Wanachama wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) kutoka Tanzania Bara na Visiwani watakutana kesho kujadili masuala muhimu ya jinsia yanayopaswa kuingizwa katika Katiba mpya.Washiriki hao watakutana kwa siku mbili Agosti 27 na 28, mwaka huu katika Makao Makuu ya Tamwa eneo la Sinza Mori jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Valerie Msoka, jana alisema miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa ni pamoja na ushiriki wa wanawake katika hatua za upatikanaji wa Katiba mpya yenye mrengo ya usawa wa jinsia nchini.
Alisema wajumbe pia watajadili kuhusu umuhimu wa kuwepo kwa sauti za wanawake katika Katiba mpya ili kuwa na sheria zinazokidhi masuala ya jamii na kutetea usawa kwa maendeleo ya taifa.
“Pia wajumbe watajadili masuala muhimu ya kijinsia yaliyojitokeza katika rasimu ya Katiba mpya na mambo ya wanawake na watoto kuimarishwa na kuingizwa katika Katiba hiyo” alisema.
Kwa mujibu wa Msoka, Tamwa ina amini kuwa kupatikana kwa Katiba mpya kutatokana na ushiriki wa wanaume na wanawake ili kuwa na makubaliano ya misingi mikuu itakayoongoza taifa.
No comments:
Post a Comment