Monday, July 30, 2012

Mnyika: Bunge liruhusiwe kujadili madai ya madaktari


Mbunge  wa Jimbo Ubungo, John Mnyika, ameutaka uongozi wa Bunge  kutoendelea kulizuia bunge kutumia uhuru wake katika kujadili matatizo yanayoikabili sekta ya afya nchini na mgogoro kati ya madaktari na serikali.

Mnyika alitoa wito huo katika taarifa yake aliyoitoa kwenye vyombo vya habari jana huku bajeti ya wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa mwaka wa fedha 2012/2013 ikitarajiwa kujadiliwa leo bungeni.

Mnyika alisema kwa zaidi ya miezi mitatu Bunge limekuwa likizuiwa kutumia haki, uhuru na madaraka yake kwa mujibu wa ibara za 63 na 100 za Katiba ya nchi kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi kuhusu hali ya sekta ya afya nchini na migogoro kati ya serikali na madaktari.

“Hali hii ilianza mwezi Februari 2012, Bunge lilizuiwa kujadili suala hilo kwa kisingizio kwamba mpaka kamati ya Bunge iende kukutana na wadau wote na kuwasilisha taarifa bungeni, ripoti ambayo mpaka sasa haijawasilishwa, hali hii ikashamiri zaidi mwezi Juni na Julai  ambapo Bunge lilizuiwa kujadili masuala husika kwa kisingizio kwamba kuna kesi mahakamani,” alisema.

Mnyika alisema chanzo cha hali duni kwenye sekta ya afya nchini na migogoro kati ya serikali na madaktari,  ni udhaifu katika utekelezaji wa bajeti ya serikali na ufinyu wa kiwango cha fedha kinachotengwa kwa ajili ya sekta husika kwa ajili ya dawa, vifaa tiba na maslahi ya watumishi wa umma kwenye sekta husika.

Mnyika aliongeza kuwa mjadala kuhusu mapato ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa mwaka wa fedha 2012/2013  iwe fursa ya Bunge kuingilia kati kutafuta ufumbuzi.

Aidha, aliuomba uongozi wa Bunge kutoendelea kutumia visingizio vya masuala ya mahakamani, badala yake uliwezeshe kutumia ipasavyo madaraka na mamlaka yake kwa mujibu wa katiba na kanuni zake kujadili hali ya huduma za afya nchini na kushughulikia chanzo cha mgogoro ulioendelea kati ya serikali na madaktari.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment