MADAKTARI 146 wamefukuzwa katika hospitali mbalimbali nchini kutokana na kushiriki mgomo unaoendelea nchi nzima kwa lengo la kuishinikiza Serikali kutekeleza madai yao.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa, madaktari hao walitimuliwa katika Hospitali za Bugando na Sekou Toure mkoani Mwanza na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya na ile ya Rufaa Dodoma.
Wakati Serikali ikichukua hatua hiyo, mgomo huo jana uliendelea katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Ocean Road, Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) za jijini Dar es Salaam, Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na Hospitali ya Rufaa ya KCMC mkoani Kilimanjaro.
Katika kile kinachoonekana kuwaunga mkono wenzao, madaktari bingwa wa MOI, MNH na Ocean Road jijini Dar es Salaam, jana walitangaza rasmi kuingia kwenye mgomo huo hadi madai hayo yatekelezwe.
Madai ya madaktari ni hali bora ya mazingira ya utoaji huduma nchini, ongezeko la mishahara, posho za kufanya kazi katika mazingira magumu, posho za kufanya kazi katika mazingira hatarishi na posho za kuitwa kazini.
Tamko la madaktari hao bingwa, lilitolewa jana na msemaji wao, Dk Catherine Mng'ong'o muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao chao kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Tamko hilo limekuja siku moja baada ya baadhi yao kuanza kushiriki mgomo huo juzi, kushinikiza pamoja na mambo mengine, Serikali itoe tamko juu ya tukio la kutekwa na kujeruhiwa kwa Dk Ulimboka.
Hata hivyo, wakati madaktari hao wakitoa tamko hilo, uongozi wa Moi jana ulitoa tangazo kuwataka madaktari wote walioshiriki mgomo huo kurejea kazini ifikapo Julai 2, mwaka huu, vinginevyo watafukuzwa kazi.
Jana jengo la MOI lilikuwa limefungwa kwa makufuli, huku wagonjwa wakielezwa kuwa huduma zote hazitolewi zikiwamo za dharura ambazo awali ziliendelea kutolewa.
Mmoja wa walinzi aliwambia waandishi wa habari kuwa, amefunga mageti kutokana na amri ya mkuu wake wa kazi.
“Mimi ninatekeleza amri ya bosi wangu, amenitaka kufunga geti na hakuna mtu kuingia, awe mgonjwa au ninyi waandishi wa habari kwa kuwa hakuna huduma zinazotolewa humu,” alisema.
Mkoani Mwanza
Madaktari 63 walio katika mafunzo ya vitendo kazini wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Hospitali ya Mkoa Sekou Toure wametimuliwa na kurejeshwa wizarani kutokana na mgomo huo.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Dk Charles Majinge alisema kuwa, juzi aliwataka madaktari waliokuwa katika mgomo kurejea kazini, lakini hawakufanya hivyo na jana akaamua kuwarejesha 47 wizarani.
Katika Hospitali hiyo ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Valentino Bangi alisema, madaktari 16 wamesimamishwa kufanya kazi kutokana na agizo la wizara.
Kilimanjaro
Madaktari walioko kwenye mgomo katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Moshi mkoani Kilimanjaro walisema jana kuwa, kinachofanywa na Serikali kuwafukuza kazi waliogoma, ni njia mojawapo ya vitisho, lakini wakasema kuwa kamwe hawataogopa.
Madaktari hao ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini walisema, wao wanaendelea na mgomo mpaka pale Serikali itakapotekeleza madai yao.
“Tumesikia wenzetu wa Dodoma na Mbeya wamefukuzwa ….Hiyo haitufanyi turudi kazini na kama Serikali inaona hiyo ndiyo njia ya kumaliza mgogoro huu waendelee sisi tutarudi kazini pale itakapotimiza tunayotaka,” alisema mmoja wa madaktari hao.
Mbeya
Juzi Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, ilitoa tangazo la kuwataka madaktari waliopo mafunzoni waliogoma kurejea kazini jana, na endapo wangekiuka agizo hilo wangekuwa wamejifukuzisha kazi. Na hadi jana jioni hospitali hiyo ilikuwa imewafukuza madaktari 72.
Ocean Road
Katika Taasisi ya Taifa ya Saratani, (Ocean Road), kutokana na madaktari sita kusitisha kutoa huduma tangu Dk Ulimboka alipojeruhiwa kwa kipigo, waligoma na jana Mkurugenzi wa Tiba na Huduma Diwani Musemo alionekana akitembelea wagonjwa.
Dodoma
Madaktari 11 wa mafunzo kwa vitendo katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma nao wamefukuzwa, tukio ambalo jana lilileta usumbufu mkubwa katika upatikanaji wa tiba hospitalini hapo.
“Kwa hakika matibabu yanaendelea ingawa ni katika hali ya kusuasua. Hatuna uhakika kama kweli kuna mgomo wa chinichini au la, maana mimi nimefika mapema, lakini bado sijahudumiwa," alisema mmoja wa wagonjwa waliozungumza na mwandishi wa habari.
Arusha
Katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, huduma zimedorora lakini Mganga Mkuu, Dk Omar Chande alisema jana kuwa, imekuwa ni vigumu kuchukua hatua kuwabana madaktari ambao wanatuhumiwa kufanya mgomo baridi, kwani wote wanaripoti kazini.
"Ni kweli kuna taarifa hizi za kuwapo mgomo baridi, lakini madaktari wote wapo kazini, ila kama kuna kufanya kazi chini ya kiwango, tumeanza uchunguzi," alisema Dk Chande.
Amana
Katika Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam utoaji wa huduma ulisuasua kutokana na mgomo huo jambo lililofanya uongozi kuweka tangazo kwenye Ofisi ya Mganga Mkuu kuwataka watumishi wote ambao hawakuwapo kazini kuanzia Juni 25, 2012 waandike barua za kurejea kazini.
Tangazo hilo pia linawataka madaktari walioko mafunzoni kuandike barua kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia kwa mganga mkuu wa hospitali hiyo.
Habari hii imeandaliwa na Frederick Katulanda, Mwanza, Rehema Matowo, Moshi, Zakhia Abdallah (SJMC), Editha Majura, Israel Mgussi, Dodoma), Victoria Mhagama na Daniel Mwingira, Sam Jacob na Issa lazaro (SJMC, Godfrey Kahango, Mbeya, na Mussa Juma, Arusha.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment