CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimevuna wanachama wapya 256 waliohamia kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Wananchi (CUF) na Tanzania Labour Party (TLP) katika kata nne za wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu wa Wilaya hiyo juzi Moses Kisenime ilisema kuwa wanachama hao walipokelewa na mwenyekiti wa baraza la vijana la taifa John Heche alipofanya ziara ya siku mbili ya muendelezo wa vuguvugu la mabadiliko ya chama hicho katika jimbo hilo.
Taarifa hiyo ilisema kuwa wanachama hao walitokana na mikutano minne iliyofanyika katika kata ya Ifakara, Mang’ula, Msolwa na Mkamba, ambapo wa CCM 214, CUF wanachama 28 na TLP wanachama 14.
Aidha taarifa hiyo ilisema kuwa Mussa Katanduki ambaye alikuwa Balozi wa Kata ya Mkamba aliamua kuhama CCM kutokana na chama hicho kukosa muelekeo na maadili ya uongozi kwani kimeshindwa kuwaondoa maadui watatu: ujinga, maradhi na umaskini.
“CCM ni chama cha kuja na kauli mbiu tofauti kila unapokuja uchaguzi kwani kinashindwa kutuambia kimetekeleza nini katika utawala wake wa miaka 35,” ilieleza.
Taarifa hiyo ilisema kuwa mratibu wa ziara hiyo Azizi Himbuka aliwahakikishia wanachama kuwa CHADEMA inajipanga vema katika uchaguzi wa vijiji na vitongoji unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni na inatarajia kuibuka na ushindi wa kishindo.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment