Tuesday, January 5, 2016

Mbunge amsihi Dk. Magufuli kuingilia sakata la Zanzibar

Mbunge wa Viti Maalum wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Simiyu, Gimbi Masaba, amemshauri Rais Dk. John Magufuli, kuingilia kati mgogoro wa kisiasa Zanzibar.

Masaba amesema hatua ya Rais Dk. Magufuli kuingilia kati suala hilo, kutalinusuru taifa kukosa msaada wa fedha za Bodi ya MCC zaidi ya Dola milioni 472.8 za Marekani
zinazotolewa na Serikali ya Marekani.

Alisema yeye kama Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, bado anayo dhamana na uwezo mkubwa kusaidia suala hilo kufikia muafaka na hatimaye taifa
kuepuka kuingia katika mtafaruku na machafuko yasiyo ya lazima.

Alitoa ushauri huo mbele ya waandishi wa habari mkoani Simiyu mjini Bariadi mwishoni mwa wiki alipokuwa akizungumzia changamoto zinazowakabili
wananchi na mustakabali wa maendeleo ya Mkoa wa Simiyu na taifa kwa ujumla.

Alisema na kutahadharisha kuwa Tanzania iko hatarini kunyimwa msaada huo muhimu kwa maendeleo ya wananchi kufuatia mgogoro huo wa kisiasa Zanzibar.

Mbunge huyo alidai kuwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu Zanzibar, yalionyesha mgombea wa Chama cha
Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, alikuwa ameshinda dhidi ya Dk. Ali Mohammed Shein, lakini Tume ya Uchaguzi Zanziabar (Zec), ilifuta matokeo hayo.

Alisema kufuatia kufutwa kwa matokeo hayo, kumechangia Serikali ya Marekeani kupitia Bodi ya MCC kutishia kutoipatia Tanzania kiasi hicho cha fedha.

Alisema ni wakati muafaka kwa Rais Magufuli kuingilia kati sakata hilo ili wananchi waendelee kuijenga nchi yao kwa amani na utulivu.

“Sababu mojawapo ya Tanzania kunyimwa msaada huo wa kimaendeleo na Marekani, ni pamoja na mgogoro wa kisiasa Zanzibar kwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana," alisema.

Aidha, Mbunge huyo pia alidai kuwa sababu nyingine inayochangia Marekani kukataa kuipatia msaada huo Serikali ya Tanzania, ni Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ambayo alisema licha ya kupitishwa kwa mbinde katika Bunge
la 10 la Jamhuri ya Muungano mjini Dodoma, bado inaendelea kuonekana kuwa kikwazo na mwiba mkali kwa ukuaji wa demokrasia, uhuru wa mawazo na kupashana habari.

No comments:

Post a Comment