Thursday, April 19, 2012

CHADEMA kuzoa vigogo CCM


WIMBI la viongozi na makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutimkia upinzani, limeanza kushika kasi baada ya jana diwani mmoja na katibu mwenezi wa UVCCM kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Mjini Dodoma, Diwani wa CCM Kata ya Sombetini jijini Arusha, Alphonce Mawazo, alitangaza kuachana na CCM na kujiunga na CHADEMA kwa madai ya kuchoshwa na uonevu na udharimu wa viongozi wa chama hicho.
Aidha, taarifa za uhakika zimebainisha kuwa baadhi ya viongozi wa CCM kwa siku kadhaa sasa wamekuwa wakifanya mawasiliano na baadhi ya viongozi wa CHADEMA ili kujulishwa taratibu za kujiunga na chama hicho.
Mmoja wa watu waliotajwa kuwa katika maandalizi ya kukihama CCM ni mwenyekiti mmoja wa mkoa wa Kanda ya Ziwa ambaye, amedai kuwa msimamo wake umekuwa ukiwasumbua baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu wa chama hicho.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa kadi mpya ya CHADEMA, Diwani Mawazo alisema kuwa ameamua kuachia nafasi yake na kujiunga na CHADEMA ili aweze kuendeleza harakati zake za kuwatetea Watanzania maskini ambao wananyonywa na viongozi wa CCM.
“Nimeondoka mwenyewe katika CCM , nimeachia nafasi ya udiwani, natangaza kujiunga rasmi na CHADEMA, sijalazimishwa na mtu yeyote wala kuahidiwa kitu chochote, ila mimetambua sehemu muhimu ambayo inaweza kuwa ya sauti ya ukombozi kwa Watanzania ni kupitia katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo.
“Nataka kusema kuwa hakuna kiongozi hata mmoja ndani ya CCM ambaye ana dhamira ya kweli ya kuwasaidia Watanzania na badala yake viongozi wengi ndani ya chama wamekuwa wakijinufaisha wenyewe.
Diwani huyo alidai kuwa viongozi wengi ndani ya CCM wapo kwa jili ya kujinufaisha wao, na kwamba chama hicho kimepoteza matumaini kwa Watanzania kutokana na kutotatua matatizo ya wananchi, ndiyo maana ameamua kuingia katika chama ambacho kinahangaika kutetea masilahi ya watu.
Alisema amekuwa akijengewa chuki na baadhi ya viongozi wa CCM, pale anapojaribu kuwatetea Watanzania ambao ni wanyonge.
Mawazo aliifananisha CHADEMA kama sauti ambayo inawalilia Watanzania wengi maskini ili waweze kuneemeka na rasilimali zilizopo.
Kwa upande wake aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA) akitoa salamu zake kwa waandishi wa habari alisema kuwa kwa sasa CCM kinakaribia kufa.
“Nataka niwaambie kuwa katika Jiji la Arusha mambo ni shwari kabisa na msishangae kusikia hata Lukuvi anatuhunga mkono kwa kuwa mwanachama wetu,” alisema Lema.
Katibu mwenezi UVCCM naye atimka
Kutoka Arusha, Katibu wa Uhamsishaji wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) wilayani Longido, Yohana Laizer naye ametimka na kujiunga na CHADEMA.
Laizer alipewa kadi na Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani hapa, Samson Mwigamba, yenye namba 0445402 baada ya kukabidhi ile ya CCM yenye namba 683025 iliyotolewa Mei 04, 2004 Tawi la Kiserian, Monduli.
Akiongea jana na  waandishi wa habari kwenye ofisi za mkoa za CHADEMA, Laizer alisema kuwa alifikia hatua hiyo ya kujivua uanachama na nyadhifa zote alizokuwa akishikilia baada ya kutoridhishwa na utaratibu wa viongozi kubebana huku wakiwakandamiza wananchi wa kawaida.
Kwa upande wake Mwigamba alimkaribisha Laizer kujiunga na kundi la wapambanaji huku akiwataka wananchi wengine kujitokeza na kujiunga na chama hicho alichodai kuwa kinaendelea kuongeza nguvu kwa ajili ya kushika dola kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Mwigamba alisema kuwa wao kama chama hawataacha kupokea watu wanaotaka kujiunga na CHADEMA ili mradi wawe na sifa za kufanya hivyo, ikiwemo kuhakikisha kuwa wana umri unaozidi miaka 18, akili timamu na wasiwe wanachama wa chama kingine cha siasa.
Alisema kuwa wanaelewa kuwa tatizo haliko kwa mwanachama mmoja mmoja bali ni mfumo wa chama hicho ambao umejikita katika misingi mibovu, ikiwamo kutafuta uongozi kwa kutumia rushwa na hila.
“CCM haiwezi kushinda uchaguzi wowote hapa nchini  bila rushwa na hila kwani wananchi wamechoshwa nayo, maana hakuna jambo la kujivunia walilowafanyia wananchi hivyo inawalazimisha viongozi na wanachama wake kufanya mambo yasiyo halali ili iweze kushinda.
“Hawa wanaoamua kukataa kufanya kazi za kutumwa ndio wanakimbilia huku CHADEMA tufanye kazi ya kupigania wananchi, hivi mtu akiwa mpagani akaenda kanisani au msikitini kutubu na kubadilika watakataliwa eti kwa sababu alishakuwa mpagani?” alihoji Mwigamba.
Alisema kuwa yeye yuko tayari kumpokea hata mwenyekiti wa taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, na hata Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, endapo wataamua kufanya uamuzi wa kubadilika na kujiunga na CHADEMA.
“Lowassa akiamua kuondoka CCM ni lazima atakuwa na sababu za kufanya hivyo, lakini na sisi ni lazima atatueleza juu ya tuhuma mbalimbali za ufisadi zinazoelekezwa kwake, tutamsikiliza, tukimwelewa hatutakuwa na sababu ya kumnyima uanachama,” alisema mwenyekiti huyo wa CHADEMA mkoani hapa.
Hata hivyo, aliwaponda viongozi mbalimbali wa CCM wanaotoa kauli za kumbeza aliyekuwa mwenyekiti wa UVCCM mkoani hapa, James Millya, ambaye alijiunga na CHADEMA wakidai kuwa alikuwa mzigo ndani ya CCM, kwa kuhoji kuwa kama alikuwa ni mzigo kwanini hawakuutua mpaka alipoamua kuondoka yeye mwenyewe.
“Mimi leo niko ndani ya CHADEMA ni kamanda, si kwa mavazi, bali matendo ya kupigania wananchi lakini nikihamia CCM nageuka fisadi kwa matendo, kwani kuna mambo nitayapigania kwa masilahi ya CCM ambayo yatawaumiza wananchi walio wengi,” alisema Mwigamba.

CHANZO - Gazeti la Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment