CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Kagera kimeisambaratisha ngome ya Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, baada ya kufanikiwa kuwahamisha viongozi na wanachama 80 wa CCM akiwamo kada maarufu, Dk. Benedictor Lukanima.
Viongozi na wanachama hao wa CCM wakiongozwa na Dk. Lukanima, ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe na mtafiti katika Chuo Kikuu cha Norte kilichopo nchini Colombia, walitangaza rasmi kuvua gamba na kuvaa gwanda katika mkutano wa hadhara wa CHADEMA uliofanyika juzi kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Chato mjini, na kuongozwa na Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Kagera, Alfred Mganyizi Rwagatare.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wakazi wa jimbo na wilaya hiyo ya Chato, Wana CCM hao waliohamia CHADEMA walikiponda vikali chama tawala, kwa madai kwamba serikali yake imeshindwa kuwasaidia wananchi kuondokana na kero nyingi, ukiwemo umaskini wa kupindukia unaozidi kuota mizizi hapa nchini.
Baadhi ya viongozi wa CCM waliohamia CHADEMA ni pamoja na Makonzela Phinias ambaye alikuwa mjumbe wa UVCCM na mwakilishi wa mkutano mkuu wa Vijana Mkoa wa Geita, Masunga Maswanzali, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Serikali ya Kitongoji cha Nyasenga, Kijiji na Kata ya Ilemela, Josephat Manyenye ambaye amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM pamoja na Dk. Benedictor Lukanima, ambaye mwaka 2010 alishika nafasi ya pili katika kura za maoni ndani ya chama hicho tawala.
Akihutubia mkutano huo, Mwenyekiti wa CHADEMA wa Mkoa wa Kagera ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama hicho, Wilfred Lwakatare alimrushia kombora zito Waziri Magufuli kwa madai kwamba, kiongozi huyo ameshindwa kuondoa kero nyingi zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo, ikiwamo ya uhaba wa huduma ya maji, afya, elimu na fursa za kiuchumi jimboni humo.
Lwakatare alimuita Dk. Magufuli bingwa wa takwimu aliyeshindwa kuwaletea maendeleo wananchi wake, licha ya kuwa waziri kwa muda mrefu serikalini.
”Magufuli ni bingwa mkubwa wa takwimu. Anaweza kuwaambieni hadi samaki walio na mimba Ziwa Victoria. Lakini ameshindwa kutoa takwimu za wanafunzi wanaokwenda shuleni bila viatu wala ‘yebo yebo’.
”Wakati umefika sasa wananchi wa Chato kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014 na uchaguzi mkuu 2015, pigeni kura za hasira baina ya CCM na huyu Magufuli, kisha kuwachagua viongozi wa CHADEMA kwa maendeleo yenu,” alisema Lwakatare.
Kuhusu bei ya pamba, Lwakatare ambaye amewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini kupitia Chama cha Wananchi (CUF), kabla hajahamia CHADEMA, alisema: “Serikali ya CCM pamoja na Magufuli imeshindwa kuwasaidia wakulima wa zao hili la pamba.”
Kwa upande wake, Dk. Lukanima aliituhumu CCM na serikali kwa kukosa mwelekeo wa kuwatumikia na kuwaletea maendeleo wananchi wake kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
”CCM imekosa mwelekeo. Mimi na usomi wangu huu siwezi kuendelea kuwa ndani ya CCM ambayo naiona haina faida kabisa kwa Watanzania wenzangu. Hivi niwaulize ni yupi mwenye unafuu aliyeshika chuma cha moto na aliyeshika ubao?
”Jibu ni aliyeshika ubao...kwa hiyo njooni tujiunge na CHADEMA kwa ajili ya ukombozi wa nchi hii. Mfano, hapa Chato hakuna fursa za kiuchumi, mashirika yamekufa, huduma za kijamii mbovu, na anayeng’ang’ania CCM ni sawa na usaliti mkubwa wa maendeleo ya taifa hili,” alisema Dk. Lukanima.
Aliwaomba wananchi wa Chato, mkoa na taifa kwa ujumla kukiunga mkono Chama hicho cha CHADEMA, ili kujikomboa na adha mbalimbali zinazolikabili taifa na wananchi wake, na kwamba kilichomsukuma kuhamia chama hicho cha upinzani ni kwenda kuongeza nguvu katika vuguvugu la mabadiliko.
Madiwani 26 CCM watishia kujiunga na upinzani
Katika hatua nyingine, uongozi wa CCM mkoani Mwanza umeanza kuhaha kujaribu kuwazuia madiwani wake 22 kati ya 36 wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi ambao inaaminika walijitangaza kutaka kuhamia CHADEMA.
Taarifa zilizoifikia Tanzania Daima jana, kutoka ndani na nje ya CCM wilayani Misungwi zimeeleza kwamba, viongozi wa CCM wa wilaya hiyo wamekuwa wakifanya vikao vya mara kwa mara na madiwani hao wakijaribu kuwabembeleza ili wasihame.
Hata hivyo, juhudi hizo zinaelekea kugonga mwamba baada ya orodha ya wanaotaka kuhama kuongezeka na kufikia madiwani 26, jambo lililoulazimisha uongozi wa CCM kupitia kwa Katibu wa wilaya hiyo, Marco Kahuluda, kuitisha kikao cha usuluhishi kati ya madiwani hao na chama.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, kikao hicho cha usuluhishi kinatarajiwa kufanyika leo katika Shule ya Sekondari ya Misungwi, nje kidogo ya mji huo, na kwamba uongozi wa chama umepanga kuwaangukia miguuni madiwani hao ili wasifikie maamuzi yao ya kukihama chama.
Julai 10 mwaka huu, jumla ya madiwani 22 wa CCM walidaiwa kujiorodhesha kwa lengo la kukihama chama hicho tawala na majina na sababu za kufanya hivyo yakipelekwa makao makuu ya CCM mjini Dodoma wakimtaka Katibu Mkuu, Wilson Mukama, akutane nao haraka iwezekanavyo ili wawekane sawa.
”Kesho (leo), tumeitwa madiwani wote wa hapa Misungwi na Katibu wa CCM wa wilaya kwenye kikao cha usuluhishi. Maji yamewafika shingoni, wameanza kutubembeleza lakini msimamo wetu upo pale pale kuhamia CHADEMA.
”Acha tukamsikilize na kuchukua posho zao, lakini hatuyumbishwi katika maamuzi yetu. Kama wanataka tubaki wafute maazimio yao ya kamati ya siasa ya wilaya ya kumtaka mwenyekiti wetu, Benald Polcarp ajivue gamba,” alisema diwani mmoja (jina linahifadhiwa).
Hata hivyo, kuna madai kwamba baadhi ya viongozi wa juu wa CCM wamebariki kuhama kwa madiwani hao na kwamba, jana kulikuwa na kikao cha siri kuwajadili madiwani hao ambao inadaiwa wanataka kuondoka na vifaa walivyochangia ndani ya chama.
Madiwani hao wanadaiwa kupinga maamuzi ya vikao halali vya kamati ya siasa ya wilaya na ile ya Mkoa wa Mwanza, ya kumtaka mwenyekiti wa halmashauri hiyo anayetuhumiwa kwa ufisadi wa mamilioni ya fedha za miradi ya maendeleo, kujivua gamba.
Madiwani hao wanataka ufanyike kwanza uchunguzi juu ya tuhuma zinazomkabili mwenyekiti huyo wa halmashauri, kubaini nani hasa alihusika na ubadhirifu huo.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inamtaja mwenyekiti huyo kuhusika kwa namna moja au nyingine katika ubadhirifu wa zaidi ya sh bilioni tano za miradi mbali mbali ya maendeleo kwenye halmashauri ya wilaya hiyo.
Kufuatia tuhuma hizo nzito, Mei 9 mwaka huu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliagiza kushushwa vyeo kisha kukamatwa na kufikishwa mahakamani Mkurugenzi wa halmashauri hiyo ya Misungwi, Exavier Tilweselekwa, pamoja na Mkurugenzi wa Sengerema, Erika Musika.
Tayari kuna taarifa zinazodai kwamba, wakurugenzi hao walikwisha kushushwa vyeo vyao, lakini bado hawajafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo, huku baadhi ya watu wakishinikiza mwenyekiti wa halmashauri hiyo achukuliwe hatua kali za kisheria, kwa vile yeye ndiye msimamizi mkuu wa mali za halmashauri hiyo.
Katibu wa CCM wa wilaya hiyo ya Misungwi, Marco Kahuluda, alipotafutwa jana na mwandishi wa habari hizi ili azungumzie kuhusu kikao hicho cha leo na madiwani wa halmashauri hiyo, alikataa kuzungumzia lolote kwa madai kwamba yupo kikaoni.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment