Friday, June 29, 2012

TAMKO LA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) KUHUSU TUKIO LA KUTEKWA KWA DKT. ULIMBOKA NA MGOMO WA MADAKTARI


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAMKO LA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) KUHUSU TUKIO LA KUTEKWA KWA DKT. ULIMBOKA NA MGOMO WA MADAKTARI
Ndugu wanahabari kwanza asanteni kwa kuitikia mwito wetu leo na kwa ushirikiano mnaotoa kwa Watanzania katika majukumu yenu ya kila siku katika kuitumikia jamii. Kuna masuala mawili tungependa kuzungumza mbele yenu leo;
Kwanza; kwa namna ya pekee, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa ya kutekwa, kuteswa na kuumizwa vibaya kwa Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari nchini Dkt. Steven Ulimboka jijini Dar es salaam. 
Tukio hili limetukumbusha mambo mengi ambayo yamekifanya chama chetu kitafakari kwa kina suala zima la mgomo wa madaktari unaoendelea nchini. Kama tulivyowahi kusema mara kadhaa kuwa ni bahati mbaya sana kuwa madaktari wetu ambao kwa hakika ni wachache sana, wanalazimika kutumia haki yao ya kugoma katika kudai maboresho ya msingi kwenye sekta ya afya, jambo ambalo linagharamu maisha ya watu hususani wa kawaida (walalahoi) ambao matibabu yao hutegemea hospitali za umma.
CHADEMA inaamini kuwa moja ya majukumu ya msingi ya serikali yoyote makini ni wajibu wa kulinda haki, mali na usalama wa kila raia na pia kuhakikisha kuwa huduma muhimu za jamii zinapatikana wakati wote kwa nchi nzima. 
Tukio la kutekwa nyara kwa kiongozi wa madaktari, Dkt. Ulimboka, si suala dogo wala la mzaha na haliwezi kuisha kwa MALALAMIKO tu, ya sisi wapinzani, wanaharakati na serikali yenyewe. Hapa ni lazima watu wenye wajibu wa kuhakikisha usalama huo wa raia wawajibike, hasa katika kutuambia ukweli wa nani aliyehusika na UGAIDI huu afahamike na hatua zichukuliwe dhidi yake.
Tukio hili linatukumbusha njama mbalimbali ambazo zimekuwa zinafanywa na serikali dhalimu katika maeneo mengine duniani dhidi ya wapigania haki au wale wote wanaotoa mawazo mbadala dhidi ya watawala. 
Lakini pia katika nchi yetu hii leo, yapo mauaji ambayo yana kila harufu ya serikali, vyombo vyake na chama tawala kuhusika. Mfano mauaji ya kijanaMbwana Masoud, aliyeuawa huko Igunga mwaka Oktoba 2011, baada ya kutekwa na kuteswa.
Mfano mwingine ni mauaji ya Kiongozi wa CHADEMA Kata ya Usa River,Msafiri Mbwambo, huko Arumeru Aprili 2012, viongozi na wanaharakati kubambikiwa mashtaka ya uongo sehemu mbalimbli nchini, kuzingirwa kwaWabunge wa CHADEMA huko Mwanza, kisha wakapigwa na kuumizwa vibaya,wanafunzi wa vyuo vikuu nchini, hususan viongozi wao, kunyimwa haki zao za kusomeshwa na kufunguliwa mashtaka yasiyo na msingi kwa sababu ya misimamo yao katika kudai haki, n.k.

Lakini pia tukio hili linakumbushia matukio ya namna hii ambayo yamehusishwa na vyombo vya dola pamoja na CCM wakati wa chaguzi ndogo katika maeneo mbalimbali mathalani huko Kiteto, Biharamulo na Busanda ambako mpaka leo pamoja na kuwepo kwa viashiria vyote kuwa serikali, kwa maana ya dola ilihusika katika matukio ya namna hii ili kukisaidia CCM kushinda uchaguzi, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa zaidi ya polisi kukalia majalada hayo mpaka leo.

Yote hayo hapo juu yanaimarisha msimamo wetu kuwa ni LAZIMA serikali iwe na jibu la kutekwa, kuteswa na kuumizwa vibaya kwa Dr. Ulimboka.

Na katika hili CHADEMA tunaweka msimamo kuwa serikali haiwezi kuaminika katika kufanya uchunguzi, wala Jeshi la Polisi pia haliwezi kuwa na uhalali wa kufanya hiyo kazi. Mpaka sasa kwa mazingira yaliyopo, serikali ni mtuhumiwa katika tukio la kutekwa, kuteswa na kuumizwa sana kwa Dkt. Ulimboka. Ni kanuni ya msingi sana katika dhana ya uongozi bora, kuwa mtuhumiwa hawezi kujichunguza mwenyewe.

Wakati ambapo Watanzania wote tunaoitakia heri nchi yetu, tukiendelea kumwombea Dkt. Ulimboka katika wakati mgumu wa maumivu makali aliyonayo apone haraka, CHADEMA kinaitaka serikali kutohusika kwa namna yoyote katika uchunguzi wa tukio la Dkt. Ulimboka.

Ili waliohusika wapatikane na kuwajibishwa, tunataka iundwe tume huru, itakayojumuisha watu wanaoaminika kutoka kada mbalimbali, ili ufanyike uchunguzi huru juu ya suala hili ambalo ni dhahiri limeibua taharuki nyingine katikati ya taharuki kubwa ya mgomo wa madaktari ambao unazidi kushika kasi kwa sababu ya serikali kutowajibika ipasavyo kwa wananchi walioiweka madarakani. Kuundwa kwa tume huru kuchunguza matukio au vifo tata kila inapotokea, imekuwa ni rai yetu mara kwa mara ili serikali ioneshe uongozi bora kwa vitendo.

Mbali ya kuwa suala hili linahusu maisha ya binadamu ambayo hayana thamani ya kitu kingine chochote, bado pia ni kitendo kinachozima demokrasia na kuhatarishaamani ya taifa.

Kuhusu mgomo wa madaktari

Ndugu wanahabari suala la pili; lazima sasa mgomo huu wa madaktari unaoendelea umalizike kwa wananchi ambao ndio wanaoathirika, kuingilia kati iliserikali imalize mvutano na madaktari. 
CHADEMA kinaona suala hili kuwa zaidi ya “siasa”. Ni suala linalohusu maisha ya watu. Tunatoa mwito kwa watu wote wenye mapenzi mema kuungana katika kushinikiza mgomo wa madaktari kupatiwa suluhisho la kudumu ili kunusuru maisha ya Watanzania, hasa wasiokuwa na uwezo wa kutibiwa nje ya nchi kama viongozi wao. Dawa ya mgomo huu iko ndani ya uwezo wa serikali; isipokuwa tuhaina nia ya kweli na dhati kutatua tatizo hili kwa manufaa ya wananchi. Kwa kuwa serikali ni ya wananchi na serikali inawajibika kwa wananchi katika masuala yote, ikiwemo kuhakikisha huduma za jamii zinapatikana, ni lazima sasa wenye nchi hawa waoneshe msimamo wao katika suala hili. Tunawaomba Watanzania kusimama kuiwajibisha, ikiwa Serikali ya Rais Kikwete chini ya CCM, itaendelea kupuuza na kufanya mzaha katika suala hili linalohatarisha amani na utulivu wa taifa.
Kama Serikali ya Rais Kikwete itaendelea kupuuza, hata baada ya msimamo wa wananchi wa kuitaka iwajibike kutatua tatizo hili, basi serikali hii itakuwa imeongeza idadi ya viashiria vinavyoikosesha uhalali wa kuongoza.

Ndugu wanahabari, kwa kipekee kabisa tunawasihi Watanzania ambao ndiyo waathirika wakubwa wa mvutano kati ya serikali na madaktari, uliosababisha mgomo unaoendelea, wamtake Rais Jakaya Mrisho Kikwete amalize mgomo huumara moja kuzuia madhara makubwa kwa maisha ya binadamu.

Tunasema hivyo kwa sababu, katika mgomo wa awali, Januari/Februari, baada ya wasaidizi wake, akiwemo Waziri Mkuu Mizengo Pinda kushindwa kuutatua, suala hili lilifika kwa Rais Kikwete, ambaye alikutana, kujadiliana na kufikia mwafaka na madaktari.
Baada ya hapo aliwatangazia Watanzania wote kupitia ‘wazee wa Dar es Salaam’, kuwa mgomo umekwisha. Rais Kikwete aliahidi pia kuwa hakutakuwa na mgomo wa madaktari tena. Sasa tunamtaka Rais Kikwete atoke hadharani tena awaambie Watanzania vitu gani alikubaliana na madaktari, ametekeleza yapi na mangapi ambayo hayajatekelezwa mpaka sasa, kiasi madaktari wameamua kugoma tena,huku wananchi wakiumia. Serikali haiwezi kukwepa kuwajibika kwa madhara yoyote yanayotokea kwa maisha ya binadamu, kutokana na mgomo wa madaktari.
Tunasisitiza huu ni wajibu wa Rais Kikwete kwa Watanzania, kwa sababu wanajua suala hili lilishafika kwake. Kinyume na hapo Watanzania wataendelea kujua wanaye rais wa namna gani katika kusimamia masuala ya msingi yanayoamua hatma yao, mtu mmoja mmoja na kama taifa.

Kwa sababu Mhimili wa Bunge ambao ndiyo mwakilishi wa wananchi, ulipaswa kuwa tegemeo na kimbilio katika kuokoa maisha ya watu, umeonekana kuwa na meno ya plastiki na kushindwa kuwaokoa Watanzania, tunatumia fursa hiikuwataka Watanzania wote watimize wajibu wao wa kuitaka serikali na Rais Kikwete kumaliza mgomo huu.

Ndugu wanahabari mwisho tunasema kuwa Serikali isiyoweza kuwahakikishia wananchi wake usalama na upatikanaji wa huduma zingine muhimu za jamii, mathalani; afya, elimu, maji, umeme n.k, ni serikali inayopoteza uhalali wa kuongoza.

Imetolewa leo Juni 28, 2012 Dar es Salaam na;
Singo K. BensonMkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo-CHADEMA
Kny. Katibu Mkuu 

No comments:

Post a Comment