Thursday, June 28, 2012

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA THBUB


Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesikitishwa kwa kitendo alichofanyiwa Dk. Steven Ulimboka cha kutekwa, kupigwa na kujeruhiwa vibaya na watu wasiojulikana kilichotokea tarehe 26 usiku, Juni 2012 na kukutwa ametupwa katika eneo la Mabwepande lililoko nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Tume inalaani kitendo hicho cha kinyama kwani kinakwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Kifungu cha 12(2) kinachoitaka jamii kutambua na kuthamini utu wa mtu.
Vile vile kitendo hicho kinakiuka haki ya msingi ya mtu kutoteswa, kutoadhibiwa kinyama na kikatili au kudhalilishwa kama inavyoainishwa katika Ibara ya 13(6)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kifungu cha 5 cha Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu.
Tanzania ni nchi yenye amani na inayofuata sheria na taratibu zake, hivyo kwa sababu yoyote ile ni kosa kumteka na kumtendea mtu vitendo vya kinyama na vya udhalilishaji wa utu wake.
Ili kuwa na jamii yenye utamaduni ambao unakuza, kulinda na kuheshimu haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inaamini kuwa haki lazima itendeke na ionekane kutendeka. Hivyo basi:
1.      Tume inalaani kitendo cha kujichukulia sheria mkononi na matumizi ya nguvu kilichofanywa na kikundi cha watu waliomteka Dk. Ulimboka;
2.      THBUB inalaani vikali vitendo vilivyofanywa na kikundi au taasisi yoyote ambacho kimemnyima Dk. Ulimboka haki yake ya kikatiba ya kuheshimiwa utu wake na kutofanyiwa vitendo vya kinyama na vya kudhalilisha;
3.      Tume inatoa wito kwa wananchi na vyombo vya dola kuheshimu sheria, utawala wa sheria, haki za binadamu na utawala bora;
4.      Tume inatoa wito kwa Serikali kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini waliofanya kitendo hicho cha kinyama, sababu za kufanya kitendo hicho na kuwachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria.
5.      Tume inampa pole sana Dk. Ulimboka na inamuombea kwa Mwenyezi Mungu apate nafuu ya haraka ili aweze kuendelea na maisha yake ya kawaida.

No comments:

Post a Comment