Friday, November 27, 2015

CHADEMA WASHINDA PINGAMIZI LILILOWEKWA NA RPC MWANZA KUHUSU MAZISHI YA ALPHONSE MAWAZO

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akizungumza na wananchi waliojitokeza nje ya mahamaka juu hatma ya kesi ya Alphonce Mawazo.

Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Lameck Mlacha, ametupilia mbali mapingamizi yaliyowekwa na RPC wa Mwanza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya kesi iliyofunguliwa jana na familia ya Marehemu Alphonce mawazo kuomba tafsri ya mahakama baada ya jeshi la polisi mkoani Mwanza kupiga marufuku mikusanyiko ya kuuaga mwili wa marehemu.

Katika mapingamizi hayo, mwanasheria mkuu wa serikali alidai kuwa mleta maombi ambae ni Baba mdogo wa Mawazo hana uhalali wa kisheria wa kuleta maombi hayo mahakamani kwa kuwa yeye si baba mzazi wa marehemu, na kuwa hajaleta hoja za kubishaniwa kwenye maombi hayo.

Upande wa utetezi unaoongozwa na mawakili John Mallya, James Millya na Paul Kipeja ulijibu hoja hizo kuwa katika hatua hiyo masuala ya kubishaniwa hayana sababu ya kuletwa kwa kuwa ni hatua ya awali sana.

Kuhusu uhalali wa kisheria wa baba mdogo wa marehemu, majibu yalikuwa kwamba baba mdogo kwa kuwa ndiye aliemlea Marehemu Mawazo, anayo mamlaka na uhalali wa kisheria wa kuleta maombi hayo.

Mahakama imekubaliana na hoja za mawakili wa mleta maombi na kuamua kuruhusu kesi ya msingi kufunguliwa kama ilivyoombwa, na kutupilia mbali mapingamizi ya RPC na mwanasheria mkuu.

Upande wa wapeleka maombi utawasilisha maombi ya kesi ya msingi leo hii mchana, kisha utasubiri maelekezo ya Mahakama kuwa kesi hiyo itaanza kusikilizwa lini kisha uamuzi wa kesi hiyo.

Alphonce Mawazo alikuwa ni mwenyekiti wa chadema mkoani Geita kabla ya kuuawa kikatili kwa kukatwa mapanga na mashoka na watu wasiojulikana Novemba 14 mwaka huu katika kijiji cha katoro wilayani Geita

No comments:

Post a Comment