Friday, April 27, 2012

Polisi watishia kumkamata Dk Slaa

JESHI la Polisi mkoani Mwanza limesema kuwa litamchukulia hatua za kisheria Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibroad Slaa ikiwemo kumkamata kutokana na kauli zake za uchochezi alizozitoa katika mkutano wake wa hadhara mwishoni mwa wiki iliyopita.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Philipo Kalangi alisema kauli zilizotolewa na Dk Slaa ni za uchochezi ambazo zinaweza kuharibu amani ya nchi.


Mwishoni wa wiki iliyopita katika mkutano wake wa hadhara kwenye Viwanja vya Sahara, Dk Slaa alitoa wiki moja kwa Jeshi la Polisi mkoani hapa kuwakamata wale wote waliohusika na vurugu katika uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Kirumba uliofanyika mwanzoni mwa mwezi huu.


Ilidaiwa kuwa vurugu hizo ambazo zinahusishwa na wafuasi wa CCM, zilisababisha kujeruhiwa vibaya kwa wabunge wa Chadema, Samson Kiwia wa Ilemela na Salvatory Mchemli wa Ukerewe.


Katika mkutano wake, Dk Slaa alisema kama Jeshi la Polisi halitawakamata watuhumiwa na kuwachukulia hatua za kisheria ndani ya siku saba, basi yeye mwenyewe atachukua jukumu la kuwahamasisha wananchi wa Mwanza kuwakamata vijana hao.


Kamanda Kalangi alisema Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi na kusema kuwa kauli za Dk Slaa haziwezi kulilazimisha jeshi lake kufanya kazi kwa matakwa yake.


“Ofisi yangu inafanya kazi yake bila kushurutishwa, mpaka hivi sasa watu 18 wamekwisha kamatwa na kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo ila kuna baadhi ya watu ambao wapo nje kwa dhamana kutokana na kutokuwepo na maelezo ya kujitosheleza,” alisema Kalangi.
 
Alisema hawezi kuwashikilia watu ambao hawana maelezo yoyote na kinachotakiwa ni wananchi kujitokeza na kuandikisha maelezo ambayo yatawaweka hatiani watuhumiwa.


Katika hatua nyingine: Aliyekuwa mgombea wa udiwani kwa tiketi ya CCM, Jackson Masamaki amesema kwamba ametoa maelezo yake Polisi kuhusiana na tukio hilo la wabunge kukatwa mapanga.
 
Alisema hakuhusika kabisa na tukio hilo na hawezi kushiriki unyama huo, akitoa mfano wa Mbunge Machemli kwamba ni ndugu yake.
Baba, watoto wadaiwa kuua mama
Jeshi la Polisi mkoani hapa linawashikilia baba na watoto wake wawili wa kiume kwa madai ya kumuua mama yao.
 
Kamanda Kalangi alidai kuwa mnamo Aprili 24, mwaka huu saa 5:00 usiku katika Kijiji cha Kisesa B, mama huyo, Scolastica Mjangera (58) alikutwa nyumbani kwake akiwa ameuawa baada ya kupigwa na kitu kizito kichwani.


Alisema katika tukio hilo, mume wa marehemu aliyetambuliwa kwa jina la Mgeka Ngapi (75) pamoja na watoto wake wawili John Mgeka (25) na Ndaki Mgeka (18) wanashikiliwa.
 
Kamanda Kalangi alisema taarifa za awali zinaeleza kuwa kabla ya kifo hicho kulikuwa na mgogoro wa kugawana fedha zilizotokana na kuuzwa kwa shamba la marehemu.
 
Alisema marehemu aliuza shamba lake kwa Sh5 milioni ambalo linadaiwa kuwa ni la urithi kutoka kwa wazazi wake. Kamanda huyo alidai kwamba baada ya kupokea fedha hizo, aliwagawia kila mmoja kiasi cha Sh200,000 ambazo walizikataa.


Alisema kuwa baada ya kutokea kwa mzozo katika nyumba hiyo, marehemu alitoa taarifa katika ofisi za Serikali ya Kijiji na kabla kuamuliwa kwa ugomvi huo, marehemu akakutwa ameuawa.


CHANZO - MWANANCHI

2 comments:

  1. Mkamate uone muziki wetu sasa hivi hadi kwa wazazi wako wewe kibalaka wa ccm.

    ReplyDelete
  2. Nyie polisi washamba washenzi,waoga,mnataka vyeo kwa mnyanyasa mtu mnaemwona ni tishio kwa ccm.Sasa hivi utaona moto jaribu kibaraka wa ccm.mnashindwa kuwakamata mawaziri wezi ,epa.mnatafuta vitu hata akili hakuna wewe tunakuweka mbegu.tutakuweka kwenye orodha yetu .Fanya utakavyo sasa.tutashuka toka nje ya nje kuja kufanya mambo hapo.

    ReplyDelete