MBUNGE wa Viti Maalum, Mariam Msabaha (CHADEMA) ameitaka serikali kutoa mikopo ya magari kwa mawakili wa serikali ili waweze kufanya kazi zao kwa wepesi zaidi.
Msabaha alitoa kauli hiyo jana bungeni mjini hapa wakati akiuliza swali la nyongeza akitaka kujua ni mawakili wangapi wa serikali wana nyumba nzuri za kuishi.
Pia alitaka kujua ni lini serikali itaboresha mazingira ya kazi kwa mawakili hao ikiwa ni pamoja na kuwapatia vitendea kazi.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki, alisema serikali kupitia Bunge, imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha kuwa watumishi wake wakiwemo mawakili wanafanya kazi katika mazingira bora na yenye usalama.
“Katika kutimiza azma hii, serikali imekuwa ikijitahidi kila inapowezekana kuboresha mazingira ya kazi kwa mawakili wa serikali kwa kuwapatia vitendea kazi,” alisema.
Kwa upande wake Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), alitaka kujua ni kwa nini vitabu vya rejea ambavyo ni vya masuala ya kisheria haviuzwi kwa mawakili wakiwemo wa kujitegemea.
Akijibu swali hilo, Kairuki alisema kuwa vitabu hivyo vimekuwa vikichapishwa isipokuwa upatikanaji wake ndio umekuwa mgumu.
Hata hivyo alisema serikali inafanya mchakato wa kuhakikisha vitabu hivyo vinapatikana kwa urahisi na kuuzwa kwa wanasheria wote nchini.
No comments:
Post a Comment