MBUNGE wa Viti Maalum, Cecilia Pareso (CHADEMA) ameihoji serikali na kuitaka itoe maelezo ni hatua gani inachukua ili kuhakikisha inadhibiti upotevu wa nyaraka mbalimbali za watumishi hatua inayosababisha usumbufu wa kushindwa kulipwa madai yao kwa wakati.
Pareso alitoa hoja hiyo jana bungeni alipokuwa akiuliza swali la nyongeza kwa kuitaka serikali itoe maelezo ni kwa nini nyaraka za watumishi zinapotea na kusababisha usumbufu kwa watumishi ikiwa ni pamoja na kuchelewa kulipwa stahiki zao.
“Serikali inatoa kauli gani kuhusu kuwepo kwa usumbufu wa upotevu wa nyaraka za baadhi ya watumishi hususan walimu, je serikali haioni kukosa umakini katika utunzaji wa nyaraka hizo kunawafanya watumishi hao kukosa haki zao kwa muda mwafaka?” alihoji Pareso.
Awali katika swali la msingi la mbunge wa Viti Maalum, Maria Hewa (CCM) alitaka kujua serikali inadaiwa na walimu kiasi gani kwa kila mkoa na ni lini serikali itafuta madeni hayo.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa (Elimu) Kassim Majaliwa alisema kuwa ni kweli kuna upotevu wa nyaraka za watumishi katika halmashauri nyingi na kuwasababishia usumbufu watumishi.
Alisema kuwa Januari 2012 serikali ilitoa sh bilioni 19.2 za madai isiyo mishahara na sh bilioni 25.5 za malimbikizo ya mishahara kulipa walimu walio katika mamlaka za serikali za mitaa kwa madeni yaliyokuwepo yamehakikiwa hadi kufikiwa Novemba 2011.
Majaliwa pia alieleza kuwa kati ya Desemba 2012 hadi Aprili 2013 regista za madeni ya watumishi kwa mikoa yote zinaonesha walimu 12,245 wana madai yasiyo mishahara yanayofikia sh bilioni 8.4 ikiwemo sh milioni 519.4 kwa walimu wa mkoa wa Mwanza.
Aidha Naibu Waziri huyo alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2013/14 serikali imetenga fedha za uhamisho sh bilioni 18.3 ikilinganishwa na sh bilioni 13.3 kwa mwaka 2012/13.
No comments:
Post a Comment