Sunday, February 25, 2018

BARUA YA CHADEMA KWA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA KUWASILISHA MAELEZO KUHUSU TUHUMA ZA UVUNJIFU WA SHERIA YA VYAMA VYA SIASA NA MAADILI YA VYAMA VYA SIASA

22 Februari, 2018

MSAJILI YA VYAMA VYA SIASA

S.L.P 63010

DAR ES SALAAM


YAH: KUWASILISHA MAELEZO KUHUSU TUHUMA ZA UVUNJIFU WA SHERIA YA VYAMA VYA SIASA NA MAADILI YA VYAMA VYA SIASA

Nakiri kupokea barua yako yenye Kumb: HA.322/362/16/34 ya tarehe 21 Februari, 2018 kichwa cha habari hapo juu cha husika.
Kabla ya kuanza kutoa maelezo naomba kueleza misingi ya Katiba na kisheria kama ifuatavyo;

Kuwa, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 13(1) inasema kuwa watu wote ni sawa mbele ya sheria na kuwa wanayo haki ya kulindwa bila ubaguzi na kupata haki sawa mbele ya sheria.

Kuwa, ibara ya 20 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa haki kwa kila mtu ya kujumuika, kukutana na kuchanganyika na watu wengine na kumpa haki ya kutoa mawazo yake hadharani.
Kuwa, Sheria ya Vyama vya Siasa kifungu cha 11 (1)(a), (4) inatoa haki kwa Vyama vya Siasa kufanya mikutano na maandamano ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Na Kuwa, Maadili ya Vyama vya Siasa kifungu cha 4 (1)(b)(e) kinatoa haki kwa Vyama vya Siasa kutoa maoni yake na kufanya maandamano kwa mujibu wa sheria ya vyama vya Siasa.

Kufuatia barua yako hiyo naomba kutoa maelezo yafuatayo;

(i) Kwamba, Jimbo la Ubungo halijafanya uchaguzi mdogo mwaka 2018 kama ambavyo umeeleza katika aya ya pili ya barua yako. Napenda kukueleza kuwa Tume ya Uchaguzi iliyatangaza Majimbo ya Kinondoni na Siha pamoja na baadhi ya Kata nchini na Jimbo la Ubungo halikuwa miongoni mwa Majimbo hayo.

(ii) Kwamba, Mwananyamala kwa Kopa haipo katika Jimbo la Ubungo kama ambavyo umeeleza katika aya ya pili ya barua yako. Napenda kukueleza kuwa eneo hilo lipo katika Jimbo la Kinondoni ambalo lilitangazwa na Tume ya Uchaguzi kufanya uchaguzi wa marudio.

(iii) Kwamba, kifungu cha 9(2) cha Sheria ya Vyama Siasa ya mwaka 1992 kinatoa masharti kwa Chama kinachoomba usajili wa muda na Chama chetu hakiombi usajili wa muda kwa wakati huu. Na hivyo kukitumia kifungu hicho kama msingi wa kututaka kutoa maelezo kwako ni kukosea kisheria .

(iv) Kwamba, Chama chetu hakikufanya maandamano yoyote katika maeneo uliyotaja ila ni kuwa siku hiyo ilikuwa ya mwisho ya kufunga kampeni katika Jimbo la Kinondoni na kwa wakati huo Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni alikuwa hajatoa barua utambulisho na viapo vya Mawakala wa CHADEMA kinyume na Kanuni za Uchaguzi ambazo zinamtaka kufanya hivyo siku saba kabla ya siku ya uchaguzi; Baadhi ya Mawakala waliokuwa hawajapewa barua za utambulisho na viapo pamoja na viongozi wa Chama waliambatana kwenda ofisini kwake kama ambavyo tulivyofanya kwenda kuonana na Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi tarehe 15 Februari, 2018 kulalamikia pamoja na mambo mengine kitendo cha Msimamizi huyo wa uchaguzi kushindwa kutoa viapo na utambulisho wa Mawakala wa uchaguzi. Napenda kuikumbusha ofisi yako kuwa eneo husika lina watu wengi na hata kama si siku ya kampeni ni ngumu kutuhusisha na wingi huo wa kawaida wa watu wenye shughuli zao na matembezi yetu kuelekea kwa Msimamizi wa uchaguzi.

(v) Kwamba, wakati wa kuelekea kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni Jeshi la Polisi bila ya kujua kinachoendelea walianza kufyatua risasi za moto, vipigo jambo lililopelekea kifo cha mwanafunzi aliyekuwa ndani ya usafiri wa umma pamoja na majeruhi ambao mpaka wakati maelezo haya yanaandaliwa wanachama, wafuasi na wananchi wengine zaidi ya 40 walikuwa wanashikiliwa katika vituo mbalimbali vya Polisi Jijini Dar es Salaam.

(vi) Kwamba siku ya tarehe 22/02/2018 mchana watu 28 ambao ni miongoni mwa waliokuwa wanashikiliwa na jeshi la polisi tangu tarehe 16/02/2018 walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kufunguliwa shitaka la “kusanyiko lisilo halali” na walikana shitaka hilo na mahakama imewapa dhamana .

(vii) Kwamba, hakuna kiongozi, mwanachama au mfuasi wa Chama chetu aliyefanya vurugu ya aina yoyote siku hiyo ya kufunga kampeni za uchaguzi katika Jimbo la Kinondoni. Jambo ambalo linatakiwa kulaaniwa na ofisi yako ni kitendo cha Jeshi la Polisi kuwafyatulia risasi za moto watu ambao hawana silaha na hawafanyi vurugu ya aina yoyote jambo lililopelekea majeruhi na kifo. Aidha, ofisi yako ilitakiwa kuchukua hatua na kulaani kitendo cha Katibu wetu wa Kata ya Hananasif marehemu Daniel John ambaye aliuwawa wakati wa kampeni za uchaguzi wa marudio wa Jimbo la Kinondoni na watu waliokuja kumchukua nyumbani kwake kwa kujitambulisha kuwa ni maafisa wa Jeshi la Polisi.

(viii) Kwamba, hakuna sehemu yoyote kwenye barua yako ambayo umenukuu hotuba au maneno ya Mheshimiwa Freeman A. Mbowe (MB) ambaye ni Mwenyekiti wa Chama chetu ambayo yamekiuka masharti ya Sheria na Maadili ya Vyama vya Siasa. Hivyo ni ngumu kutoa maelezo kwa madai na tuhuma ambazo ni jumuishi kama ambavyo ofisi yako imeona ni busara kutuhumu. Ni vema ofisi yako ikaeleza na kunukuu maneno hayo na ieleze pia kama yalizua taharuki kwa nani na au yamemchochea nani ili iwe rahisi kutoa maelezo.

(ix) Kwamba, katika barua yako hukuainisha mtu au taasisi ambayo imekulalamikia kwa kuudhiwa au kuchochewa na maneno au hotuba aliyotoa Mheshimiwa Mbowe hadi kuchukua hatua ya kututaka kutoa maelezo kwa tuhuma ambazo nimeeleza katika aya iliyotangulia kuwa ni jumuishi na hivyo kuwa vigumu kuzitolea maelezo.

(x) Kwamba, kuna mashauri yanaendelea Mahakamani na Polisi kuhusu jambo hili na jinsi ulivyoandika barua yako ni kwamba tayari umeshaihukumu CHADEMA kukiuka Sheria na Maadili ya Vyama kabla hata shauri/mashauri ya jinai kuhusu jambo hilo hilo halijafika mwisho.

(xi) Ninatambua kwamba Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa kifungu cha 6(1)(b) kinamtaka Msajili wa vyama katika kusimamia maadili hayo anao wajibu wa “kupokea malalamiko yaliyowasilishwa kwake yanayohusu ukiukwaji wa maadili haya na kusikiliza pande zote mbili”. Niweke wazi kuwa katika barua yako hukusema kama ulipokea malalamiko na yalitoka kwa nani na hayakuambatanishwa ili niweze kuyajibu na hatimaye uweze kutuita kama ambavyo kanuni zinataka. Jambo hili limenifanya nione kuwa ofisi yako au wewe mwenyewe umeamua kulalamika na unataka kuchukua hatua kwenye jambo ulilolilalamikia wewe, kulisikiliza na kulitolea uamuzi wewe mwenyewe.

Kwa maelezo hayo napenda kukueleza kuwa Chama chetu kitaendelea kuwa mstari wa mbele kuzingatia taratibu za kisheria na kupaza sauti ya kukemea pale ambapo mamlaka za Serikali zinaposhindwa zenyewe kuzingatia matakwa ya sheria. Ningependa kujua kama ulishawahi kumwandikia barua kumtaka kutoa maelezo Rais John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM kwa kauli yake ambayo aliitoa hadharani kuwa anazuia mikutano ya hadhara mpaka mwaka wa 2020 kinyume cha Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992.

Napenda kukushauri kuwa itapendeza kama hatua zozote unazochukua zitakuwa zinazingatia misingi ya haki kwa Vyama vyote na sio kufumbia macho makosa ya Vyama vingine bila kuwachukulia hatua.

Nimalizie kwa kuitaka ofisi yako iwe na msimamo dhabiti katika kuisimamia utekelezwaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 ikiwemo haki ya vyama kufanya mikutano ya hadhara na maandamano .

Pamoja na salaam za CHADEMA.

……………………

John Mnyika,
Kaimu Katibu Mkuu,
CHADEMA

No comments:

Post a Comment