CHAMA CHA DEMOKRASIA
NA MAENDELEO (CHADEMA)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI NA UMMA
KUHUSU
BAADA YA HUKUMU YA
MAHAKAMA KUU, MASUALA SABA YA MUHIMU; UCHAGUZI HURU NA HAKI NCHINI
Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA), kimepanua wigo wa mjadala wa uhitaji wa taasisi na
mifumo itakayohakikisha nchi inafanya chaguzi huru na haki kwa kuitaka Serikali
kufanyia kazi masuala 7 muhimu, wakati huu inapojiandaa kutekeleza amri ya Mahakama
Kuu ya Tanzania ambayo imefuta vifungu 7(1) na 7(3), vya Sheria ya Taifa ya
Uchaguzi namba 5 ya mwaka 1985, vilivyokuwa vikiwapatia mamlaka wakurugenzi wa
halmashauri nchini kusimamia uchaguzi.
Aidha, CHADEMA kimetoa
rai kwa wadau mbalimbali wa demokrasia na utawala bora ndani na nje ya nchi
kupigania na kusaidia kwa kila njia inayowezekana kutekelezwa kwa masuala hayo
7, kwa sababu mfumo wa uchaguzi huru na haki ni mojawapo ya sifa kuu za
demokrasia duniani zinazodhihirisha mamlaka ya wananchi katika kuamua namna
wanavyotaka kujitawala na kuongozwa.
Pia, taasisi imara na
mifumo thabiti ya chaguzi huru na haki, inaondoa uwezekano wa nchi kutumbukia
katika machafuko kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa mchakato wa uchaguzi
huku pia ikidhibiti mianya ya kuchaguliwa na kuwekwa madarakani mamlaka za
kidikteta zenye kujali na kusimamia maslahi ya wachache badala ya maslahi ya
taifa na matakwa ya wananchi.
Akizungumza
katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika leo Makao Makuu ya CHADEMA,
jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uenezi, Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya
Nje, John Mrema ameyataja masuala hayo 7 ambayo CHADEMA kinaamini ni sehemu
muhimu ya mjadala wa muda mrefu nchini kuhusu hitaji la chaguzi huru na za
haki, kuwa ni pamoja na;
1. Tume
Huru ya Uchaguzi (Tanzania Independent Electoral Commission-TIEC)
2.
Matokeo ya uchaguzi wa rais kupingwa mahakamani
3.
Haki ya mgombea kukata rufaa (na kupata haki yake ya kugombea) anapokuwa
amenyimwa fomu, fomu zake kukataliwa kupokelewa au kutoteuliwa na Msimamizi wa
Uchaguzi.
4. Mfumo usiruhusu
mgombea kupita bila (kupingwa) kupigiwa kura.
5. Mfuko Maalum wa
Fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli za TIEC kusimamia uchaguzi.
6. Maamuzi ya Tume
Huru ya Uchaguzi kuweza kupingwa mahakamani.
7. Kuwepo kwa mgombea
binafsi.
CHADEMA inaweka bayana
kuwa mapendekezo hayo ni kwa ajili ya maslahi ya nchi hasa Watanzania
wanapojiandaa kuelekea kwenye chaguzi mbili muhimu, Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa (2019) na Uchaguzi Mkuu (Rais, Wabunge na Madiwani-2020), ambapo wapiga
kura wanahitaji kuhakikishiwa kuwa karatasi za kura sio tu ziko salama, bali
hazitaangaliwa kama karatasi zingine za kawaida.
"CHADEMA
tunapendekeza iundwe Tume Huru ya Uchaguzi kwa maana ya TIEC, Tanzania
Independent Electoral Commission) ambayo itawekewa utaratibu mpya wa uteuzi
kuwapata wajumbe wake, mathalani katika nchi za Kenya, South Africa, Malawi au
Ghana watu hao wanapatikana kwa kutuma maombi ya kazi na kufanyiwa vetting
(uchambuzi) na mamlaka husika kabla ya uteuzi. Uteuzi uwe huru usiwe chini ya
mtu mmoja ambaye naye anakuwa na maslahi binafsi au ya chama chake wakati wa
uchaguzi. Tunataka wajumbe wa Tume wawe na uhakika wa usalama wanapotimiza
majukumu yao. Muhula wao kazini ujulikane na ulindwe. Masharti yao ya kazi
yajulikane. Mnakumbuka wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, kuna watumishi
waliondolewa kazini katikati ya uchaguzi kinyume cha utaratibu."
"Tunataka TIEC
hiyo iwe na mfuko wake maalum kwa ajili ya kuendeshea shughuli zake badala ya
kupiga magoti kuombaomba Serikali Kuu. Hii inapunguza uhuru wa Tume kwa sababu
inaomba fedha kwa watu ambao inatakiwa kuwasimamia. Mfano mzuri ni huu wa sasa
ambapo Tume ya Uchaguzi haijaandikisha daftari la wapiga kura, kinyume na
maelekezo ya kisheria ambayo yanataka daftari liandikwe mara mbili. Hii ni kwa
sababu tume haina mfuko wake wa fedha zake yenyewe, inasubiri hadi ipewe,"
amesema Mrema.
Aidha, CHADEMA
inasisitiza kuwa hakuna haja ya kuendelea kuwepo na zuio la kutoruhusu maamuzi
ya Tume ya Uchaguzi kuhojiwa mahakamani, kwa sababu iwapo makamishna na watendaji
wa Tume watajua kuwa tume inaweza kushtakiwa na kuhojiwa mahakamani watafanya
maamuzi yao kwa kuzingatia haki ili wasifikishwe mahakamani. "Lakini pia
kama tume ni huru kunakuwa na hofu gani ya kuzuia maamuzi yake kuhojiwa
mahakamani? Maana yake basi hiyo tume isiyohojiwa mahakamani haiko huru."
Huku ikitambua na
kuunga mkono juhudi ambazo zimechukuliwa tayari na wadau wengine kwa kufungua
kesi Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, ambayo tayari imesajiliwa
kwa namba 018/2018, kwa ajili ya kupinga Ibara ya 41(7) inayozuia kuchunguza au
kuhoji matokeo ya uchaguzi Mahakamani, kwa sababu ibara hiyo inakiuka Mkataba
wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, CHADEMA inaweka bayana kuwa ibara hiyo
inapaswa kuondolewa ili mtu yeyote awe na haki ya kuhoji matokeo ya uchaguzi
huo iwapo na ushahidi kuwa ulikuwa na makosa, kama inavyoruhusiwa kupinga
mahakamani matokeo ya uchaguzi wa Wabunge na Madiwani.
Kuhusu uwepo wa
vifungu vya Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kifungu cha 45(2) na
kifungu cha 44 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, vinavyoruhusu mgombea kupita
bila kupingwa ikitokea ameteuliwa peke yake, CHADEMA inapendekeza kuwa ikitokea
mazingira (yasiyokiuka sheria) kuwa mgombea ameteuliwa peke yake, asihesabiwe
au asitangazwe kuwa ameshinda kwa kupita kupingwa bali wananchi wapate fursa na
kutumia haki yao kwa kumpigia kura ya NDIYO au HAPANA. Mbali ya kuwapatia
wananchi haki hiyo na kuona iwapo mgombea anaungwa mkono na wananchi, pia
itaondoa uwezekano wa wagombea wengine kuenguliwa kwa hila kwa kunyimwa fomu,
fomu zao kukataliwa au kutopokelewa au kutoteuliwa kwa makusudi, ili kumsaidia
mgombea fulani apite bila kupingwa kama ambavyo imetokea katika chaguzi kadhaa
hivi karibuni.
CHADEMA pia inataka
kuwepo kwa mfumo wa kisheria utakaohakikisha utekelezwaji wa Ibara ya 21 ya
Katiba ya Nchi, ili kuondokana na vikwazo wanavyowekewa baadhi ya wagombea wa
nafasi mbalimbali hasa wa vyama vya upinzani ambao wamekuwa ama wakinyimwa fomu
za kugombea, fomu zao kutopokelewa (wasimamizi kukataa au kujificha) au
kuenguliwa wakati wa uteuzi huku haki yao ya kugombea ikiishia hapo, bila kuwa
na haki ya kukataa rufaa, kama ilivyotokea wakati wa uchaguzi wa marudio Jimbo
la Korogwe vijijini mwaka jana.
Katika hali ya kupinga
ukiukwaji huo wa Katiba na haki za binadamu, aliyekuwa mgombea wa CHADEMA
katika uchaguzi huo wa marudio Korogwe Vijijini, Bi. Aminata Suguti amefungua
shauri Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, kesi namba 7/2019 iliyoko mbele ya Jaji
Mruma, tayari imetajwa mnamo tarehe 30 Aprili, mwaka huu na itaanza kusikilizwa
Juni 4, mwaka huu. Upande wa mpeleka maombi unaiomba Mahakama kutoa amri kuwa
iwapo mgombea hajateuliwa na msimamizi wa uchaguzi kwa sababu fomu zake
hazikupokelewa, awe na haki ya kukata rufaa. Mahakama pia, iwe na mamlaka ya
kumtangaza mgombea wa namna hiyo kuwa ni mgombea halali wa uchaguzi almuradi
awe amepitia mchakato wa ndani wa chama chake.
Pia, CHADEMA imesema
kuwa ni wakati mwafaka sasa kuwepo na Sheria inayoruhusu mgombea binafsi ili
kutekeleza Katiba ya nchi, jambo ambalo pia litasaidia makundi mbalimbali
katika jamii, ambayo hayahitaji kufungamana na itikadi za vyama vya siasa, kuwa
na uwakilishi katika vyombo vya maamuzi.
CHADEMA imetoa wito
kwa Serikali pamoja na Chama kilichoko madarakani kutokuwa na hofu ya kuweka
mazingira yanayoweka misingi ya taasisi na mifumo imara kwa ajili ya chaguzi
huru na haki, kwa sababu kama chama au serikali iliyoko madarakani imefanya
kazi kama inavyotakiwa itachaguliwa katika mazingira hayo na itakuwa na uhalali
zaidi wa kuongoza wananchi badala ya mfumo wa sasa ambao unatia walakini
chaguzi zinazofanyika nchini, hivyo viongozi wengi wanaochaguliwa wanakuwa na
uhalali wa kisheria lakini si uhalali wa kisiasa (kukubalika au kuungwa mkono
na watu).
Imetolewa leo
Jumapili, Mei 12, 2019 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya
Habari na Mawasiliano
CHADEMA
No comments:
Post a Comment