Wanasheria na wanaharakati Zanzibar wamepinga muundo wa Bunge la Katiba la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutaka uangaliwe upya kabla ya kufanyika kwa kura ya maoni mwakani.
Msimamo huo waliuweka wakati wakijadili Sheria Namba 8 ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2012 katika kongamano lililokuwa likijadili sheria hiyo kuanzia kifungu cha 22 (1) cha kuitisha Bunge Maalum, mjini Unguja jana chini ya Mwenyekiti Profesa Chris Peter Maina.
Akitoa maoni yake, Mzee Makame Usi kutoka vyama vya wafanyakazi alisema wabunge na wawakilishi lazima wapunguzwe katika Bunge la Katiba na nafasi za uwakilishi kwa uwiano ziangaliwe zaidi toka makundi mengine ya kijamii ili kuepusha utashi wa kisiasa kutawala zaidi.
Alisema kundi la vijana na wanawake lishirikishwe ipasavyo badala ya nafasi nyingi kuchukuliwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Wabunge na asasi za kiraia.
Kwa upande wake, Abdulowaluif Fatawi alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatakiwa ikiangalie upya kifungu cha 22 (1) ili Bunge la Katiba liwape nafasi walimu na wanasheria hasa kwa kuzingatia suala la kikatiba ni la kitaaluma na si kujaza wanasiasa wanaoongozwa na itikadi za vyama vyao.
“Walimu na wanasheria wapewe nafasi katika uundwaji wa Bunge la Katiba badala ya kujaza wawakilishi wa NGOs, wabunge na wawakilishi hii si sawa, hofu yangu tutaharibikiwa tuendako,” alisema Fatawi.
Mwanasheria Horold Sungusia wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, alisema Watanzania wanaweza kujikuta wakicheza pata potea ikiwa hawataongozwa na umakini pamoja na kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya vyama vya siasa.
Alisema katiba ya zamani imeshuhudiwa kuwa ndiyo chimbuko la uvunjaji wa haki za binadamu, kulegalega kwa misingi ya utawala bora wa sheria, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.
Kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Bunge la Katiba litakuwa na wabunge 604 na wawakilishi 81 ambapo uwakilishi mkubwa utatoka katika vyama vya siasa huku CCM wakiwa na wabunge 398 sawa na asilimia 66 na upinzani wabunge 206 sawa na asilimia 34.
Mwenyekiti wa kongamano hilo, Profesa Maina alisema muundo wa Bunge la Katiba unahitaji kuangaliwa upya na mapema ili kuwapata wajumbe watakaopata fursa ya kushiriki kwa kuzingatia maslahi ya kitaifa wakati wakijadili badala ya mitazamo ya vyama vyao vya siasa.
Hata hivyo, Mkuu wa Utawala wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mrakib Mbarokuk Mrakib, alisema suala la CCM kuwa na uwakilishi mkubwa halikwepeki na kwamba upana wa uwakilishi wake ni kielelezo cha kukubalika kwake mbele ya wananchi.
Alisema si kigezo kizuri cha kulitenga kundi la wanasiasa kwa madai ya uwakilishi wao kwenye chombo hicho wakati wao ndiyo waliotokana na uwakilishi kamili wa wananchi waliowachagua katika majimbo yao tofauti na wanaotaka kuingizwa kupitia milango mingine isiyo rasmi.
“Uwakilishi wa CCM na wingi wao haukwepeki, ukiwakwepa ni kuwabagua na hiyo haitakuwa haki inayostahili, wasitazamwe wanasiasa na vyama ila waangaliwe kutokana na dhamana ya uwakilishi walionao kutokana na wananchi,” alisema Mrakib.
No comments:
Post a Comment