Tuesday, July 24, 2012

Chadema chalia na wanawake kutokiunga mkono


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoani wa Morogoro, kimesema wanawake ndio kikwazo cha mabadiliko ya mageuzi nchini  na  kuwataka wanaume kuwalazimisha wake zao kukiunga mkono chama hicho hata ikiwezekana kuwatishia kwa talaka.

Chadema kimesema  mikutano mingi ya chama hicho imekuwa ikiungwa mkono na wanaume huku kukiwa na idadi ndogo ya wanawake jambo ambalo ni kikwazo kwa chama hicho.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika jirani la ofisi za Kikosi cha Zima Moto mjini hapa juzi, Katibu wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) Wilaya ya Morogoro, Mercy Maula, alisema wanawake wamekuwa mtaji wa Chama cha Mapinduzi(CCM) katika chaguzi licha ya kundi hilo kukabiliwa na changamoto nyingi.

AlisemA ipo haja kwa wanaume kuwashawishi wake zao kushiriki katika mikutano inayoitishwa na chama hicho ili kuwa na chachu ya mabadiliko bila woga.

“Jitahidini katika mikutano mingine mje na wake zenu na wale wenye girlfriend (rafiki wa kike) waleteni pia ili kutambua madhaifu ya CCM na kujua kwanini Chadema inataka mabadiliko nchini”alisema Maula.

Naye Mhamasishaji wa Chadema Taifa, Steven Daza, alisema chama hicho kinakusudia kufanya maandamano katika mkoa wa Morogoro ya kupinga ugumu wa maisha na kutaka wananchi kuyaunga mkono.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment