanyonga mafisadi na wahujumu uchumi kwa kuwa matendo hayo pia ni uuaji.
"Katika taifa letu tuna wadudu sijui tuwaite mchwa ambao wanaharibu yaliyotengenezwa kwa maslahi yao. Nawashauri wananchi kwa kuwa sasa tuko kwenye suala la Katiba, wasisahau kupitisha sheria ili watu wahujumu uchumi tuwaue, tena kwa risasi.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment