Thursday, August 22, 2013

Warioba asisitiza mambo ya msingi yajadiliwe Katiba mpya

Watanzania wametakiwa kujadili mambo ya msingi yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba kama afya, elimu, kilimo na uchumi  kwa ujumla ili kuepuka kupata Katiba yenye mafungu tofauti.Rai hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, wakati akifungua mkutano wa Kitaifa wa Baraza la Katiba la Tasnia ya Habari ulioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
“Tuwasikilize wananchi, tusipofanya hivyo tutakuwa tumepata Katiba ya mafungu …amueni mawazo yenu yaende katika Rasimu na siyo kukimbilia kujadili mihimili," alisisitiza.
Aliongeza: “Kuna mambo ya msingi ya kujadili ili Katiba ikamilike kama vile afya, elimu, uchumi pamoja na maadili badala ya kupoteza muda kujadili masuala yaliyo nje ya rasimu mtakuwa na viongozi ambao hawatekelezi maadili ya jamii yetu.”
Alifafanua kuwa watu wanazungumzia mambo ya madaraka na muundo wa Katiba bali maoni yao yajielekeze kwenye Rasimu ya Katiba.
Warioba alisema Tume yake haiwezi kuchukua maoni kwenye mikutano ya hadhara kwa sababu kipindi cha maoni kilishapita kinachojadiliwa ni kuboresha rasimu.
Mkutano huo wa siku moja ulihudhuriwa na wadau wa habari kutoka mikoa mbalimbali nchini.

No comments:

Post a Comment