Wednesday, July 11, 2012

Madiwani 22 wajiorodhesha kuhamia CHADEMA


MADIWANI 22 kati ya 36 wa Chama cha Mapinduzi wilayani Misungwi wamejiorodhesha wakitaka kukihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA.
Taarifa zilizoifikia Tanzania Daima Jumatano jana kutoka Misungwi, zinaeleza kuwa uamuzi huo madiwani umekuja baada ya kukasirishwa na hatua ya Kamati ya Siasa ya mkoa pamoja na ile ya wilayani kumtaka Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Benald Polcarp (CCM ) ajivue gamba bila uthibitisho wowote dhidi ya tuhuma za ufisadi wa fedha za umma zinazomkabili.
Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo zimethibitishwa na baadhi ya madiwani hao, tayari wamekwishajiorodhesha majina yao na kata wanakotoka, kisha dhamira yao hiyo kuipeleka Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma jana.
“Kwanza leo (jana), madiwani hawa walitaka kufanya maandamano kwenda ofisi za CCM wilaya kudai mali zao walizokuwa wakichangia. Lakini waliogopa kuandamana baada ya magari ya FFU kuonekana yakizagaa kwa lengo la kupambana nao,” kilisema chanzo chetu cha habari kutoka Misungwi.
Chanzo hicho kililidokeza gazeti hili kuwa madiwani hao wamechukizwa kitendo cha kamati ya siasa kushindwa kufuata maazimio ya baraza la madiwani la kutaka ufanyike kwanza uchunguzi wa kina juu ya tuhuma hizo zinazomkabili mwenyekiti huyo.
Mmoja wa madiwani hao (jina tunalihifadhi) alilithibitishia gazeti hili na hatua yao hiyo akisema wanajiandaa muda wowote kuihama CCM na kwenda CHADEMA.
Hivi karibuni, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kupitia ripoti yake, aliituhumu Halmashauri hiyo ya Misungwi inayoongozwa na madiwani wa CCM kufuja zaidi ya sh bilioni tano za miradi mbali mbali ya maendeleo.
Baada ya ripoti hiyo ya CAG, Mei 9 mwaka huu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliagiza kushushwa vyeo kisha kukamatwa na kufikishwa mahakamani mkurugenzi wa halmashauri hiyo ya Misungwi, Exavier Tilweselekwa pamoja na Mkurugenzi wa Sengerema, Erika Musika.
Tayari kuna taarifa zinazodai kuwa wakurugenzi hao waliishashushwa vyeo vyao, lakini bado hawajafikishwa mahakamani kujibu tuhuma za ubadhirifu wa mali za umma.
“Tumechoka na mwenyekiti wetu tuliyemchagua sisi madiwani kuandamwa kwa tuhuma za ufisadi bila uthibitisho. Sisi kwenye baraza tuliazimia uchunguzi ufanyike na ikibainika ashtakiwe mahakamani.
“Kwa maana hiyo, tumejiorodhesha madiwani 22 na mwingine yupo wa 23 anataka ajiorodheshe naye kwa lengo la kuhamia CHADEMA. Tumeshapeleka orodha yetu makao makuu ya CCM Dodoma wakaione huko,” alisema diwani huyo kwa njia ya simu yake ya kiganjani.
Alisema, katika waraka wao walioupeleka makao makuu ya CCM, wanamtaka Katibu Mkuu wao aende haraka sana Misungwi ili akakutane nao kabla hawajafikia uamuzi wa kutimkia CHADEMA.
Tanzania Daima inayo majina 15 ya madiwani na kata zao wanakotoka, wakiwemo madiwani wa viti maalumu ambao wamejiorodhesha kwa nia ya kuihama CCM.
Mwenyekiti Polcarp pamoja na katibu wa CCM wilaya hiyo ya Misungwi, Marco Kahuluda, walipotafutwa jana jioni kwa simu zao za viganjani ili kuzungumzia taarifa hizo, simu zao zilikuwa zimezimwa.
Lakini taarifa nyingine zinadai kwamba, tishio la madiwani kuhamia CHADEMA, limechochewa na kigogo mmoja wa halmashauri hiyo kwa lengo la kutaka kukikomoa chama hicho tawala.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment