Thursday, August 29, 2013

Chadema: Tutapeleka mapendekezo yetu Katiba mpya kwa lori

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimefunga rasmi mikutano yake ya kukusanya maoni kutoka kwa wananchi kuhusu Rasimu ya Katiba mpya kupitia mabaraza huru ya chama hicho, jijini Dar es Salaam.

Chama hicho kimesema kimefanikiwa kukusanya maoni ya wananchi milioni tano na kwamba wanatarajia kupeleka maoni hayo kwenye ofisi za Tume kwa lori kwa kuwa ni mengi. 

Akifunga mikutano hiyo juzi jijini humo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willbrod Slaa, alisema katika mikutano 49 waliyoifanya ndani ya mikoa tisa nchini, wamekusanya takribani maoni milioni tano kutoka kwa Watanzania kuhusu maboresho ya rasimu hiyo dhidi ya milioni mbili yaliyokusanywa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoka kwa wanachama wake.

Dk. Slaa alitoa kauli hiyo juzi katika viwanja vya Mwembeyanga wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam, wakati akihitimisha mkutano wake wa mabaraza huru ya kukusanya maoni kwa Watanzania juu ya Rasimu ya Katiba mpya. Alisema, Chadema wanaunga mkono  Rasimu ya Tume ya  Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, lakini wanapingana naye katika baadhi ya vipengele kama vile Tanzania Bara kuitwa Tanganyika.

Baadhi ya wananchi waliokuwapo kwenye mkutano huo walipendekeza kuongezwa kwa vipengele vya haki kwenye tunu za taifa.

Tunu saba za taifa ambazo zimependekezwa katika rasimu hiyo ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya taifa.

Wananchi hao walipendekeza kwamba kwenye rasimu hiyo kiongezwe kipengele kinachomruhusu kila Mtanzania kuwa na haki ya kumiliki ardhi, kupata huduma bora za afya kama viongozi wa serikali na wabunge wanavyofanyiwa.

Dk. Slaa alisema katika mikutano hiyo  wamezunguka katika mikoa tisa na kufanya mikutano 49 huku zaidi ya Watanzania milioni tano wakiwa wametoa maoni yao juu ya rasimu hiyo.

1 comment:

  1. SAsa juzi ulikuwa wapinga nini juu ya Kinana kusema mambo ya chama chake,Acha ubinafsi,wewe na chama chako mkisema/mkitoa maoni yenu ni sawa lakini wengine hawapaswi kufanya hivyo,hebu jaribu kuwa na moyo subira na uvumilivu ili nchi isonge mbele badala ya kuendeleza mvutano usio na sababu.

    ReplyDelete