Thursday, September 5, 2013

MAONI YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA SHERIA NA KATIBA, MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA MAREKEBISHO YA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA, YA MWAKA 2013


(Kanuni ya 86(6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2013)

UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Huu ni Muswada wa marekebisho ya pili ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ya Sheria za Tanzania. Kama Bunge lako tukufu litakavyokumbuka, Sheria hii ilifanyiwa marekebisho ya kwanza kwa kupitishwa kwa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Na. 2 ya mwaka 2012, mwezi Februari ya mwaka jana. Mabadiliko hayo ya kwanza yalihusu Sehemu ya Tatu na ya Nne ya Sheria hii, na yalilenga vifungu mbali mbali vinavyohusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba na utekelezaji wa majukumu yake.
Muswada huu wa sasa unalenga kufanya marekebisho katika Sehemu ya Tano ya Sheria inayohusu ‘Kuitisha Bunge Maalum.’ Sambamba na mapendekezo haya, kuna mapendekezo ya kufanya marekebisho katika Sehemu ya Sita kwa kufuta vifungu vya 32 hadi 36 vya Sheria vinavyohusu utaratibu wa kura ya maoni kwa ajili ya kuhalalisha ‘Katiba Inayopendekezwa.’ Marekebisho haya yamewekwa katika aya ya 57 ya Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni, 2013. Mapendekezo ya Muswada huu ni muhimu lakini yana utata mkubwa.
Mheshimiwa Spika,
Katika kutekeleza majukumu yake ya kuuchambua Muswada huu, Kamati ya Bunge lako tukufu ya Katiba, Sheria na Utawala ilikutana na wadau wengi mbali mbali. Hivyo, kwa mfano, Kamati ilipata maoni ya taasisi za kidini na za kiraia; taasisi za elimu ya juu na za kitaaluma; vyama vya siasa na asasi nyingine. Kwa sababu ambazo Kamati haikuelezwa vizuri na uongozi wa Bunge hili tukufu, mapendekezo ya Kamati kwenda Zanzibar kwa lengo la kukusanya maoni ya wadau wa Zanzibar juu ya Muswada huu muhimu kwa mustakbala wa Jamhuri ya Muungano yalikataliwa.
Kwa maana hiyo, ni muhimu Bunge lako tukufu lifahamu ukweli huu kwamba wadau pekee walioshirikishwa kutoa maoni yao juu ya Muswada ni Watanzania Bara tu. Wazanzibari hawakupatiwa fursa hiyo na hawakushirikishwa kabisa, licha ya Sheria yenyewe kuwa na mambo mengi yanayoihusu Zanzibar. Kwa vile wadau wa Zanzibar walishirikishwa kikamilifu kutoa maoni yao kuhusu Muswada uliopelekea Sheria hii kutungwa mwaka 2011, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni kwa nini uongozi wa Bunge na wa Serikali umeona si busara na sahihi kuwapatia Wazanzibari fursa ya kutoa maoni yao kuhusu Muswada huu wa kurekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo inawahusu pia Wazanzibari na nchi yao.
URAIS WA KIFALME KWA MARA NYINGINE TENA!!!!
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imepigia kelele jitihada za serikali hii ya CCM kudhibiti mchakato wa Katiba Mpya kwa kuendeleza kile tulichokiita miaka miwili iliyopita, “... kivuli kirefu cha Urais wa Kifalme katika mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.[i] Hapo tulikuwa tunazungumzia mamlaka ya Rais ya uteuzi wa Wajumbe na watendaji wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na tulisema kwamba mamlaka hayo yalikuwa na lengo moja tu: “kuhakikisha kwamba matokeo ya kazi ya Tume hiyo ni yale tu yanayotakiwa na Rais na Serikali yake na chama chake cha CCM.

Mheshimiwa Spika,
Katika Maoni yetu wakati wa kutungwa kwa Sheria hii mwezi Novemba mwaka 2011, Kambi Rasmi ya Upinzani ilipinga vikali mapendekezo ya kumwezesha Rais kuteua Wajumbe wa Bunge Maalum wasiotokana na Bunge lako tukufu na Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Tulisema yafuatayo kuhusiana na jambo hili: “... wajumbe ... wanaopendekezwa kuteuliwa kwenye Bunge la Katiba kwa mujibu wa ibara ya 20(2)(e) na (4) ya Muswada Mpya sio, na hawawezi kuwa, wawakilishi wa wananchi. Kwanza, hawajachaguliwa na mtu yeyote na wala taasisi zao kuwawakilisha katika Bunge la Katiba kwa sababu Muswada Mpya unapendekeza wateuliwe na Rais.
Kwa sababu ya upinzani huo, mapendekezo ya kumfanya Rais kuwa mteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum wasiokuwa wabunge na Wawakilishi yaliondolewa katika Muswada huo wa Sheria hii. Badala yake, kifungu cha 22(1)(c) cha Sheria iliyotungwa na Bunge lako tukufu kiliweka wazi kwamba “wajumbe mia moja sitini na sita [watateuliwa] kutoka ...” taasisi zilizotajwa katika kifungu hicho.
Mheshimiwa Spika,
Ni kweli kwamba kifungu cha 22(1)(c) kama kilivyotungwa kilileta giza badala ya mwanga katika suala la uteuzi wa wajumbe hao. Kama tulivyoieleza timu ya wataalamu wa Serikali kufuatia mkutano wetu na Rais Jakaya Kikwete uliofanyika Ikulu tarehe 26 Novemba, 2011: “Toleo la Kiswahili la Sheria linasema kwamba wawakilishi wa makundi mengine ‘watakaoteuliwa kutoka’ kwenye makundi yaliyoorodheshwa. Toleo la Kiingereza linasema wajumbe hao watakuwa ‘drawn from’ (kwa tafsiri ya Kiswahili ‘watachukuliwa kutoka’). Maana za maneno haya hazifanani na wala hayako wazi kuhusu nani ‘atakayewateua’ au ‘kuwachukua’ wajumbe hao kutoka kwenye taasisi zao.[ii]
Kwingineko katika mkutano wetu na Rais Kikwete tulimweleza kwamba: “Wajumbe 166 wengine wanaowakilisha taasisi nje ya Wabunge na Wawakilishi hawajachaguliwa na mtu yeyote na wala na taasisi zao kwani Sheria haisemi ni nani atakayewateua na/au kuwachagua.” Kwa sababu hiyo, tulipendekeza kwamba “Sheria iweke wazi kwamba wajumbe hawa ‘watateuliwa na’ taasisi zilizotajwa. Hii itaondoa utata juu ya uwakilishi wao na juu ya mamlaka yao ya uteuzi.[iii]

Bonyeza Read More Kuendelea

Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo ya marekebisho yaliyoko kwenye Muswada huu yanaonyesha wazi kwamba ushauri wetu kwa Rais Kikwete na kwa timu yake ya watalaamu umepuuzwa. Badala yake, serikali hii sikivu ya CCM imeamua kuturudisha nyuma kwa zaidi ya miaka miwili kwa kuibua tena pendekezo la kumfanya Rais kuwa mteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum wasiotokana na Wabunge au Wawakilishi wa Zanzibar. Hii ni kwa sababu aya ya 3 ya Muswada inapendekeza kwamba wajumbe hao sasa wateuliwe Rais. Hiyo ni sawa na kusema kwamba kilichokuwa hakifai miaka miwili iliyopita sasa kinafaa; na kilichokataliwa wakati ule sasa kinakubalika!
Ili kuficha ukweli kwamba mwenye mamlaka ya uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum wasiokuwa Wabunge au Wawakilishi ni Rais, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, Muswada unapendekeza kuongezwa kwa vifungu vidogo vipya viwili katika kifungu cha 22. Kwanza, inapendekezwa kuwe na kifungu kidogo cha (2A) ambacho kitamruhusu Rais kualika kila kundi lilioainishwa katika kifungu kidogo cha 1(c) “kuwasilisha kwake orodha ya majina ya watu wasiozidi watatu ili kuteuliwa kuwa wajumbe.” Pili, inapendekezwa kuwe na kifungu kidogo cha (2B) kitakachomlazimu Rais kuzingatia sifa na uzoefu wa watu waliopendekezwa, na usawa wa jinsia wakati wa kufanya uteuzi wa wajumbe hao.
Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo ya kumpa Rais mamlaka ya kuteua wajumbe wa Bunge Maalum hayakubaliki na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaliomba Bunge lako tukufu lisiyapitishe kuwa Sheria. Kwanza, mapendekezo haya yanarudisha dhana kwamba wajumbe hawa watakuwa watu wa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM. Rais Kikwete na chama anachokiongoza ni wadau wakubwa wa mchakato wa Katiba Mpya na wana maslahi halisi na makubwa ya kuhakikisha kwamba matakwa ya chama chao ndio yanakuwa Katiba Mpya ya nchi yetu.
Ushahidi wa maslahi haya ya CCM ni kile kinachoitwa Ufafanuzi Kuhusu Rasimu ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Wanachama na Viongozi wa CCM uliotolewa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM tarehe 10 Juni, 2013. Katika Ufafanuzi huo, CCM imekataa mapendekezo yote muhimu yaliyoko kwenye Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume. Needless to say, Rais Kikwete ni Mwenyekiti wa vikao vyote vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Kumpa Rais, na Mwenyekiti wa CCM Taifa, mamlaka ya kuteua wajumbe wa Bunge Maalum litakaloijadili – na kuikubali au kuikataa – Rasimu ya Katiba ambayo chama chake kimekwishaikataa ni sawa na kuipa CCM fursa nyingine ya kujaza Bunge hilo na makada wake kwa lengo la kutekeleza matakwa ya chama hicho.
Pili, hata bila wajumbe hawa kuteuliwa kwa namna inayopendekezwa, tayari CCM peke yake ina zaidi ya 72% ya wajumbe wote wa Bunge Maalum wanaotokana na Wabunge na Wawakilishi. Kumpa Mwenyekiti wa CCM mamlaka ya kuteua wajumbe wengine zaidi, kama inavyopendekezwa katika Muswada huu, ni kutoa mwanya kwa CCM kutumia kivuli cha makundi ya kiraia, taasisi za kidini na makundi mengine ili kujiongezea wajumbe wengine zaidi, na hivyo kuhakikisha kwamba Bunge Maalum litatekekeleza matakwa ya kuendeleza status quo.
Kwa maneno mengine, Serikali hii ya CCM na Wabunge wake inataka Mwenyekiti wao wa Taifa ayachagulie makanisa na awachagulie Wakristo wawakilishi wao katika Bunge Maalum; awachagulie Waislamu wa BAKWATA, Baraza Kuu, JUMAZA na taasisi nyingine za Kiislamu wawakilishi wao katika Bunge hilo; avichagulie vyama vya siasa vinavyoipinga CCM wawakilishi wao; awachagulie wafanyakazi, wakulima, wafugaji, wahadhiri, wanafunzi, wafanyabiashara, walemavu na makundi mengine ya kijamii wawakilishi wao katika Bunge Maalum! Kama ni hivyo, hilo halitakuwa Bunge Maalum la Watanzania, bali litakuwa Bunge Maalum la CCM na Mwenyekiti wao. Hili halikubaliki kwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na, tunaamini, halitakubalika kwa wananchi wa Tanzania katika ujumla wao.
Tatu, kwa jinsi yalivyo kwa sasa, mapendekezo haya hayawezi kutekeleza matakwa ya kifungu cha 22(1)(c) cha Sheria kinachotaka wajumbe wa Bunge Maalum wasiotokana na wabunge au wawakilishi kuwa mia moja sitini na sita. Hii ni kwa sababu, hata kama watu wote waliopendekezwa na makundi yaliyoainishwa na kifungu hicho watateuliwa kuwa wajumbe, bado idadi yao itakuwa wajumbe ishirini na saba kwa kuwa makundi yenyewe yako tisa tu! Muswada uko kimya juu ya wajumbe wengine mia moja thelathini na tisa watatoka wapi na watateuliwa na nani na kwa utaratibu upi.
Kuna hoja kwamba utaratibu wa uteuzi wa wajumbe unaopendekezwa na Muswada unafanana na uteuzi wa wajumbe wa Tume ulioko kwenye kifungu cha 6(6) cha Sheria ambapo Rais alialika vyama vya siasa, jumuiya za kidini, asasi za kiraia, n.k., kuwasilisha orodha ya majina ya watu ili kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume. Hoja hii sio sahihi. Kwanza, Tume ya Katiba sio sawa na Bunge Maalum. Tume ni chombo cha kitaalamu chenye majukumu ya kitaalamu ya kukusanya maoni ya wananchi, kuandaa ripoti pamoja na Rasimu ya Katiba. Uhalali wa Tume unatokana na utaalamu wa wajumbe wake na weledi katika kutekeleza majukumu yao ya kitaalamu.
Kwa upande mwingine, Bunge Maalum ni chombo cha uwakilishi ambacho wajumbe wake wana majukumu ya kisiasa ya kuwakilisha wananchi wa makundi mbali mbali kwenye kazi ya kisiasa ya kuandika Katiba Mpya. Uhalali wa Bunge Maalum unatokana na upana na ubora wa uwakilishi wake wa makundi mbali mbali ya kisiasa na kijamii. Chombo cha uwakilishi cha aina hii lazima kitokane na wananchi na/au makundi ya kijamii kinachoyawakilisha ili kiwe na uhalali wa kisiasa. Dhana ya Rais – na Mwenyekiti wa CCM – kuteua Wajumbe wa Bunge Maalum inavuruga au kuondoa kabisa dhana ya uwakilishi wa wananchi na uhalali wa kisiasa katika mchakato wa Katiba Mpya.
Pili, kumpa Rais mamlaka ya kuteua wajumbe wasiokuwa Wabunge au Wawakilishi wa Zanzibar kunaleta dhana ya ubaguzi. Hii ni kwa sababu, Rais hana mamlaka ya kuteua wajumbe wa Bunge Maalum watakaotoka kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Hawa wataingia katika Bunge Maalum kwa mujibu wa nafasi zao Bungeni au katika Baraza na sio kwa fadhila ya Rais. Swali la kujiuliza hapa ni kwa nini Rais awe na mamlaka ya kuteua wajumbe wasiokuwa Wabunge au Wawakilishi wakati hana mamlaka hayo kuhusu Wabunge na Wawakilishi? Needless to say, ubaguzi huu unaenda kinyume na matakwa ya ibara ya 13(2) ya Katiba ya sasa na, kwa hiyo, haukubaliki.
Tatu, uteuzi wa wajumbe wa Tume uliofanywa na Rais na ambao unatumiwa kama mfano wenyewe ulikuwa na walakini kubwa. Katika hili, kuna ushahidi wa wawakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza la Kikristo Tanzania (CCT) na asasi mbali mbali za kiraia zikiwemo za walemavu waliowasilisha maoni ya taasisi zao kwa Kamati juu ya Muswada huu. Wawakilishi hao waliiambia Kamati kwamba ijapokuwa waliandikiwa na Rais kuwasilisha majina ya wajumbe wao kwa ajili ya kuteuliwa kwenye Tume, na walifanya hivyo, hakuna hata moja ya majina waliyopendekeza aliyeteuliwa na Rais kuwa wajumbe wa Tume.
Badala yake, Rais aliteua watu aliowaona yeye na washauri wake wanafaa. Kama taarifa za wadau hawa ni za kweli maana yake ni kwamba Rais na Mwenyekiti huyu wa CCM Taifa hawezi kuaminika tena kuteua wajumbe halisi wa taasisi hizi katika Bunge Maalum ambalo ndilo litakalojadili na kuipitisha – au kuikataa - Rasimu ya Katiba Mpya ambayo tayari CCM na wapambe wao wametamka wazi kwamba wanaikataa!
WAJUMBE WA BUNGE MAALUM WAONGEZWE
Mheshimiwa Spika,
Ili kutatua mkanganyiko huu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza Bunge lako tukufu lirejee na kukubali mapendekezo yetu kwa Timu ya Wataalamu wa Serikali ya Januari mwaka jana:
Ø “Sheria iweke wazi kwamba wajumbe hawa ‘watateuliwa na’ taasisi zilizotajwa. Hii itaondoa utata juu ya uwakilishi wao na juu ya mamlaka yao ya uteuzi;

Ø “Sheria itaje kwamba idadi ya wajumbe wa Bunge Maalum watakaotokana na kila taasisi iliyoorodheshwa katika kifungu cha 22(1)(c) itakuwa 354 kama walivyoorodheshwa hapa chini:
(a)           “Asasi zisizokuwa za kiserikali zilizotajwa katika aya (i) zifafanuliwe kuwa ni makundi yanayounganisha asasi hizo, yaani, ANGOZA, TANGO, TACOSODE na Jukwaa la Katiba na kila moja ya makundi hayo itakuwa na wajumbe watano kwa jumla ya wajumbe 20;
(b)           “Asasi za kidini zilizotajwa katika aya (ii) zifafanuliwe kuwa ni makundi yanayounganisha asasi hizo, yaani, BAKWATA, Baraza Kuu, JUMAZA, TEC, CCT na PCT na kila moja ya makundi hayo itakuwa na wajumbe watano kwa jumla ya wajumbe 30. Aidha, Waadventista wa Sabato (SDA), Hindu, Shia Ithnaasheri na Sikh watakuwa na mjumbe mmoja mmoja, kwa jumla ya wawakilishi 35 wa taasisi za kidini;

(c)           “Vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu vilivyotajwa katika aya (iii) vitakuwa na wajumbe 72 watakaogawanywa katika makundi mawili: 1) vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu vitakuwa na wajumbe 42 ikiwa ni wajumbe wawili kwa kila chama; 2) vyama vya siasa vyenye uwakilishi Bungeni vitakuwa na wajumbe 30 ikiwa ni CCM 18, CHADEMA 7, CUF 3 na NCCR-Mageuzi, TLP na UDP 3 kwa ujumla wao. Hii ni kufuatana na uwiano wa kura zote za Wabunge ambazo vyama hivyo vilizipata kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2010;

(d)           “Taasisi za elimu ya juu zilizotajwa katika aya (iv) zifafanuliwe kuwa ni vyuo vikuu 28 vinavyotambuliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na vyuo vya elimu ya juu 16 vinavyotambuliwa na Baraza la Elimu ya Ufundi la Taifa (NACTE). Taasisi hizi zitakuwa na mjumbe mmoja kwa kila moja kwa jumla ya wajumbe 44;

(e)           “Taasisi za elimu ya juu zinahusisha pia vyama vya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu ambavyo vitakuwa na mjumbe mmoja mmoja kwa chama cha wanafunzi kwa jumla ya wajumbe 44;

(f)  Taasisi za elimu ya juu zinahusisha pia vyama wahadhiri/wakufunzi wa vyuo vya elimu ya juu ambavyo vitakuwa na mjumbe mmoja mmoja kwa kila chama kwa jumla ya wajumbe 44;

(g)           “Makundi yenye mahitaji maalum yaliyotajwa katika aya (v) yafafanuliwe kuwa ni mashirika yanayowakilisha wenye ulemavu wa macho, ngozi, viziwi/bubu, viwete na walemavu wa aina nyingine ambayo yatakuwa na wajumbe 10 kwa ujumla wao;

(h)           “Vyama vya wafanyakazi vilivyotajwa katika aya (vi) vifafanuliwe kuwa ni vile vilivyosajiliwa na vitakuwa na wajumbe 40 ikiwa ni wajumbe wawili kutoka kila chama cha wafanyakazi kilichosajiliwa;

(i)   “Jumuiya ya wakulima iliyotajwa katika aya (vii) itakuwa na wajumbe 10 watakaotokana na vyama vya wakulima wa mazao kama vile pamba, kahawa, korosho, chai, katani, karafuu, miwa na wavuvi;

(j)   “Jumuiya ya wafugaji iliyotajwa katika aya (viii) itakuwa na wajumbe 10 watakaotoka Baraza la Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya Wafugaji na Wawindaji/wakusanya matunda ya porini (PINGOS Forum);

(k)“Vikundi vingine vya watu wenye malengo yanayofanana vilivyotajwa katika aya (ix) vifafanuliwe kumaanisha Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Chama cha Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC); Chama cha Wafanyabiashara ya Madini na Nishati (TCME); vyama/mashirika ya wachimbaji madini wadogo wadogo; Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOWAT), Chama cha Waandishi Habari/Jukwaa la Wahariri Tanzania, Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Chama cha Mawakili Zanzibar (ZLS), Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET) na Chama cha Wakandarasi Tanzania (CATA). Makundi haya yatakuwa na wajumbe wawili kwa kila moja kwa jumla ya wajumbe 26.”

Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa kifungu cha 22(1) cha Sheria kama ilivyo sasa, Bunge Maalum litakuwa na jumla ya wajumbe 604, yaani Wabunge 357, Wawakilishi 81 na wajumbe 166 wanaowakilisha makundi mbali mbali. Mapendekezo haya ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni yatafanya uwakilishi katika Bunge Maalum kupanuka hadi wajumbe 792 kwa Tanzania yenye idadi ya watu milioni 45 kwa takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.
Hili, kwa vyovyote vile, ni ongezeko kubwa la wajumbe wa Bunge Maalum. Hata hivyo, ukubwa huu unaopendekezwa hauna tofauti kubwa sana na Mabunge Maalum ya nchi nyingine ambazo zimekamilisha utungaji wa Katiba Mpya kwa kutumia utaratibu huu. Kwa mfano, Bunge Maalum la Jamhuri ya Nepal la mwaka 2011 lilikuwa na wajumbe 601 kwa nchi yenye idadi ya watu milioni 26; Bolivia (2009) lilikuwa na wajumbe 255 katika nchi yenye watu milioni 9; Kenya (2005) lilikuwa na wajumbe 629 kwa idadi ya watu milioni 31; Eritrea (1997) lilikuwa na wajumbe 527 kwa idadi ya watu milioni 3.2, wakati Bunge Maalum la Ufaransa ya Mapinduzi ya 1789 lilikuwa na wajumbe 1145 katika nchi iliyokuwa na idadi ya watu milioni 28.[iv]
Kikubwa na muhimu zaidi, kwa mapendekezo haya, ni kwamba Bunge Maalum la Katiba litakuwa na sura ya Kitanzania zaidi badala ya utaratibu wa sasa unaolifanya Bunge Maalum kuonekana la kiCCM zaidi. Kwa kuongezea tu, Mheshimiwa Spika, wadau karibu wote waliotoa maoni yao kwenye Kamati walipendekeza kuongezwa kwa idadi ya wajumbe wa Bunge Maalum. Kwa kigezo chochote kile, kwa hiyo, mapendekezo haya ni ya kidemokrasia na tunaliomba Bunge lako tukufu liyaunge mkono ili kuiwezesha nchi yetu kujipatia Katiba Mpya yenye sura halisi ya kitaifa kuliko inavyopendekezwa sasa.
UWAKILISHI WA ZANZIBAR KATIKA BUNGE MAALUM
Mheshimiwa Spika,
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekwishatoa Rasimu ya Katiba kwa mujibu wa kifungu cha 19(1)(d) cha Sheria. Rasimu hiyo imepndekeza mabadiliko makubwa katika muundo wa Jamhuri ya Muungano kwa kupendekeza muundo wa shirikisho lenye serikali tatu. Baada ya kukamilika kwa mchakato wa kutoa maoni juu ya Rasimu hii kwa mujibu wa kifungu cha 18, Tume itawasilisha ripoti kwa Rais na kwa Rais wa Zanzibar kwa mujibu wa kifungu cha 20(1). Baada ya hapo, Rais, “... atachapisha Rasimu ya Katiba katika Gazeti la Serikali na kwenye magazeti mengine pamoja na maelezo kwamba Rasimu ya Katiba itawasilishwa kwenye Bunge Maalum kwa ajili ya kupitishwa Katiba inayopendekezwa.”[v]
Mheshimiwa Spika,
Ili kutimiza matakwa haya ya Sheria na kwa kuzingatia mapendekezo ya Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume, Bunge lako tukufu linahitaji kuangalia upya suala la uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge Maalum. Kwa mujibu wa kifungu cha 22(2) cha Sheria, idadi ya wajumbe wa Zanzibar katika Bunge Maalum watakaotokana na makundi yaliyoainishwa katika kifungu cha 22(1)(c) “... haitapungua theluthi moja ya wajumbe hao.” Hii ina maana kwamba, kwa uchache kabisa, wajumbe hao wa Zanzibar hawatapungua 55.
Rasimu ya Katiba itakayojadiliwa na Bunge Maalum inahusu Katiba ya Jamhuri ya Muungano peke yake. Rasimu hiyo imependekeza kwamba masuala yote yasiyo ya Muungano ya Washirika wa Muungano, yaani Tanzania Bara na Zanzibar, yashughulikiwe na Katiba za Washirika hao.[vi]
Kwa sasa Wabunge wanaotoka Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano ni 83, wakati Baraza la Wawakilishi Zanzibar lina wajumbe 76. Kwa ujumla, kwa hiyo, ili kutekeleza matakwa ya kifungu cha 22(1) na (2) cha Sheria, Zanzibar itakuwa na wajumbe 219 katika Bunge Maalum lenye wajumbe 604, sawa na takriban 36% ya wajumbe wote. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua: kama ilikuwa busara na sahihi kwa nusu ya wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoka Zanzibar, kwa nini isiwe busara na sahihi vile vile kwa nusu ya wajumbe wa Bunge Maalum litakaloijadili na kuipitisha Katiba Mpya hiyo kutoka Zanzibar? Au ndio kusema kwamba hoja za usawa kati ya nchi Washirika wa Muungano huu ni kelele za majukwaani tu?

Mheshimiwa Spika,
Profesa Palamagamba J.A.M. Kabudi wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mjumbe wa Tume aliwahi kusema kwenye Semina ya Wabunge Juu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba iliyofanyika hapa Dodoma tarehe 12 Novemba 2011 kwamba: “Katika kuandika katiba mpya, wabia wa Muungano wanarudi kwa usawa.” Kwa sababu hiyo, na kwa kuzingatia mapendekezo ya ‘hadhi na haki sawa’ baina ya Washirika wa Muungano yaliyoko katika Rasimu ya Katiba,[vii] Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba idadi ya wawakilishi wa Zanzibar katika Bunge Maalum iongezwe hadi kufikia nusu ya wajumbe wote wa Bunge Maalum.
Hili linawezekana kwa namna mbili. Kwanza, kwa kuongeza idadi ya wajumbe waliotajwa katika kifungu cha 22(1)(c) hadi 354 kama tulivyopendekeza katika Maoni haya. Na pili, kwa kurekebisha kifungu cha 22(2) ili kisomeke kwamba idadi ya wajumbe kutoka Zanzibar ‘haitapungua asilimia hamsini na tano ya wajumbe hao.’ Kama pendekezo hili litakubaliwa na Bunge lako tukufu, wajumbe wa Bunge Maalum kutoka Zanzibar wataongezeka kutoka 214 kwa mujibu wa Sheria ilivyo sasa, hadi 323. Muhimu zaidi, Bunge Maalum litakuwa limetimiza matakwa ya usawa wa Washirika wa Muungano kwa kuwa na idadi sawa ya wajumbe katika Bunge hilo. Hili litaondoa manung’uniko yanayoweza kujitokeza baadae kwamba Wazanzibari hawakutendewa haki sawa katika Bunge la Katiba.
WATUMISHI WA BUNGE MAALUM
Mheshimiwa Spika,
Muswada unapendekeza marekebisho mengine katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Hivyo basi, aya ya 4 inapendekeza marekebisho ya kifungu cha 24(4) kama ifuatavyo: “Katibu wa Bunge Maalum baada ya kushauriana na Naibu wake na taasisi husika, atateua kutoka katika Bunge, Baraza la Wawakilishi na taasisi husika idadi ya watumishi kama itakavyoonekana inafaa kwa utekelezaji wa majukumu na mamlaka ya Bunge Maalum.” Kama kilivyo hivi sasa, kifungu hicho kinasomeka kama ifuatavyo: “Katibu wa Bunge Maalum baada ya kushauriana na Naibu Katibu wa Bunge Maalum watateua watumishi kutoka kwenye Bunge na Baraza la Wawakilishi kwa idadi watakayoona inafaa kwa ajili ya kutekeleza kwa ufanisi majukumu ya Bunge Maalum.”
Mheshimiwa Spika,
Kama inavyoonekana wazi, mabadiliko pekee yanayopendekezwa na Muswada ni maneno ‘taasisi husika.’ Maneno haya hayajatafsiriwa mahali popote katika Sheria, na Muswada uko kimya juu ya maana yake. Hata Maelezo ya Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria mbele ya Kamati yako kimya juu ya maneno hayo.[viii]
Ukimya huu una mwangwi mkubwa. Kama pendekezo hili litakubaliwa, kutakuwa na uwezekano wa watumishi wa Bunge Maalum la Katiba kuteuliwa kutoka katika taasisi na idara mbali mbali za serikali, au hata taasisi zisizokuwa za kiserikali. Kwa sababu Bunge Maalum litatekeleza majukumu yake kwa muda maalum unaopendekezwa katika aya ya 6 ya Muswada huu, ni wazi watumishi hao watatumikia Bunge Maalum on secondment kutoka kwenye taasisi zao za mwanzo. Kwa maana hiyo, watumishi hao watawajibika kwa taasisi zao na wanaweza kutumiwa na taasisi zao kutoa taarifa au siri muhimu juu ya shughuli za Bunge Maalum kwa taasisi zao.
Kwa upande mwingine, watumishi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wamepewa kinga ya kikatiba inayowakataza kupokea maelekezo kutoka taasisi nyingine nje ya Bunge. Kama kifungu cha 4(3) cha Sheria ya Uendeshaji Bunge, Na. 14 ya 2008, inavyoweka wazi, katika utekelezaji wa majukumu yao, watumishi wa Bunge “... hawatapokea maelekezo kutoka mahali popote nje ya Utumishi (wa Bunge).” Katika mazingira haya, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba mapendekezo ya kurekebisha kifungu cha 24(4) hayakidhi matakwa ya uhuru wa Bunge Maalum na, kwa sababu hiyo, yasikubaliwe na Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Spika,
Kuna hoja kubwa zaidi juu ya pendekezo hili. Hoja hii inahusu mamlaka ya Katibu wa Bunge Maalum na Naibu wake kuteua watumishi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Mapinduzi Zanzibar kuwa watumishi wa Bunge Maalum chini ya kifungu cha 24(4) cha Sheria, na pendekezo la Muswada la kukifanyia marekebisho.
Kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Bunge, Katibu wa Bunge hana mamlaka ya kuteua watumishi wa Bunge peke yake. Hayo, kwa mujibu wa Sheria hiyo, ni mamlaka ya pamoja kati ya Katibu na Tume ya Utumishi wa Bunge na utekelezaji wake unahitaji mashauriano kati ya vyombo hivyo viwili.[ix] Kwa sababu hiyo, na kwa kuzingatia utaratibu wa Sheria hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza watumishi wa Bunge Maalum wateuliwe kutoka miongoni mwa watumishi wa Bunge na Baraza la Wawakilishi baada ya mashauriano kati ya Katibu wa Bunge Maalum na Naibu wake pamoja na Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum. Pendekezo hili lina faida kwamba watumishi wa Bunge Maalum watakuwa wameteuliwa na watawajibika kwa Bunge Maalum na siyo kwa taasisi nyingine nje ya Bunge Maalum. Kwa maana hiyo, pendekezo la Muswada juu ya uteuzi wa watumishi wa Bunge Maalum nje ya Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi Zanzibar halina umuhimu na linapaswa kukataliwa.
TAFSIRI YA RASIMU YA KATIBA
Mheshimiwa Spika,
Muswada unapendekeza marekebisho ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inayohusu tafsiri ya maneno mbali mbali. Mapendekezo ya Muswada yanahusu tafsiri ya maneno ‘Rasimu ya Katiba’ na ‘Kanuni.’ Pendekezo la kutafsiri neno ‘Kanuni’ halina utatanishi wowote na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaliunga mkono. Kwa upande mwingine, Kambi Rasmi Upinzani Bungeni inapinga tafsiri inayopendekezwa ya maneno ‘Rasimu ya Katiba.’ Kwa mujibu wa aya ya 2 ya Muswada, maneno ‘Rasimu ya Katiba’ yatakuwa na maana ya “... Rasimu ya Katiba ambayo imetayarishwa na Tume kutokana na maoni na mapendekezo ya wananchi chini ya Sheria.”
Pendekezo hili linapingana na maudhui ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kwanza, pamoja na kwamba maoni ya wananchi ni chanzo muhimu cha ripoti ya Tume na Rasimu ya Katiba, maoni hayo sio chanzo pekee cha ripoti ya Tume na Rasimu ya Katiba. Kwa mujibu wa kifungu cha 17(4) cha Sheria, Tume inatakiwa kupitia “na kuchambua michango, mawazo, maoni, taarifa na mapendekezo yaliyokusanywa na kufanyiwa tathmini siku za nyuma....” Kifungu hicho kimeorodhesha nyaraka nyingi muhimu na za kihistoria ambazo zimejenga taswira ya kikatiba ya nchi yetu tangu uhuru wa Tanganyika mwaka 1961. Tume inawajibika kuzipitia na kuzichambua nyaraka zote hizo “katika kutekeleza majukumu yake chini ya Sheria hii....”
Pili, Tume pia inawajibika kutumia “tafiti za kiuchambuzi na kitaalam zitakazofanywa na Tume”,[x] na “nyaraka nyingine zozote ambazo Tume itaona ni muhimu.”[xi] Vyanzo vyote hivi vinatakiwa kutumika katika matayarisho ya Rasimu ya Katiba. Kwa maana hiyo, madhara ya mapendekezo ya Muswada juu ya tafsiri ya maneno ‘Rasimu ya Katiba’ ni ya wazi na mabaya. Kama yatakubaliwa na kuwa Sheria, vyanzo vyote hivi vya ripoti ya Tume na Rasimu ya Katiba vitakuwa redundant.
Aidha, mapendekezo ya Tume na Rasimu ya Katiba yanayotokana na vyanzo hivyo yatakuwa kinyume cha Sheria na yatabidi yaondolewe kwenye ripoti na Rasimu ya Katiba. Kwa sababu hizi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba maneno ‘Rasimu ya Katiba’ yatafsiriwe kumaanisha “... Rasimu ya Katiba ambayo imetayarishwa na Tume kwa mujibu wa Sheria hii.” Tafsiri hii inayopendekezwa inajumuisha maoni ya wananchi pamoja na vyanzo vingine vyote vya ripoti ya Tume na Rasimu ya Katiba vilivyoainishwa kwenye Sheria.
UHALALISHAJI WA KATIBA MPYA
Mheshimiwa Spika,
Muswada unapendekeza marekebisho katika kifungu cha 31 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinachohusu ‘uendeshaji wa kura ya maoni.’ Inapendekezwa kwamba kifungu hicho kifutwe na badala yake kiwekwe kifungu kipya kitakachosema kwamba “masharti yote yanayohusu uendeshaji wa kura ya maoni utawekwa na Sheria ya Kura ya Maoni.” Kwa vile tayari kuna Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni, 2013, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakubaliana na pendekezo hili.
Hata hivyo, kifungu cha 31 sio kifungu pekee katika Sheria hii chenye masharti ya uendeshaji wa kura ya maoni. Kuna vifungu vingine vinavyotaja au kuweka utaratibu wa kura ya maoni. Ukweli ni kwamba Sehemu ya Sita yote inayohusu ‘uhalalishaji wa Katiba Inayopendekezwa’ inahusika na masuala mbali mbali ya kura ya maoni. Vile vile, kifungu cha 4(1)(n) na (2) navyo pia vinataja kura ya maoni. Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, vifungu hivi pamoja na Sehemu ya Sita yote vinahitaji kurekebishwa kwa kufutwa.
Mheshimiwa Spika,
Muswada unapendekeza kufanya marekebisho katika kifungu cha 27(2) cha Sheria kinachohifadhi ‘uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge Maalum’ kwa kuweka kinga ya mashtaka dhidi ya wajumbe wa Bunge Maalum. Zaidi ya hayo, Muswada unapendekeza muda usiozidi siku sabini kwa Bunge Maalum kujadili Rasimu ya Katiba. Muda huo unaweza kuongezwa kwa siku nyingine zisizozidi ishirini kwa ridhaa ya Rais “baada ya kukubaliana na Rais wa Zanzibar....” Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakubaliana na mapendekezo yote haya ya Muswada kwa caveat kwamba pendekezo la muda wa nyongeza lisiwekewe muda mahsusi. Hii ni kwa lengo la kuwezesha muda kuongezwa kulingana na hali halisi ya majadiliano ndani ya Bunge Maalum.
JEDWALI LA MAREKEBISHO LA SERIKALI
Mheshimiwa Spika,
Serikali iliwasilisha Jedwali la Marekebisho ya Muswada huu mbele ya Kamati ikipendekeza marekebisho kadhaa katika Muswada na katika Sheria mama. Mapendekezo haya ni ya aina mbili. Kwanza, ni mapendekezo ya marekebisho ya Muswada uliosomwa mbele ya Bunge lako tukufu katika Bunge la Kumi na Moja, na ambayo yalijadiliwa na Kamati na wadau mbali mbali. Haya ni marekebisho yanayopendekezwa katika sehemu A, B na D ya Jedwali la Marekebisho ya Serikali. Marekebisho haya yanaenda sambamba na matakwa ya kanuni ya 84(3) na (4) ya Kanuni za Kudumu na kwa hiyo yanakubalika kikanuni.
Kwa upande mwingine, marekebisho yanayopendekezwa katika sehemu C na E za Jedwali la Marekebisho ya Serikali ni mambo mapya ambayo hayakuwepo kwenye Muswada uliosomwa kwa Mara ya Kwanza katika Bunge lililopita. Marekebisho haya hayakujadiliwa na wadau wan je ya Bunge, na hayajulikani kwa Wabunge wasiokuwa wajumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala. Kwa sababu hiyo, marekebisho haya yanakiuka masharti ya kanuni ya 86(7) ya Kanuni za Kudumu inayoelekeza kwamba “mjadala wakati wa Muswada wa Sheria Kusomwa Mara ya Pili utahusu ubora na misingi ya Muswada huo tu.” Ili kulinda heshima ya Bunge lako tukufu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakuomba, Mheshimiwa Spika, utekeleze wajibu wako chini ya kanuni ya 5(2) ya Kanuni za Kudumu kwa kufutilia mbali sehemu C na E za Jedwali la Marekebisho ya Serikali kwa sababu zinakiuka matakwa ya kanuni tajwa ya Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Spika,
Sehemu C ya Jedwali la Marekebisho ya Serikali tunaokuomba uifutilie mbali inapendekeza kuongezwa kwa kifungu kipya cha 22A katika Sheria. Katika pendekezo la awali kuhusu kifungu hicho, ilikuwa inapendekezwa kumfanya Spika wa Bunge hili tukufu kuwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum kwa ajili ya kutengeneza Kanuni za Kudumu za Bunge Maalum, na kwa ajili ya uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum. Baada ya Kamati kuhoji na kuelezwa kwamba Spika/Mwenyekiti wa Muda atakuwa pia na haki ya kugombea kuwa Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum na hivyo kutengeneza mgongano wa wazi wa maslahi, Kamati ilielekeza kwamba Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalum watasimamia uchaguzi wa Mwenyekiti wa Muda ambaye hatakuwa na haki ya kugombea nafasi ya Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum. Hata hivyo, hoja ya msingi kwamba hili ni pendekezo jipya ambalo halikuwepo kwenye Muswada uliosomwa Mara ya Kwanza inabaki pale pale.
Kuhusu sehemu E ya Jedwali la Marekebisho ya Serikali, sehemu hiyo inapendekeza kufifisha matakwa ya kifungu cha 26(2) cha Sheria inayoweka masharti ya kupitisha Katiba inayopendekezwa kwa theluthi mbili ya wajumbe wote wa Bunge Maalum wanaotoka Tanzania Bara na idadi hiyo hiyo ya wajumbe wanaotoka Zanzibar. Pendekezo jipya ni kupunguza idadi ya uungwaji mkono hadi wingi wa kawaida (simple majority) ya wajumbe wote wanaotoka Tanzania Bara na idadi hiyo hiyo ya wajumbe wanaotoka Zanzibar endapo Bunge Maalum litashindwa kupitisha Katiba inayopendekezwa kwa theluthi mbili baada ya kupiga kura mara mbili. Pendekezo hili nalo linakiuka matakwa ya kanuni ya 86(7) na linapaswa kuondolewa katika mjadala wa Muswada huu.
MENGINEYO
KUITISHWA TENA BUNGE MAALUM?
Mheshimiwa Spika,
Kuna maeneo mengine ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo, kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, yanahitaji kufanyiwa marekebisho ili kuwezesha utekelezaji bora wa Sheria hii. Eneo mojawapo ni masharti ya kifungu cha 28(2) yanayoruhusu Bunge Maalum kuitishwa tena baada ya kukamilisha majukumu yake kwa mujibu wa Sheria na kuvunjwa chini ya kifungu cha 28(1) cha Sheria hii.
Kifungu cha 28(1) kinasema: “Baada ya kutunga Katiba Inayopendekezwa, masharti yatokanayo na mashrti ya mpito, Bunge Maalum litavunjwa na mamlaka ya kutunga masharti ya Katiba inayopendekezwa, masharti yatokanayo na masharti ya mpito yatakoma.” Kwa upande mwingine, kifungu cha 28(2) kinatengua masharti ya kifungu cha 28(1) kwa maneno yafuatayo: "Kuvunjwa na kukoma kwa mamlaka ya Bunge Maalum hakutachukuliwa kuwa kunaondoa mamlaka ya Rais kuliitisha tena Bunge hilo kwa lengo la kuboresha masharti yaliyomo kwenye Katiba inayopendekezwa.”
Mheshimiwa Spika,
Misingi mikuu ya tafsiri za kisheria inaelekeza kwamba chombo chenye mamlaka au majukumu ya kisheria ya kufanya jambo fulani kikishakamilisha kutekeleza mamlaka au majukumu yake hayo kinakuwa functus officio katika jambo hilo, yaani kinakuwa hakina mamlaka tena kisheria juu ya jambo hilo.[xii] Huu ndio msingi wa kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Athari ya kifungu cha 28(2) ni kulifufua kutoka katika wafu Bunge Maalum ambalo, kwa mujibu wa kifungu cha 28(1), linakuwa limekuwa functus officio baada ya kupitisha Katiba Mpya na masharti ya mpito. Na hii inafanywa na Rais ambaye – na chama cha siasa anachokiongoza – ni mdau mkubwa wa mchakato wa Katiba Mpya.
Katika Maoni yetu wakati wa mjadala wa kupitishwa kwa Sheria hii mwezi Novemba 2011, tulisema yafuatayo juu ya kifungu hiki: “Maana halisi ya maneno haya ni kwamba Rais atakuwa na mamlaka ya kuita tena Bunge la Katiba ili lifanye marekebisho ya mambo ambayo yeye au serikali yake au chama chake hawayapendi katika Katiba Mpya kabla haijapigiwa kura ya maoni na wananchi! Kama chombo huru cha wananchi, Rais hawezi kujipa madaraka ya kupingana na kauli ya wananchi kupitia Bunge la Katiba.”
Katika mapendekezo yake kwa timu ya Wataalam wa Serikali iliyoundwa kufuatia mkutano wa tarehe 26 Novemba, 2011 kati ya CHADEMA na Rais Jakaya Kikwete, CHADEMA ilipendekeza kwamba kifungu cha 28(2) kifutwe kabisa.[xiii] Huu ni wakati muafaka kukiangalia upya kifungu hiki ambacho kinaweza kuleta mgogoro usiokuwa na sababu endapo Rais ataamua kuliitisha tena Bunge Maalum kwa sababu Serikali au chama chake hakikubaliani na Katiba Mpya iliyopitishwa na Bunge Maalum.
MCHAKATO WA KATIBA YA TANGANYIKA NA ZANZIBAR
Mheshimiwa Spika,
Tarehe 3 Juni, 2013 Tume ilichapisha Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 2013. Kwa kufanya hivyo, na kwa mujibu wa kifungu cha 18(5) cha Sheria, Tume imekamilisha jukumu lake la kwanza baada ya kukamilisha zoezi la kukusanya maoni ya Watanzania juu ya Katiba Mpya. Rasimu hii inapendekeza mambo mengi na muhimu kwa mustakbala mzima wa nchi yetu na tayari imezua mjadala mkali wa kitaifa. Mwanazuoni mmoja maarufu nchini ameyaita mapendekezo ya Rasimu ‘Mapinduzi ya Kimya Kimya’[xiv]; wakati mwingine amehoji kama Rasimu hii ni ‘Mwarobaini au Sanduku la Pandora?’[xv] Aidha, Profesa Issa G. Shivji ambaye pengine ni msomi maarufu wa masuala ya kikatiba katika sehemu hii ya Afrika, ameonyesha kile ambacho amekiita ‘Utatanishi na Ukimya Katika Rasimu ya Katiba Mpya. [xvi]
Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kama ilivyo kwa wadau wengine ambao wamezungumzia Rasimu hiyo ya Katiba, eneo muhimu pengine kuliko yote ni muundo wa Jamhuri ya Muungano kama shirikisho lenye serikali tatu. Kwa sababu hiyo, Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume imejikita katika masuala ya Muungano tu. Na kwa mujibu wa Mwenyekiti wake, Tume haikushughulikia masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanganyika na Zanzibar kwa sababu mambo hayo yanatakiwa kushughulikiwa na Katiba za Washirika wa Muungano.
Kwa maana hiyo, masuala haya sasa itabidi yashughulikiwe kwa utaratibu mwingine wa kisheria Zanzibar na Tanganyika vile vile, ambao utakuwa tofauti na utaratibu uliowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kutokana na mapendekezo ya Rasimu ya Katiba, mchakato wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano hautakamilika bila ya kuwepo, na kukamilika, kwa mchakato wa Katiba Mpya kwa masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanganyika na ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
Kuanza na kukamilika kwa mchakato wa Katiba Mpya kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano ya Tanganyika na Zanzibar ni suala muhimu kwa muundo wowote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano au hata bila Muungano kuwepo, kwa sababu zifuatazo. Kwanza, hata kama muundo wa Muungano utakuwa wa serikali moja, au mbili za sasa, au tatu zinazopendekezwa na Rasimu, ni lazima masuala yote yanayoihusu Tanganyika yaingizwe kwenye mchakato wa Katiba Mpya. Hii ni kwa sababu Rasimu inahusu masuala saba ya Muungano tu, na Zanzibar ina Katiba yake tayari. Pili, hata kama wananchi wa Tanzania watakataa kuendelea na Muungano wa aina yoyote na kudai uhuru kamili wa Washirika wa Muungano, bado masuala ya Katiba Mpya ya Tanganyika na Zanzibar yatahitajika kufanyiwa kazi. Tatu, bila masuala ya Tanganyika kuamuliwa katika Katiba Mpya, mchakato mzima hautakamilika, na kwa maana hiyo, hakuwezi kukawa na uchaguzi wowote wa Jamhuri ya Muungano kwa upande wa Tanganyika.
Kwa vyovyote vile, constitutional gridlock hii lazima ipatiwe suluhisho. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba mchakato wa Katiba Mpya ya Tanganyika na marekebisho ya Katiba ya Zanzibar, 1984 uanze mara moja ili uendane sambamba na mchakato wa Katiba Mpya ya Jambhuri ya Muungano. Kwa vyovyote vile, kwa maoni yetu, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kama ilivyo sasa haiwezi kutumika kwa ajili ya mchakato huo kwa sababu sheria hiyo ilitungwa kwa ajili ya mchakato wa Katiba ya Muungano tu.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa kwa ajili ya mchakato wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Na Tume yenyewe imekiri kwamba haikujishughulisha na masuala yasiyokuwa ya Muungano kwa sababu hayakuwa sehemu ya majukumu iliyokabidhiwa kisheria. Kwa muundo wake, Tume hiyo haiwezi kujibadilisha na kuwa Tume ya Katiba ya Tanganyika. Kwa maana hiyo, mchakato wa Katiba ya Tanganyika unatakiwa kuwekewa utaratibu mpya na tofauti kabisa wa kisheria na wa kitaasisi. Hii itahitaji kutungwa kwa sheria mpya kwa ajili ya mchakato huo.
Sambamba na mchakato wa Katiba ya Tanganyika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kuanzishwa kwa mjadala juu ya masuala ya mpito kwa sababu kuna uwezekano mkubwa kwamba Katiba Mpya, ya Muungano peke yake au ya Muungano na za Washirika wake, yaani Tanganyika na Zanzibar, zisiwe tayari kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015. Au hata kama zitakuwa tayari kabla ya Uchaguzi Mkuu, kuna uwezekano mabadiliko makubwa ya kisheria na ya kitaasisi yatakayohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa Katiba Mpya, yasiwe tayari kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao. Kwa kuangalia mfano wa Kenya, Katiba Mpya ya nchi hiyo ilikamilika mwezi Agosti, 2010. Hata hivyo, mabadiliko mbali mbali ya kisheria na kitaasisi kwa ajili ya utekelezaji wa Katiba hiyo yalichukua zaidi ya miaka miwili na nusu hadi Uchaguzi Mkuu wa mwezi Machi, 2013.
Ikumbukwe kuwa Kenya haikuwa na suala la Muungano kama Tanzania. Sisi tuna Muungano wa muundo ambao upande mmoja wa Muungano huo una dola yenye Katiba na taasisi kamili za dola, wakati upande mwingine hauna dola wala Katiba na taasisi kamili za dola. Hii ina maana kwamba maandalizi yetu ya kisheria na kitaasisi yanaweza kuhitaji muda mrefu zaidi kuliko ilivyokuwa kwa Kenya. Hatuna budi kuanza kuyafikiria na kuyajadili mambo haya muhimu sasa.

TUNDU A.M. LISSU
WAZIRI KIVULI & MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA KATIBA NA SHERIA






No comments:

Post a Comment