Monday, November 16, 2015

KAULI YA UKAWA KUHUSU KUUNGA MKONO USHINDI WA MAALIM SEIF KWENYE UCHAGUZI WA ZANZIBAR






Ndugu Watanzania wenzangu
Kama nilivyo waambia Viongozi Wakuu wa UKAWA walikaa juzi kutafakari hali ya kisiasa nchini na hususan Zanzibar na matukio yaliyoandamana na Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktober mwaka huu.

Wakuu wa UKAWA kwa kauli moja walikariri tamko lao la kumuunga mkono kwa dhati, Mh. Maalim Seif Sharif Hamad kwa ushindi wake dhahiri na kuitaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar imtangaza kuwa Rais wa Zanzibar mara moja.

Viongozi wa UKAWA walilaani vikali uamuzi wa ZEC kufuta uchaguzi halali na wakaonya kuwa mbinu mpya za kutaka uchaguzi urudiwe hazikubaliki na zitahatarisha amani na utilivu Zanzibar.

Viongozi wa UKAWA walimpongeza Maalim Seif na viongozi wote wa CUF Zanzibar kwa busara na ustahimili wao mkubwa na jitihada zao zinazoendelea kulinda amani na utulivu nchini humo.

Kinyume na Tanzania bara, uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa wa wazi na wa amani.

Vyama vyote vya siasa na hata wawakilishi wa Kimataifa walikiri hivyo mpaka pale ilipobainika kuwa CCM inashindwa.

Wakuu wa UKAWA walikataa dhana kuwa uchaguzi ule ule unaodaiwa kufutwa kwa kuwa ulikuwa na mizengwe, ulizaa matokeo halali wa Wawakilishi wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano na ya Urais wa Tanzania lakini batili kwa wajumbe la Baraza la Wawakilishi na Rais wa Zanzibar. Dhana hii haina mantiki yoyote bali ni ubabe wa kisiasa tu.

Haiwezekani chungu kimoja kikapika halali na haramu kwa pamoja. Kwa kigezo cha ZEC kuwa uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa batili basi matokeo yake yote ikiwa ni pamoja na yale ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano pia ni batili.

Hii ina maana kuwa hata ushindi unao-daiwa na Bwana Magufuli, mbali ya kuwa ni matokeo haramu ya wizi kwa kura za Tanzania bara, pia ni batili kisheria kwani hana ridhaa ya watu wa pande zote mbili za Muungano.

Aidha kwa kauli moja Wakuu wa UKAWA walikubaliana kuwa hali si shwari nchini licha ya ukimya wa Wananchi.

Wananchi wanaelewa fika kuwa CCM na Serikali yake wamepora ushindi wao na sasa inaendelea kushinikiza kwa vitisho vya majeshi yenye silaha yanayoranda mitaani ili matokeo ya wizi huo wa waziwazi yakubalike.

CCM na serikali yake wanajua kuwa haikubaliki na hata ifanye vipi haiwezi kushinikiza nafsi za Watanzania.

Kama CCM inadai kuwa imeshinda kwa nini ihitaji majeshi, magari ya washa washa na silaha za vita ili wakubalike? CCM ilitayarisha mkakati wa kuhujumu uchaguzi na ndiyo maana ikanunua magari, na vifaa vya vita kwa mabilioni ya fedha ili kuutisha Umma wakati wananchi wanakufa kwa kukosa dawa na huduma hospitalini.

Kama CCM inadai imeshinda kwa nini wana hofu kubwa mpaka kuhujumu uhuru wa vyombo yva habari, kupiga marufuku mikutano ya kisiasa na kutunyima viongozi wa UKAWA hata fursa ya kuwashukuru Wananchi kwa kutuunga mkono katika safari yetu ya kuleta mabadiliko?

Hii ni aibu kwa taifa letu.

Tuna ushahidi wa kutosha kuonyesha jinsi matokeoa ya Uchaguzi wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano yalivyochakachuliwa na kiasi cha kura zilizoibiwa.

Wakati muafaka tutaweka bayana ushahidi huo ili Watanzania wajue kwa nini UKAWA inasema kwa dhati kuwa haitambui matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi na kwa nini haitashirikiana na serikali ya sasa ambayo ni batili kisheria.

Kama sheria ingeturuhusu tungekuwa mahakamani kupinga uamuzi wa Tume ya Uchaguzi.

Uamuzi huo umetekelezwa tu kwa sababu ya fitna ya sheria mbovu zilizotungwa kuhakikisha kuwa CCM inabaki madarakani milele. Hii lazma tuendelee kuikataa na kuipinga kwa nguvu zetu zote.

UKAWA itaendelea kuwataka Watanzania wakatae matokeo batili ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania Bara na waendelee kuwa watulivu. UKWAWA itaendeleza harakati za kisiasa katika nyanja mbalimbali ili kutekeleza azma ya kuleta mabadiliko ya kweli nchini.

Aidha UKAWA itaendelea kudai Katiba ya Wananchi itakayohakikisha kuwa Tanzania inakuwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Serikali inayowajibika kwa Umma.

Ni wazi kuwa uchaguzi mwingine katika mazingira ya sasa na chini ya Katiba ya sasa hauwezi kuzaa matunda tofauti.

Bila Katiba mpya ya Wananchi, Tanzania haitakuwa na demokrasia na itaendelea kuwa nchi inayotawaliwa kwa mizengwe na udikteta wa CCM.

Asanteni sana.

No comments:

Post a Comment