WAMTAKA ASIONEKANE HADI 2015
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willibrod Slaa ametakiwa kutokanyaga mkoani Mbeya kuanzia sasa hadi ifikapo mwaka 2015 wakati wa uchaguzi mkuu.
Kauli hiyo imetolewa juzi mjini hapa na kundi kubwa la wanachama na wapenzi wa CHADEMA mara baada ya kumalizika kwa mkutano mkubwa ambao umevunja rekodi ya mikutano iliyowahi kufanyika kwenye viwanja vya Luanda-Nzovwe, maarufu Uwanja wa Dk. Slaa.
Wamedai kwamba hakuna haja kwa Slaa kwenda mkoani humo kwa ajili ya mikutano ya kuhamasisha, badala yake wamemtaka atulie na kuanza maandalizi kabambe ya timu ya uchaguzi mkuu ujao.
Bila kutaja majina yao, wengi wa wanachama hao wamesema kumruhusu Dk. Slaa kuzunguka mikoani katika operesheni ya M4C ni kumchosha bure kwa kile walichodai anahitaji kukusanya nguvu katika mapambano makubwa ya safari ya kuelekea kushika hatamu za nchi 2015.
“Tunamtaka Dk. Slaa mwaka 2015. CCM wanasema eti kazeeka, sisi vijana tunamtaka Dk. Slaa na uzee wake.
“Nchi hii lazima iendeshwe na wazee wenye akili, hekima na busara, wazee wenye kujua uchungu wa watu wanyonge kama mzee wetu awaonyeshe CCM jinsi nchi ya wapigania haki inavyopaswa kuongozwa,” walisema vijana hao waliojitambulisha kwa majina ya Saleh Issa, John Paul na mmoja aliyejitaja kwa jina la Mussa.
Katika mkutano huo ambao ulihutubiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, ulishuhudia baadhi ya wanachama wa CCM wakichangia harambee ya papo kwa papo ambapo kiasi cha sh milioni 3.2 zilipatikana.
Baadhi ya askari polisi walioshiriki kulinda mkutano huo, wamekiri kuwa ulitawaliwa na utulivu wa hali ya juu tofauti na ilivyokuwa ikihisiwa na walinzi hao wa amani.
Mkutano huo wa juzi ulimalizika kwa chama hicho kusimika uongozi imara wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini chini ya mratibu wake, Frank James Mwaisumbe, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa, aliyekuwa kada wa CCM ambaye amejiunga na CHADEMA, Mwaisumbe aliangushwa katika kura za maoni mwaka 2010 alipogombea ubunge jimbo la Mbeya mjini kwa tiketi ya CCM.
Licha ya kuwepo kwa mafanikio makubwa katika mkutano huo, baadhi ya wapenzi na wanachama wa chama hicho walielezea kukerwa na nguvu za ziada zinazoonyeshwa na vijana wa ulinzi wa chama hicho, Red Brigedi, na kushauri wapewe mafunzo ya amani na uvumilivu ili kukisimamia vyema chama hicho.
Yakishika bayana CCM, Maswa
Naye Mwandishi Samwel Mwang kutoka Maswa anaripoti kuwa mkutano wa CHADEMA mjini hapo jana ulikivuruga vibaya Chama cha Mapinduzi baada ya kuzoa mamia ya wanachama wake waliojiunga na upinzani.
Katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya wazi vilivyoko Madeco mjini Maswa wabunge wa CHADEMA wakingozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Taifa Shilugushela Nyangaki walidai kuwa hakuna haja tena ya Watanzania kuiamini CCM ambayo kwa miaka 51 bado watu ni maskini wa kutupwa kutokana na sera zake mbovu.
Wabunge hao Rahel Mashishanga, Viti Maalumu, jimbo la Shinyanga, Silvester Kasulumbayi wa Maswa Mashariki, Meshack Opolukwa wa Meatu na John Shibuda wa Maswa Magharibi walisema serikali ya CCM imewatelekeza wananchi wake katika sekta za elimu, afya, maji miundo mbinu na hata chakula.
Wabunge Mashishanga na Opolukwa walisema kushindwa vibaya kwa wanafunzi wa kidato cha nne ni matokeo ya mitaala mibovu ya elimu ya msingi hadi sekondari na mgomo baridi wa walimu.
Kuhusu sekta ya afya wabunge hao walisema kuwa wananchi wamekuwa wakihaha kupata madawa na kuwepo kwa migomo baridi kwa madakari na wauguzi hasa maeneo ya vijijini.
Naye Shibuda alisema kuwa serikali ya CCM imekuwa ikikopa pesa nyingi na badala ya kuwasaidia wakulima imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha kwa anasa na safari lukuki za viongozi nje ya nchi wakiambatana na misafara mikubwa.
Aliongeza kuwa serikali imejaa rushwa hali ambayo inasababisha kuwepo kero nyingi kwa wananchi na kukosa huduma muhimu hasa vijijini.
No comments:
Post a Comment