Tuesday, January 1, 2013

CHADEMA yatangaza kiama cha CCM

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) itaondolewa madarakani na watumishi wa umma. Chama hicho kikuu cha upinzani kimesema kuwa, CCM itaondolewa madarakani iwapo haitapandisha mshahara wa kundi hilo kabla ya mwaka 2015.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi Chadema, John Mnyika, alisema nguzo pekee iliyobaki kwa CCM ni watumishi wa umma, ambao wanauwezo mkubwa wa kuiangusha.

Mnyika alisema ndani ya miaka miwili Chadema imefanikiwa kueneza sera na malengo yao na kufanikiwa kuungwa mkono kwa asilimia 90 ya Watanzania wasio watumishi wa umma.

Alisema kazi iliyobaki hivi sasa ni kukata nguzo hiyo iliyosalia ambayo ni watumishi wa umma na kuwataka walimu, madaktari na watumishi wengine wa idara zote za Serikali kuondoa hofu ya kupoteza ajira zao na kuungana na Chadema ili kuiondoa madarakani.

“Hatuingii Ikulu mwaka 2015 kwa fadhila wala hila za CCM, bali tunaingia kwa nguvu ya umma na ishara za nguvu ya umma zimejidhihirisha jinsi wananchi walivyounga mkono Vuguvugu la Mabadiliko (M4C).

“CCM itarajie nguvu kubwa mwaka unaoanza kesho (leo), baada ya ratiba ya kikao cha Kamati Kuu kukaa na kuweka mpango kazi, CCM isidhani inaweza kuisambaratisha Chadema kirahisi kama inavyofikiri.

“Kwanza wao wenyewe wameanza kutofautiana kauli, juzi Naibu Katibu Mkuu Bara, Mwigulu Nchemba amesema ifikapo 2016 Chadema itakuwa imekufa.

“Wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira aliwahi kusema Chadema itakufa baada ya mwaka mmoja sasa hapo nani mkweli?

“Ni vema CCM ikaachana na propaganda za uchaguzi wa mwaka 2015 na badala yake iwatumikie wananchi kwa kupanua vyanzo vya mapato na kutumia rasilimali za nchi ili watumishi wa umma waweze kuongezewa mshahara wao vinginevyo watajutia.

“Hadi sasa asilimia 90 ya wananchi wasio na kazi wanaunga mkono M4C na mara zote wamekuwa wakiwalaumu watumishi wa umma kwa kuiunga mkono CCM kwa kuhofia kibarua chao. Sasa tunawaomba kuungana nasi ili kuiondoa CCM madarakani,” alisema.

Mnyika alisema ameshangazwa na kitendo cha Nchemba kushindwa kutangaza majina ya wabunge sita wa Chadema walioomba kujiunga na CCM, kama alivyoahidi badala yake ameendeleza propaganda.

Alisema CCM inapaswa kuwaeleza Watanzania juu ya mpango wao wa kujivua gamba umefikia wapi na kwa nini imeshindwa kutatua migogoro inayowakabili wananchi huku miaka 50 ya uhuru ikiwa imepita.

Yamuonya Spika Makinda 

Akizungumzia namna chama chake kilivyojipanga kwenda bungeni mwaka huu, Mnyika alisema wabunge wa Chadema wamejipanga kwenda na mfumo mpya wa kuwasilisha maoni, hotuba, maswali na uchangiaji bungeni.

Mnyika alitoa wito kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda kuongoza Bunge mwaka 2013 kwa kufanya marekebisho ya kanuni na kumtaka atambue kwamba anaongoza chombo cha juu.

“Huu ni wito kwa Spika Makinda anapaswa kubadilika mwaka huu, lazima atoe nafasi kwa wabunge wote kuishauri na kuisimamia Serikali, ili aweze kutenda haki lazima asimamie upande wa wananchi.

“Atambue maendeleo ya haraka ya nchi hayapatikani kwa mbunge mmoja mmoja kutoa fedha zake kwa wananchi wake bali wabunge wote kushirikiana na Serikali kuendeleza mipango ya maendeleo,” alisema.

Tathmini ya mwaka 2012

Akitoa tathmini Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Katibu Mkuu, Victor Kimesera alisema mwaka 2012 ulioisha jana ulikuwa mwaka wa ubakaji wa demokrasia ulioambatana na matukio ya mauaji ya wananchi.

Kimesera alisema vitendo vilivyotokea mwaka 2012 kama mauaji ya raia wasio na hatia, bidhaa kupanda bei, umeme, nauli na vitu vingine ni matokeo ya Serikali kushindwa kutenda haki kwa Watanzania.

Aliwataka wananchi kutokata tamaa na maisha yao kwani Chadema bado ina matumaini ya kuwakomboa hasa pale watakapoungana pamoja na katika kuiondoa CCM madarakani.


Mtanzania

No comments:

Post a Comment