Tuesday, July 10, 2012

Mdee, wananchi waandamana hadi Manispaa


Mgogogro wa ardhi uliopo eneo laTegeta-Kimanga katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, umechukua sura mpya baada ya wananchi wa eneo hilo wakiwa na Mbunge wao, Halima Mdee, kuandamana mpaka Ofsi za Manispaa hiyo kutaka msimamo wa serikali kuhusu hatma yao.

Wananchi hao wameilalamikia Manispaa kwa kukaa kimya wiki mbili tangu wavamizi wanaosadikiwa kutumwa na anayedai kuwa na hati miliki ya eneo lenye mgogoro, Salum Abdalah kuwaondosha kwa nguvu katika eneo hilo.

Waziri Rashidd ni mwathrika wa mgogoro huo alisema Juni 29 walivamiwa na nyumba zao 10 kubomolewa, kuiba simu, mali, nguo na kusababisha wananchi kulala nje na watoto kushindwa kwenda shule.

“Tamko letu na Mbunge wetu ni kwamba hatutaondoka hapa Manispaa mpaka suala letu litolewe maamuzi, ni wiki mbili sasa watoto hawaendi shule, tunalala nje, hatuna chakula, hivi sisi ni Watanzania?” alihoji Rashidd.

Mbunge wa Kawe ambaye pia ni waziri kivuli Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee alisema, amesikitishwa na Manispaa kuwadanganya wananchi kuwa Ofisa Mpango Miji anafuatilia lakini hadi sasa hajafika eneo husika wala kutoa taarifa yoyote.

“Tumekuja kufuatilia usemi wa Manispaa…maana imekuwa danganyatoto kuwa suala linafuatiliwa na Ofisa Mipango Miji,” alisema Halima.

Mdee alikishauri kitengo cha usalama kiunde Oparesheni maalumu kuwasaka wanaohusika na uvamizi wa mara kwa mara katika maeneo halali ya wananchi na kutaka kuwaondosha kwa nguvu.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni Charles Kenyela, alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwani liko Mahakamani na taratibu nyingine zitachukuliwa kuwakamata wahusika.

Kenyela aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na Operesheni maalum ya kuwakamata wavamizi wa maeneo halali ya wananchi na kwamba mpaka jana vinara 12 wa matukio hayo wameshakamatwa na wako rumande kwa uchunguzi mwingine.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment