Tuesday, July 24, 2012

Mdee Naye amkana Zitto na Urais


Kwenye barua yake kwenda kwa uongozi wa juu wa gazeti la mwananchi, hii ni sehemu ya barua yake.
Nasikitika kutumia nafasi hii kukuandikia kukutaarifu kuwa gazeti lako la Mwananchi la Julai 23, 2012, katika habari yake iliyoongoza ukurasa wa kwanza (lead story) limenilisha maneno na kunikuu isivyo sahihi.

Katika habari hiyo yenye kichwa cha habari kisemacho “Wabunge wamsafishia Zitto njia ya urais 2015,” gazeti lako limeandika hivi “Mdee aliyepewa nafasi ya kuwasalimia wananchi alisema amekuwa na Zitto tangu Chuo kikuu cha Dar es Salaam na kwamba kutokana na ujasiri na umahiri wake katika kutetea masilahi ya wanyonge na taifa, anafaa kuwa mmoja wa viongozi wa juu katika Taifa.”Gazeti lako pia katika aya iliyofuata limenukuu kuwa mimi nimesema;
*“Ndugu zangu watu wa Kigoma, kwa kweli mna bahati sana, achilia mbali kuwa na vipaji katika sanaa ya muziki na michezo hasa mpira wa miguu, lakini mna wanasiasa wakali ambao ni tishio hapa nchini. Mimi namkubali sana Zitto Kabwe na ninaamini kuna siku atakuwa kiongozi wa juu katika nchi yetu," alisema Mdee”
Nasikitika kusema kuwa gazeti lako limeandika habari zisizo za kweli kwa kunilisha *maneno na kudai kuwa mimi ndiye nimesema maneno hayo, kisha kuyaweka kwenye nukuu, likisema kuwa ni nukuu yangu. Sijajua nia au kusudio la gazeti lako kuamua kupotosha ukweli na kushindwa kabisa kuninukuu kwa usahihi, kama inavyotakiwa katika misingi ya taaluma ya habari.
Nasikitika pia kusema kuwa gazeti lako ambalo limeonekana kujijengea heshima miongoni mwa wasomaji wa kada mbalimbali nchini na hivyo linapaswa kuwa mfano wa kuigwa, linaweza kusigina misingi ya uandishi wa habari na hususan katika kufuata maadili ya taaluma hii muhimu, kwa kiwango cha kufanya moja ya dhambi kubwa ya kukilisha maneno chanzo cha habari.
Kwa ajili ya kutunza heshima ya gazeti lako, lakini pia kwa ajili ya maslahi mapana ya taaluma ya habari na jamii ya Watanzania, nakuandikia kulitaka gazeti lako likanushe maneno liliyoninukuu katika toleo hilo la Julai 23, 2012. Ni vyema sana hilo likafanyika kwa uzito unaostahili kama ilivyoandikwa katika toleo hilo.
Habari hiyo imeniletea usumbufu mkubwa hasa kwa wanachama wa chama changu, CHADEMA, ambao wanajua kuwa chama chao makini ni mahiri katika kufuata katiba, kanuni na taratibu katika kuendesha mambo yake kwa manufaa ya watu wote. Napenda kuwa mmoja wa Watanzania makini na viongozi wanaojua wajibu, ikiwemo kufanya nini na kusema nini, mahali gani na wakati gani.

Nakutakia utekelezaji mwema katika hilo.

No comments:

Post a Comment