Thursday, June 28, 2012

Kiongozi wa madaktari atekwa, aumizwa ·


 MADAKTARI WAZUSHA VURUGU KUBWA MUHIMBILI
WATU wasiojulikana, juzi usiku walimteka kisha kumpiga na kumjeruhi vibaya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka.
Ulimboka ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi inadaiwa alitekwa na watu hao akiwa na daktari mwenzake aliyetajwa kwa jina la Deo, eneo la Kinondoni, baada ya kupigiwa simu na watu hao.
Kiongozi huyo ameng’olewa meno na kucha na watu ambao hawajajulikana, huku baadhi wakidai ni watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa, na wengine wakisema ni majambazi.
Ulimboka alifikishwa Muhimbili majira ya saa 04:54 asubuhi na kupelekwa moja kwa moja katika Kitengo cha Mifupa (Moi) na kupokewa na Dk. Cuthbert Mcharo.
“Tumempokea Dk. Ulimboka ambaye hali yake si nzuri, tumempeleka katika chumba cha dharura ili kumfanyia vipimo na uchunguzi,” alisema Dk. Mcharo.
Baadhi ya madaktari walishindwa kuhimili na kuangua vilio vilivyoongeza simanzi huku wengine wakisema kauli ya ‘liwalo na liwe’ iliyotolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda imeanza kutekelezwa.
Ulimboka anena
Akizungumza kwa taabu baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk. Ulimboka alisema akiwa na rafiki zake alipigiwa simu na mtu anayemfahamu na ambaye walishawahi kukutana akimtaka wakutane.
Ulimboka alisema mara baada ya mtu huyo kufika walipokuwa, walianza mazungumzo, lakini wakiwa katikati yule mtu aliwasiliana kwa njia ya simu na watu asiowafahamu, na baada ya muda mfupi kabla ya kuagana liliwasili gari moja lenye rangi nyeusi likiwa halina namba.
“Wakashuka watu kama watano hivi wakiwa na bunduki wakawaambia wale wenzangu na yule niliyekuwa naongea naye kuwa wako free (huru), wakaniingiza kwenye gari lao kwa nguvu,” alisema Dk. Ulimboka.
Naye Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Godwin Chitage alisema juzi wakiwa na Dk. Ulimboka walipigiwa simu na mtu wa Usalama wa Taifa (jina limehifadhiwa) akamtaka wakutane usiku huo.
“Walitoka Ulimboka na Dk. Deo wakaenda maeneo ya Kinondoni Stereo walipokutana naye akaanza kupiga simu likaja gari jeusi, wakashuka watu wanne wakiwa na silaha, na kumtaka Dk. Deo aondoke, ndipo yakaanza malumbano kabla ya kumzidi nguvu na kumwingiza kwenye gari kisha kuondoka naye.”
“Tulipopata taarifa kutoka kwa Deo tukaanza kupiga simu ya Dk. Ulimboka ikawa haipatikani tena. Tulienda Oysterbay Polisi kutoa taarifa lakini hatukupata ushirikiano wa kutosha, tukaenda ‘Central’ (Kituo Kikuu) tukaambiwa tusubiri hadi kesho, hapo ilikuwa saa saba tangu saa tano walipomteka.
Alisema asubuhi walipata taarifa kutoka kwa msamaria mwema kwamba Ulimboka amepigwa sana na ametelekezwa kwenye msitu wa Pande, na walifuatilia ingawa anadai walikosa ushirikiano kwenye Kituo cha Polisi Bunju.
“Kitendo alichofanyiwa mwenyekiti wetu kimetufanya kuwa imara zaidi katika kupigania haki zetu. Tutasimama kwa pamoja kwa gharama yoyote hata kama ni kutoa uhai wetu.
“Nawaomba Watanzania wote wanaoitakia amani Tanzania walaani kitendo hiki, tunawalaani wote waliofanya juhudi za kumchelewesha Dk. Ulimboka kufika hospitali ili lengo lao la kumtoa uhai litimie,” alisema Dk. Chitage.
Kauli ya MAT
Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kimelaani kitendo alichofanyiwa Dk. Ulimboka na kusema kimewafadhaisha na kimewavunja moyo katika utendaji kati yao na serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya jengo la MOI alikolazwa Dk. Ulimboka, Mwenyekiti wa MAT, Dk. Namala Mkopi, alisema wamesikitishwa zaidi na kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyoitoa bungeni jana baada ya kuulizwa kuhusu mgomo huo akisema liwalo na liwe.
“Kazi ya MAT ni kulinda na kutetea haki za watumishi wa sekta ya afya hususan madaktari kuhakikisha wanakuwa na mazingira bora ya kazi kwa manufaa ya wananchi,” alisema.
Mkuu wa Polisi Salender apigwa
Katika tukio lisilo la kawaida mtu mmoja anayedaiwa kuwa mkuu wa Kituo Kidogo cha Polisi Daraja la Salender alipata kipigo kikali kutoka kwa kundi la madaktari, baada ya kuhisiwa kuwa ni mmoja wa watu waliohusika kumteka nyara Dk. Ulimboka.
Inadaiwa polisi huyo alichepuka baada ya kumwona Ulimboka, kisha akasikika akizungumza na wenzake kwa njia ya simu kwamba alikuwa (Ulimboka) hajafa.
Ofisa huyo aliokolewa na askari wanaolinda hospitali hiyo na kupelekwa kwenye chumba kidogo kilichopo jirani na lango la kuingilia hospitalini hapo, ambapo baada ya muda polisi zaidi waliwasili wakiwa katika gari lenye namba za usajili T 226 AMV wakiingia na kutoka katika chumba hicho.
Majira ya saa 05:20 asubuhi gari aina ya Toyota lenye namba za usajili T 716 BKZ ililiwasili na kumchukua ofisa huyo ambaye alidai kupoteza “Radio call” na bastola yake katika shambulio hilo.
Kova aunda tume ya uchunguzi
Katika hatua nyingine, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, ameunda tume maalumu ya wataalamu wa jeshi hilo, kuchunguza kwa makini tukio zima la kushambuliwa kwa kiongozi huyo wa madaktari nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kova alisema tume hiyo itaongozwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Ahmed Msangi, na kwamba wahusika watakaokamatwa watafikishwa mahakamani bila kujali ni kina nani.
Akizungumzia kupigwa kwa polisi Muhimbili, Kova alisema waliohusika walitenda kosa baada ya kudhani kuwa ni mmoja wa watu waliohusika kumpiga Ulimboka.
“Huyu alikuwa katika kazi ya operesheni kuwasaka waliohusika na tukio hilo. Na alifika pale kuhakikisha kama kweli amepatikana na ndiyo maana akachepuka pembeni kutuarifu kuwa alikuwa Ulimboka. Sasa wao wakachukua sheria mkononi na kuanza kumshambulia,” alisema Kova.
Kipigo alichopata kiongozi wa madaktari, Dk. Steven Ulimboka na kauli nzito aliyoitoa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu mgomo wa madaktari, vimelivuruga Bunge.
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), ndiye aliyechafua hali ya hewa jana baada ya kutilia shaka kauli ya Waziri Mkuu Pinda na kipigo cha daktari huyo.
Jana asubuhi wakati waziri mkuu akijibu mwongozo wa Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM), aliyetaka kujua msimamo wa serikali kuhusu mgomo huo, alisema  leo serikali itatoa uamuzi mzito kuhusu mgomo wa madaktari na ‘liwalo na liwe.’
Mbunge huyo alisema wakati madaktari walipotoa tishio la mgomo wiki mbili zilizopita, Waziri wa Afya, Dk. Hussein Mwinyi alitoa kauli ya Serikali Juni 22 kwamba Serikali imetekeleza madai ya madaktari na kuongeza posho.
Kwa mujibu wa Zambi, licha ya kauli hiyo, madaktari katika baadhi ya hospitali ikiwamo Muhimbili walianza mgomo.
"Mheshimiwa Spika, leo nimepigiwa simu kutoka Mbeya, Dar es Salaam, Moshi nimeambiwa mgomo unaendelea. Naomba mwongozo wako, hatua gani serikali itachukua kuwaokoa wagonjwa?”
Akijibu mwongozo huo, Waziri Mkuu Pinda alikiri kuwa ni kweli serikali imeenda mahakamani kupinga mgomo huo na mahakama iliwazuia madaktari kugoma na kuwataka watangaze kwenye vyombo kwamba wamesitisha mgomo.
Kwa mujibu wa Pinda, madaktari walikaidi amri hiyo na jana serikali ilikimbilia tena mahakamani na mahakama ilikazia uamuzi wake wa awali.
"Tunafikiri si vizuri kuingilia kazi ya mahakama lakini pia tulidhani madaktari wataheshimu amri ya mahakama.
"Kesho (leo) serikali itatangaza hatua za kuchukua. Maana wakati mwingine Waswahili wanasema ‘liwalo  na liwe,’ alisema Pinda na kushangiliwa na wabunge wote.
CHADEMA yataka tamko
Hata hivyo, kauli ya Pinda imeleta tafrani baada ya wabunge wawili wa CHADEMA, Halima Mdee, ambaye ni Mbunge wa Kawe na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, kutaka maelezo yakinifu kuhusiana na mambo ya kutatanisha katika mgogoro huo.
Mdee alimtaka Waziri Mkuu Pinda kutoa maelezo ya serikali kuhusiana na tukio la kuvamiwa, kutekwa na kisha kupigwa vibaya kwa Ulimboka, ikitiliwa shaka kauli ya kiongozi huyo mkuu wa shughuli za serikali bungeni, aliyedai kuwa sasa ‘liwalo na liwe’.
Mbunge huyo alidai kuwa kauli ya Pinda inaleta mashaka na hisia kuwa serikali inahusika na tukio la kinyama alilofanyiwa Dk. Ulimboka.
Naye Mnyika alisema kukamatwa na kushambuliwa kwa kiongozi wa madaktari, Ulimboka, kutachochea zaidi mgogoro kati ya madaktari na serikali.
“Udhaifu wa serikali kuharakisha kwenda mahakamani kabla ya Bunge kupewa fursa ya kujadili madai ya madaktari na kuisimamia serikali umelifikisha taifa hapa tulipo,” alisema.
Mbunge huyo aliliambia Bunge kuwa serikali inajikanyaga katika sakata hilo kwa sababu imekishitaki Chama cha Madaktari nchini (MAT), lakini iliyotangaza mgomo ni Jumuiya ya Madaktari.
Pia Mnyika aliomba Bunge liruhusiwe haraka kujadili hoja za madai ya madaktari ili kuisimamia serikali kwa mujibu wa ibara ya 63 (2) ili kupitisha maazimio kupata suluhu ya mgogoro huo.
“Waziri Mkuu Mizengo Pinda ametoa maelezo bungeni kuwa kesho tarehe 28 Juni, 2012 serikali itatoa kauli bungeni kuhusu suala la mgomo wa madaktari, hata hivyo kauli hiyo itatolewa kwa mujibu wa kanuni ya 49 (1) hivyo Bunge halitaruhusiwa kujadili kauli husika na hivyo kukoseshwa fursa ya kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi.
Alisema Bunge linakoseshwa fursa ya kusikiliza upande wa pili wa madaktari na wahudumu wengine wa afya ambao walipewa nafasi ya kuwasilisha maelezo na vielelezo vya upande wao kwenye Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii.
Mnyika alidai kumshangaa Naibu Spika, Job Ndugai, kudai kuwa tayari Kamati ya Huduma za Jamii imewasilisha taarifa bungeni wakati wabunge hawajapewa nakala husika na wala haijawasilishwa kwenye Bunge kwa ajili ya kujadiliwa.
“Ikumbukwe kwamba jana tarehe 26 Juni 2012 niliomba muongozo kuhusu kauli za mawaziri kwa mujibu wa kanuni ya 49 (2) na 116, hata hivyo niliruhusiwa kuomba kutoa maelezo kuhusu kauli ya serikali juu ya utekelezaji wa madai ya madaktari na uboreshaji wa masilahi ya madaktari.
Mnyika alisema kuzembea ama kupuuza kuchukua hatua dhidi ya udhaifu uliojitokeza kutaleta madhara zaidi kwa kuwa hata serikali ikichukua hatua za kudhibiti mgomo kwa kutumia vyombo vya dola, madaktari na watumishi wa afya wataendelea na mgomo wa chini kwa chini, hivyo afya na maisha ya wananchi yataendelea kuathirika kwa muda mrefu zaidi.
“Ikiwa wabunge tutaelezwa ukweli na kupewa taarifa kamili tutaweza kuisimamia serikali na kuwaeleza ukweli madaktari kipi kinawezekana na kipi hakiwezekani na nichukue fursa hii kuwaomba madaktari kufanya kila kinachowezekana kuokoa uhai wa wagonjwa katika kipindi hiki kigumu,” alisema Mnyika
Zitto: Sitaki kuamini Tanzania tumefika huko
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, ameeleza kuchukizwa kwake na tukio la kutekwa, kupigwa na kuumizwa vibaya kwa Dk. Ulimboka, akidai mambo kama hayo yanatokea kwenye nchi za kidikteta na kuongozwa kiimla.
“Sitaki kuamini kwamba Tanzania imefikia huko.
Serikali kama mlinzi wa usalama kwa raia ina wajibu kueleza tena kwa haraka ni nini kimetokea kwa kijana huyu msomi na kiongozi wa wataalamu wenzake.
“Nimemuomba Waziri kivuli wa Afya wa CHADEMA kufuatilia suala hili kwa karibu sana ili kuhakikisha kwamba ukweli wote unafahamika. Kamwe hatuwezi kuacha Mtanzania yeyote aonewe, anyanyaswe au akandamizwe eti kwa sababu ya kudai haki yake na za wenzake,” alisema Zitto.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment