Wednesday, August 28, 2013

Mnyika ahofia Katiba mpya kuvurugwa

MBUNGE wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika, (Chadema) ameitaka jamii kupaza sauti juu ya mwenendo wa mchakato wa Katiba Mpya ili kuepusha mianya inayoelekea kuvuruga mchakato huo. Mnyika alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati akifungua mkutano wa vijana waliochujwa katika Mabaraza ya Katiba ya Kata Wilaya ya Ilala.
Alisema kuna kila dalili zinazoashiria mchakato huo kuvurugwa na mkono wa serikali iliyopo madarakani kwa sababu ya kuwapo kwa shinikizo la kupitisha sheria ambazo zinampa mamlaka zaidi Rais kuingiza mkono wake katika mchakato unaoendelea sasa.

“Jamii inabidi ipaze sauti kwa hili kwani ni dhahiri kwamba mchakato huu unaelekea kuvurugwa, kwa mfano kuna miswada miwili inayopelekwa katika bunge hili linaloendelea, ambayo ina msukumo ya kupitishwa haraka ili  iwe sheria kamili ambazo rais ataitumia kuingiza nguvu yake ndani ya mchakato huu,”alisema Mnyika.

Alitaja miswada hiyo kuwa ni wa Sheria na Marekebisho ya sheria ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na ule wa Sheria ya Kura ya Maoni.

Alisema kama miswada hiyo haitajadiwa kwa kina na Bunge na kupitisha kuwa sheria basi rais atapata nguvu ya kuteua watu wake ambao watavuruga zaidi malengo ya mchakato mzima wa kuzalisha Katiba iliyobeba mawazo ya Watanzania.

Akitolea mfano Bunge la Katiba, Mnyika alisema kama miswada hiyo, itapitishwa na kuwa sheria basi rais atakuwa na mamlaka ya kuteua wajumbe 166 kwa ajili ya kuunda Bunge la Katiba, hivyo ni vigumu kwao kugeuka matakwa anayoyahitaji rais.

Aidha alisema kwa upande wa mswada wa Sheria ya Kura za Maoni, kunahitajika tume huru ya kura ya maoni ambayo itajengwa na watu kutoka makundi mbalimbali ya kijamii.

No comments:

Post a Comment