Sunday, March 10, 2013

BAWACHA yampa tuzo Nkya


BARAZA la Wanawake wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA) limempa tuzo ya heshima ya kuthamini mchango wake katika jamii aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Ananilea Nkya.
BAWACHA ilitoa tuzo hiyo katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika juzi katika Ukumbi wa Don Bosco, Upanga jijini Dar es Salaam.
Tuzo hiyo ilikabidhiwa kwa mgeni rasmi, Gema Akilimali kwa niaba ya Nkya ambaye yupo masomoni Uingereza.
Makamu Mwenyekiti wa BAWACHA, Suzan Lyimo alisema walimzawadia tuzo hiyo kutokana na kazi zake kwa jamii; haki za wanawake na watoto katika matendo ya ubakwaji, ukeketaji na unyanyasaji.
Lyimo alisema utaratibu wa BAWACHA kutoa tuzo kwa mwanamke jasiri utaendelea kila mwaka ili kuionesha jamii kwamba mwanamke ni mtu muhimu katika jamii na kwamba anao uwezo wa mkubwa kufanya kila jambo zuri la maendeleo.
Naye Akilimali aliwataka BAWACHA kufanya kazi kwa vitendo ili maendeleo yaonekane kulingana na kaulimbiu ya dunia inayosema “ahadi ni ahadi umefika wakati wa utekelezaji kivitendo, ukomeshaji wa ukatili dhidi ya mwanamke na mtoto.”
Mwanaharakati huyo mkongwe aliwataka wanawake kugombea katika nafasi za uongozi na uamuzi ili kuuondoa mfumo dume na kuleta usawa wa kijinsia katika nyanja zote za kisiasa, kijamii, kiutamaduni na kiuchumi.

No comments:

Post a Comment