BARAZA la Vijana la CHADEMA (BAVICHA), limesema sera ya majimbo ndio mwarobaini wa kuhakikisha rasilimali zilizopo zinawanufaisha wananchi na taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa BAVICHA Taifa, Deogratias Munishi katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotaka serikali itoe maelezo ya kina kwa vijana na wananchi wa Mtwara kwa ujumla juu ya gesi yao kutaka kusafirishwa Dar es Salaam.
Alisema sera hiyo licha ya kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali za taifa kwa manufaa ya taifa zima, pia inawapa mamlaka wananchi wa eneo husika lenye rasilimali hizo kuamua njia bora za kuzitumia.
“BAVICHA inawataka vijana na wananchi wa Mtwara na Tanzania kwa ujumla kuelewa kuwa mbadala halisi wa sera haramu ya CCM na serikali yake ambayo CHADEMA imekuwa ikiwaeleza wananchi ni ile ya kubadili mfumo wa utawala wa sasa wa kila kitu kuamuliwa Dar es Salaam, na kuweka mfumo mpya unaotokana na sera ya majimbo.
“Kwa sera hii ya CHADEMA ya mfumo mpya ya utawala kwa njia ya majimbo, rasilimali kama ya gesi ingekuwa msaada kwa wananchi wa Mtwara ambako mitambo ya gesi ingefungwa huko na kuzalisha kama ni umeme na kuingizwa kwenye gridi ya taifa,” alisema.
Pamoja na hayo, alisema wananchi wa Mtwara hususan vijana wana haki ya kupinga gesi kusafirishwa Dar es Salaam, ili kuepuka yale yanayotokea kwenye maeneo mengine ya nchi na kutoa mfano maeneo yenye migodi ya dhahabu.
No comments:
Post a Comment