OPERESHENI Sangara inayofanywa na CHADEMA na Zinduka inayofanywa na CUF katika maeneo mbalimbali hapa nchini zimewatisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda na mbunge wa Same Mashariki Anne Kilango Malecela (CCM).
Ingawa Pinda na Kilango hawakuzitaja operesheni hizo kwa majina lakini CHADEMA na CUF ndivyo vimekuwa vikifanya operesheni hizo kwa lengo la kujiimarisha zaidi.
Pinda alikiri kuonja joto ya operesheni hizo jimboni kwake lakini amewataka wanasiasa wanaofanya operesheni za vyama vyao kuwa wakomavu kwa kuzungumzia sera na kukosoa kwa kutumia kauli za staha badala ya matusi na kuchochea vurugu.
Pinda alitoa kauli hiyo jana bungeni mjini hapa wakati akijibu swali la mbunge wa Same Mashariki, Anne Killango Malecela (CCM), aliyetaka kujua ni hatua gani serikali inachukua kwa wanasiasa na vyama vinavyofanya mikutano kwenye majimbo ya wabunge na kukosoa utekelezaji wao wa kazi.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuwa sisi wabunge humu ndani na hata nje ya Bunge tuna uwezo wa kujenga au kubomoa amani ya nchi kutokana na kauli zetu. Hivi sasa kuna baadhi ya wabunge wanakwenda kwenye majimbo ya wabunge wengine wanafanya mikutano na kutoa lugha za matusi na wakati mwingine kusababisha machafuko, je serikali inachukua hatua gani? Alihoji Killango.
Katika majibu yake, Waziri Mkuu alisema kuwa wanasiasa wote waliopevuka kisiasa hutumia muda mwingi kujadili masuala ila wale ambao hawajapevuka wakati wote huzungumza watu.
“Nataka nikubaliane na mheshimiwa Killango kuwa dalili hizi za namna hiyo zipo maana hata mimi jimboni kwangu yalinipata lakini mambo hayo yanategemeana na ukomavu wa mwanasiasa mwenyewe kuelewa kuwa anapokwenda kwenye shughuli za kisiasa huko si kutukana watu bali kueleza sera za chama na hata kama ni kukosoa jambo analodhani halijakaa sawa anatumia staha si kauli za matusi,” alisema.
Pinda alifafanua kuwa aliwahi kukaa na Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, na kumwelekeza akutane na vyama vya siasa kimoja kimoja na kushauriana na kukumbushana wajibu wao kisheria ili wakati vinafanya kazi zake visikiuke taratibu za usajili.
“Kanuni na sheria za usajili wa vyama vya siasa zinajulikana wazi na zinatoa utaratibu kwa msajili kukifuta chama ambacho hakina usajili wa kudumu endapo kitakiuka utaratibu lakini vile vile hata chama kilichosajiliwa msajili akijiridhisha kwa mujibu wa sheria kuwa kinakiuka utaratibu na kufanya vurugu na uchochezi, anaweza kukifuta.
CHADEMA kuanza Sangara
Wakati Pinda akizizungumzia operesheni hizo, CHADEMA imetangaza kuanza operesheni Sangara Agosti 4-18 katika mikoa mitano.
Akizungumza na Tanzania Daima jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi, Msafiri Mtemelwa, alisema kuwa operesheni hiyo itahusisha wilaya moja katika kila mkoa.
Alisema kuwa ratiba yao ambayo imewekwa wazi katika ofisi ya makao makuu ya chama hicho iliyoko Kinondoni; operesheni hiyo itaanzia katika mkoa wa Morogoro.
Alitaja mikoa mingine kuwa ni Dodoma, Singida, Iringa na Manyara.
Mtemelwa alisema kuwa operesheni hiyo itaongozwa na viongozi wakuu wa kitaifa akiwepo Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe na Katibu wake Dk. Willibrod Slaa.
“Tutakuwa na timu 10 zitakazofanya operesheni hiyo na katika kila mkoa tutazungukia wilaya moja ambapo huku watakuwepo Manaibu Katibu wakuu na wabunge,” alisema.
Tanzania Daima
Kampeni hizo zitumike kuelimisha Wananchi juu ya mabo yanayowahusu kisiasa,kiuchumi na kijamii.
ReplyDeleteNawatakia mafanikio mema.
MWANZA.