Sunday, July 29, 2012

DEMOKRASIA KITANZINI


Urais wa Kifalme na Uspika wa Kifalme
HALI ya demokrasia hapa nchini iko njiapanda. Pamoja na tambo za Rais Jakata  Kikwete, chama chake na serikali yake kuwa Tanzania ni mfano wa kuigwa katika uendeshaji wa mambo kidemokrasia, bado haiingii akilini unapoangalia uendeshaji wa Bunge na Serikali.
Wapo wanaojipa matumaini bandia kuwa mchakato wa kuandika katiba mpya unaweza kubadilisha hali hii na kuleta katiba mpya ambayo itaondosha hali hii.
Kwangu mimi, nina mashaka mengi kuliko matumaini kwa sababu hata mchakato wenyewe tayari umeingiliwa na mkono wa dola na chama kuhakikisha ufalme wa rais na ufalme wa spika unaendelezwa.
Sasa makada wa CCM na wakuu wa wilaya wanahaha nchi nzima kupanga watu na kuwapa maoni ya kutoa mbele ya tume ya kuratibu maoni ya katiba mpya. Maoni wanayojaribu kuyaingiza kimagendo yamejaa dhana ya urais wa kifalme na uspika wa kifalme.
Kambi ya upinzani bungeni katika mkutano wa bajeti ya mwaka uliopita ilitamka hadharani kuwa urais wa taifa letu ni kama wa kifalme (imperial presidency).
Hoja ilijengwa na kubainisha kuwa kwa hali ilivyo rais ni kila kitu katika taifa letu na ndiyo maana hata pale anapokuwa dhaifu, kuna wengi wanaoogopa kumlaumu na kuishia kulaumu wasaidizi na washauri wake. Rais wetu anateua, anafukuza, anapandisha vyeo, anashusha vyeo, anaua, anasamehe, anataifisha, anabatilisha haki fulani, anafuta sheria, anakataa kusaini muswada uwe sheria hata kama umejadiliwa na watu wengi, anaunda mkoa na kuufuta akitaka, anatoa uraia na kuufuta, n.k.
Rais huyu huyu ni sehemu ya Bunge lakini kimsingi na kiukweli Bunge ndilo sehemu yake au kwa upana zaidi, rais ndiye Bunge. Katika ukiritimba wa chama tawala ambacho mwenyekiti wake ni rais, spika huteuliwa kwa matashi ya rais na chaguo lake halipingwi na wabunge wake.
Baada ya kumuweka spika huyo, ni hatari kwa spika huyo kutenda au kuamua kinyume na matakwa ya rais. Hata kama rais hana hulka ya kuagiza matashi yake kwa bunge kupitia kwa spika, bado spika mdhaifu atajipeleka mwenyewe kwa rais kuuliza afanye nini.
Jitihada za kulifanya Bunge lijitegemee, zilimtokea puani Samwel Sitta. Mpaka hapa tukubaliane kuwa rais wa kifalme si sehemu ya bunge bali ndiye bunge maana inapobidi huwataka wabunge watende kinyume na dhamiri zao. Hata kama katiba kinadharia inatoa uhuru wa bunge kutenda kinyume na matakwa ya rais, ni katiba ile ile inayotoa uhuru na madaraka kwa rais wa kifalme kulivunja bunge hilo iwapo amebaini kuwa bunge hilo linaasi matakwa yake.
Hapa kwetu Rais ndiye mteuzi wa jaji mkuu, majaji, wasajili wa mahakama zote na watendaji wakuu wa mhimili huo. Ukiweka kando uwezekano wa nidhamu binafsi ya rais kutoingilia mhimili huu katika utendaji wake, uwezekano wa majaji “kuasi” mamlaka iliyowateua katika kufanya maamuzi yao yanayogusa maslahi mapana ya mteuzi na serikali yake ni sawa na kuwafanya majaji kuwa malaika.
Hata inapotokea jaji mmoja au kundi likawa na msimamo huria kuhusu masuala fulani, bado upo uwezekano mkubwa wa kuvuruga mpango huo kupitia mabadiliko ya ndani ya mhimili yanayofanywa na jaji mkuu.
Sitaki kusema zaidi ya hapa lakini itoshe nikisema kuwa kivuli cha rais mfalme kinautesa mhimili huu muhimu kwa utoaji haki hapa nchini. Si siri tena kuwa hata wawakilishi wa huyu rais mfalme katika ngazi za mikoa na wilaya wakati mwingine wanapitiliza na kuiona mahakama katika maeneo yao kama sehemu ya serikali wanayoiongoza kwa njia ya maelekezo na madokezo.
Pale mahakimu wanapokaidi maelekezo hayo, hatua za siri huchukuliwa kuiomba mamlaka ya juu ya mahakimu hao, ili ama waonywe au wahamishwe kutoka katika maeneo hayo.
Pamoja na kwamba wizara ya sheria na ofisi ya jaji mkuu wanaweza kukanusha ukweli huu, shuhuda za mahakimu na majaji walioathirika na mizengwe hii ya watawala wanaomwakilisha rais mfalme hazikanushiki.
Mwisho wa siku ni rahisi kwa jaji au hakimu kukaidi maamuzi ya jaji au hakimu aliye juu yake kiutendaji lakini kamwe hawezi kuwa salama ikiwa kile anachokikaidi kina maelekezo ya rais mfalme.
Mhimili wa Bunge umeleemewa zaidi kwa sababu una wafalme wawili yaani spika na rais. Ufalme wa spika kwa bunge unakera  zaidi kwa sababu ni wa moja kwa moja.
Ukifuatilia Bunge linavyoendeshwa, utaona ni kejeli ya hatari kudai kuna demokrasia katika Bunge letu. Kinachoonekana wazi ni ufalme wa spika aliye na haki, uhuru usio na mipaka, madaraka yasiyochujwa na ulevi usioweza kukemewa na yeyote. Ni spika anayeweza kusema chochote cha ovyo bila uwezekano wa kukiri kosa na kufuta kauli yake. Ni spika aliye na mamlaka ya kutafsiri kanuni bila kupingwa na yeyote. Ni Spika mwenye mamlaka ya kuamuru mbunge afunge mdomo, akae chini, atolewe nje ya lango la bunge na asihudhurie vikao kadhaa vya bunge.
Ni Spika, bila kuwasiliana na yeyote au kushauriwa, anaweza kugoma kuahirisha shughuli mpaka atakaporidhika yeye kuwa kuna dharura. Kipimo cha lipi ni dharura na si dharura ni uamuzi wa spika hata kama kanuni inaweza kusema vinginevyo kwa sababu ya kinachoitwa “busara ya kiti na mila, desturi na utamaduni”.
Vitu hivi havina maandishi popote na kwa hiyo ni spika mwenye uwezo wa kuamua ipi ni mila na desturi nzuri kutegemea na alilala wapi na ameamkia upande upi. Ni spika anayeweza kukashifu, kutukana na kuudhi bila madhara yoyote na kulazimisha ashangiliwe na wabunge wa chama chake.
Madhara ya ufalme wa spika kwa demokrasia hapa nchini ni makubwa sana. Watu wengi wenye nafasi za uenyekiti katika vyombo wanavyoviongoza wanadhani mtindo (style) ya kuongoza vikao vya Bunge unaoonyeshwa na Spika na Wenyeviti wa Bunge, ndicho kiwango mahsusi cha kuendesha vikao.
Kwa kuwa Bunge ni chombo cha juu na cha heshima, wanashawishika kuiga mtindo wa uendeshaji unaoonyeshwa na Spika. Taratibu lakini kwa uhakika, Taifa linatengeneza kizazi cha madikteta wanaodharau fikra za watu wenye maoni tofauti na kuzama katika fikra za kuamini kuwa ukiishakuwa mwenyekiti, una chanjo ya kutofanya makosa ya kufikiri na kuamua. Tabia hii ni kashfa kwa demokrasia yetu.
Kutokana na ufalme wa spika bungeni, athari nyingine za hatari zimejitokeza. Orodha ya athari hizo ni ndefu lakini nitaje baadhi bila kufafanua. Bunge letu limegeuka kuwa kiota cha rushwa pale ambapo kiti kinatumika kunyamazisha wale wanaotaka kukemea tabia hii. Inawezekana sasa unaweza kuonana na kiti ukakiaandaa ili kiwanyamazishe watoa tuhuma.
Kiti kinaweza kuongea kama rais na kama mahakama. Tuhuma za rushwa zaweza kunyamazishwa kwa kisingizio cha usalama au kuingilia mhimili wa mahakama. Maamuzi ya spika ni kama ya kimbingu maana hayana rufaa, na rufaa ikikatwa bado ni yeye atakayeitolea maamuzi.
Tabia hii inachonganisha Bunge na wananchi na inachochea maasi ya wananchi dhidi ya Serikali yao. Mawaziri wazembe wamepata kichaka cha kujificha kupitia ufalme wa spika, na udhaifu wa serikali hauwezi kupata dawa kwa sababu unakingiwa kifua na spika mfalme.
Baadhi ya mawaziri wachache wachapa kazi wanalalamika kuwa tabia hii ya spika haiwasaidii wachapa kazi wala mawaziri wazembe. Mwisho wa siku, uspika wa kifalme ni kitanzi cha demokrasia na ni pepo ya wazembe, wezi, mafisadi na wachumia tumbo.
Kwa kuwa vyombo vingi vya habari vimekuwa vinaandika na kuchambua udhaifu huu wa uendeshaji wa Bunge lakini spika na wenyeviti wananyamaza, haishangazi kuona watu wengi wanamkumbuka Spika aliyepita kwa kujaribu kurejesha heshima ya chombo hiki.
Uamuzi wa kumwondoa ulisababishwa zaidi na udhaifu wa taasisi ya urais. Maamuzi yale yamelifanya Bunge kuwa dhaifu sambamba na serikali.
Msomaji Raia

No comments:

Post a Comment