Thursday, March 31, 2016

TAMKO LA WAZIRI KIVULI WA MAMBO YA NJE JUU YA UAMUZI WA SHIRIKA LA MCC KUSITISHA MAHUSIANO NA TANZANIA

TAMKO LA WAZIRI KIVULI WA MAMBO YA NJE JUU YA UAMUZI WA
SHIRIKA LA MCC KUSITISHA MAHUSIANO NA TANZANIA



Kwa Vyombo vya Habari.
Nimesikitishwa na Tanzania kukosa fedha za MCC ambazo zilikuwa ni muhimu sana katika kuharakisha upatikanaji wa umeme kwa Watanzania wa vijijini. Hata hivyo, ningependa kuweka wazi kuwa Tanzania haijaonewa hata kidogo kunyimwa msaada wa Shilingi Trilioni Moja na Shirika la Misaada la Marekani la MCC kama ilivyopotoshwa na Serikali. Kauli ya Waziri wa Mambo Nje, Balozi Agustine Mahiga, ya kuelezea “kushitushwa na kusikitishwa” na uamuzi wa Bodi ya MCC kusitisha msaada na mahusiano yake na Tanzania, ni kauli isiyo ya kidiplomasia, ya kinafiki na inayopaswa kupingwa kwa nguvu zote na kila Mtanzania mwenye kujali kujali utu, demokrasia, utawala bora na ushirikiano mwema baina ya Nchi hii na mataifa mengine.
Nikiwa ni Waziri wa Mambo Nje napinga upotoshwaji na utetezi uliotolewa na Serikali kwasababu zifuatazo;
1. Ni vema ikazingatiwa kuwa MCC inazingatia vigezo 17 katika kuchagua nchi inayostahili kupata msaada na miongoni mwa vigezo vya msingi kabisa ni nchi husika kuwa na dhamira ya dhati ya kuimarisha demokrasia na kuendesha chaguzi zilizo huru na haki. Na katika taarifa yake MCC ilieleza maeneo ambayo Tanzania imekiuka vigezo kuwa ni marudio ya uchaguzi haramu wa urais Zanzibar na kupitisha Sheria ya Makosa ya Mawasiliano ya Mitandaoni –“Cyber Crime”, sheria inayonyima uhuru wa wa kujieleza na uhuru wa kujumuika; nanukuu:

"Serikali ya Tanzania haijachukua hatua za kuhakikisha kuheshimiwa kwa uhuru wa kujieleza na uhuru wa kujumuika katika utekelezwaji wa sheria ya Uhalifu wa Mtandao.”

“Tanzania iliendelea na uchaguzi wa marudio Zanzibar ambao haukushirikisha wote na wala haukuakisi maoni ya wote, licha ya malalamiko kutoka kwa serikali ya Marekani na jamii ya kimataifa”, mwisho wa kunukuu.

Kwa mantiki hii, ni dhahiri kuwa Tanzania haikupaswa “kushitushwa” na uamuzi wa MCC. Serikali ilivifahamu vizuri na mapema vigezo vya kustahili kupewa misaada na MCC. Inashangaza na kusikitisha kuona Msomi na Mwanadiplomasia mzoefu kama Balozi Mahiga akilitia Taifa “Aibu ya Mwaka” kwa kulalamikia “kuonewa” na kutoa kauli za “hovyo” kama alivyozitoa.

Kauli ya Waziri Mahiga, za kukataa kukiri makosa yaliyo dhahiri yaliyofanywa na Serikali na Chama Chake (CCM), zinaweza kabisa kuuweka rehani uhusiano na ushirikiano mzuri wa kidiplomasia ambao Tanzania imekuwa ikiupata kutoka kwa nchi mbalimbali na mashirika ya kimataifa kama MCC. Tukiweka mbele maslahi ya nchi hii yakiwemo ya kudumisha mahusiano mazuri ya kimaendeleo na nchi nyingine, Kambi rasmi ya Upinzani tunaiomba MCC, Marekani na mataifa mengine kuzipuuza kauli za hovyo zilizotolewa na Waziri Mahiga, kwani haziakisi ustaarabu wa Watanzania.

2. Pili, Tanzania si Mbia mgeni kwa MCC. Tanzania ilishapokea awamu ya kwanza ya fedha za msaada kutoka MCC ambazo zilikuwa ni Dola za Marekani milioni 698. Fedha hizi zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa barabara za Tunduma- Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo-Songea-Mbinga. Zilitumika pia kujenga upya mfumo wa huduma za maji kwa ajili ya miji ya Dar es Salaam na Morogoro na kusambaza umeme katika vijiji vya mikoa 10 ya Tanzania Bara. Zilitumika kutandaza njia ya pili ya kusafirisha umeme chini ya Bahari ya Hindi kati ya Bara na Tanzania Visiwani na kujenga barabara zote kuu za Kisiwa cha Pemba na baadhi ya barabara za Unguja kwa kiwango cha lami. Kwa namna yoyote ile isingewezekana kwa MCC walewale kuionea Tanzania ile ile waliyoisaidia katika awamu ya kwanza ya misaada yao. Ni dhahiri kuwa Nchi imepoteza sifa kwasababu zilizoelezwa – na kimsingi sababu zenyewe ni uchu na ulevi wa madaraka uliopitiliza unaofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali yake.

Hatua ya MCC kusitisha uhusiano na Tanzania ni ushahidi tosha kuwa hujuma za uchaguzi na ukiukwaji mkubwa wa demokrasia na utawala bora, unaofanywa na serikali ya CCM na ambao Wapinzani tumekuwa tukiulalamikia mara kwa mara sasa umefikia hatua mbaya zaidi kiasi cha kugusa hisia za jumuiya ya kimataifa.

Ni mtazamo wangu kuwa MCC na jumuiya ya kimataifa bado walichelewa sana kugundua “udhalimu” wa Serikali ya CCM, ambayo karibu mara zote imekuwa ikihujumu haki na uhuru wa watu kwenye chaguzi, na si kwa upande wa Zanzibar tu, bali pia na uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano. Sheria kandamizi zilizopo Tanzania si hiyo ya “Cyber Crime” tu. Tume ya Jaji Francis Nyalali ilibainisha Sheria nyingi kandamizi na kushauri zifanyiwe mapitio ya kuziboresha lakini hadi leo “serikali isiyo ya kidemokrasia ya CCM” imeendelea kuzidumisha sheria hizo na kuongeza nyingine kama hii ya “Cyber Crime”. Natoa rai kwa jumuiya ya kimataifa kutokukubali kurubuniwa tena na serikali ya CCM na badala yake ishirikiane kwa karibu na Watanzania wote wazalendo katika kuboresha misingi ya utawala bora na demokrasia kwenye nchi hii.

3. Tatu, mabalozi wa nchi mbalimbali washirika wa maendeleo ikiwemo Marekani, walishatoa rai zaidi ya mara moja wakiionya na kuishauri Serikali ya Rais Kikwete na baadaye Rais Magufuli kuchukua hatua za kuutatua mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar. Aidha, walishauri mara kadhaa kuwa uchaguzi wa marudio usingeweza kuwa suluhu halali ya kumaliza tatizo la Zanzibar. Badala ya kuchukua hatua hasa za kukisihi Chama chake kuheshimu maamuzi halali ya wapiga kura wa Zanzibar yaliyofanywa Oktoba 25 mwaka jana, Rais wa Jamhuri ya Muungano, John Magufuli, alipuuza rai zote hizo na kwa kiburi cha hali ya juu alisema “hahusiki na suala la Zanzibar”.

Mbali na Mabalozi hao, hata aliyekuwa Waziri wa Mambo Nje wa Serikali ya Awamu ya Nne, Bernard Membe, alionya na kutoa tahadhari kuhusu suala la Zanzibar lilivyokuwa likichukuliwa kwa mzaha-mzaha, badala ya kutatuliwa kwa umakini. Matokeo yake ndiyo haya ya kutengwa na MCC. Inasikitisha kuona Serikali ya Magufuli ikiwa na uweledi finyu katika medani ya diplomasia ya kimataifa na kuupuza nchi rafiki.

Uamuzi wa MCC unapaswa kuchukuliwa kwa tahadhari kubwa na Serikali. Nchi nyingi rafiki ni nchi zinazosimamia misingi ya utawala bora na demokrasia na zilishaonyaonyesha kutoridhishwa na suala la Zanzibar na Sheria ya Cyber Crime. Naonya kuwa upo uwezekano kwa nchi wahisani, kila moja kwa nafasi yake, kuchukua uamuzi kama uliochukuliwa na MCC wa kusitisha ushirikiano wa kimaendeleo na Tanzania, kama hatua za dharura hazitachukuliwa kurekebisha hali ya mambo

USHAURI KWA SERIKALI
Kambi rasmi ya Upinzani siku zote tumekuwa msitari wa mbele kuitaka serikali na vyombo vyake ijenge uwezo endelevu wa kujitegemea. Hata hivyo, ni ukweli ulio dhahiri kuwa wakati tukijenga uwezo wa kujitegemea, bado tunahitaji kuutumia vizuri ushirikiano wa kutegemeana na nchi rafiki na mashirika ya kimataifa. Tanzania haiwezi kuishi kama Kisiwa, hii ni Dunia ya kuhitajiana.
Trilioni Moja za MCC ni muhimu katika kuharakisha usambazaji umeme vijijini. Tanzania inataka kufikia hadhi ya kuwa nchi yenye uchumi wa kiwango cha kati kama ilivyo India na Malaysia ifikapo mwaka 2025 kwa mujibu wa Dira ya Taifa. Nchi hizi tunazotaka kuzifikia nazo zinajenga uwezo zaidi wa kimaendeleo kwa kutegemeana pia na nchi na washirika wengine wa kimaendeleo. Serikali isijifanye haitaki misaada wakati ukweli ni kuwa bado Bajeti yetu ya nchi inahitaji kusaidiwa na nchi rafiki. Ni wakati wa Serikali kuacha kauli za hovyo na kuchukua maamuzi magumu ya kujirekebisha kama ifuatavyo.
1. Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Dr. Mohamed Shein wanapaswa kuonyesha kuwa wanawapenda zaidi Watanzania kuliko wanavyovipenda vyeo vyao vya kulazimisha. Dk Shein akatae kuburuzwa, akatae kuanzia sasa kubeba laana ya dhuluma na kusababisha Tanzania na Zanzibar zitengwe. Namshauri achukue uamuzi wa kishujaa wa kujiuzulu urais haramu wa Zanzibar, ili apishe mazungumzo mapya ya kutafuta muafaka Zanzibar.
2. Serikali ilete muswada Bungeni wa kurekebisha Sheria ya Makosa ya Mitandaoni na Sheria nyingine zote kandamizi kama zilivyoainishwa na Tume ya Jaji Nyalali.
3. Serikali ianze bila kuchelewa kutekeleza mchakato wa kupata Katiba Mpya kwa kuanzia pale ilipoishia Tume ya Jaji Warioba, vinginevyo naonya kuwa madai na kishindo kipya cha vuguvugu la Katiba Mpya ambalo Wapinzani tunakusudia kulianzisha upya, linaweza kuiweka Tanzania katika picha mbaya. Tunaitaka serikali itupe ushirikiano katika kujenga demokrasia na utawala bora kwenye nchi hii.

Imetolewa Na:
Mchungaji Peter Simon Msigwa (Mbunge)
Waziri Kivuli – Wizara ya Mambo Nje na Ushirikiano wa Kimataifa

Tuesday, March 29, 2016

Msife moyo, uchaguzi ni mchakato, si tukio – Mbowe

FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amewashauri Watanzania wasife moyo kwa matokeo mabaya ya uchaguzi yaliyopinduliwa; na kwamba matokeo hayo yawe chachu ya kufanya vizuri zaidi katika uchaguzi ujao, anaandika Josephat Isango.

Amesema uchaguzi si tukio, bali mchakato; na kwamba kama kuna watu wamekufa moyo kwa sababu ya kilichofanywa na serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupindua matokeo, hasa ya urais, watafakari upya na wajipange kwa kazi kubwa inayokuja, kwani mafanikio ya kisiasa hayapimwi kwa tukio moja la uchaguzi na matokeo yake. Alisema matokeo hayo yanapswa kuwatia hasira na kuwahamasisha waendelee kupambana,

Mbowe amesema hayo Masaki, nyumbani kwa Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa Zamani ambaye pia alikuwa Mgombea Urais wa Chadema aliyeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwenye hafla ya kumshukuru Mungu iliyoandaliwa na familia hiyo. Ukawa unaundwa na Chadema, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD.

“Hatukushinda serikali kuu kama tulivyokusudia na kupenda iwe kwa sababu ambazo si wakati wake kuzisema sasa, lakini ni vema tukumbuke kwamba mapambano tunayofanya, kama kuna yeyote miongoni mwetu anafanya kwa ajili yake binafsi, ana wajibu wa kujitafakari upya,” amesema Mbowe.

Aliongeza kwamba, kazi ya mapambano wanayofanya viongozi sasa ina manufaa kwa kizazi kijacho, na kama wanaoifanya sasa wakafanikiwa kuonja matunda ya kazi ya mikono yao basi ni jambo la kumshukuru Mungu.

“Kazi anayofanya Lowassa (Baba Kadeti) si lazima aone matunda yake leo, huenda mtoto wake ataonja na asipoonja Kadeti basi wajukuu wataonja matunda hayo na kutambua mchango mzuri wa babu yao kwa kazi kubwa ya maana anayofanya sasa,” amesema.

Aliwahimiza Watanzania zaidi ya 600 waliokuwepo kwenye halfa hiyo kuwa wale walio wafuasi wa vyama vya siasa hata wasio na vyama wana wajibu wa kuendelea kwa nguvu zote na kazi ya kupambana ambayo Lowassa amejiunga nayo, kwani wakati wa uchaguzi watu wengi walipigana kumsaidia sio kwa ajili ya familia yake ila walifanya vile kwa sababu ya nchi hii, huku Lowassa akiwa kiongozi na mpeperusha bendera.

Mbowe alitumia fursa hiyo kuwataka watanzania waendelee kumwombea neema, ujasiri na afya njema Lowassa kwani taifa bado linamhitaji kuliko pengine anavyohitajika na familia yake.

Aidha, Mbowe alimsifu pia Regina, mke wa Lowassa, kwa ujasiri wake na familia nzima kwa uamuzi mzuri na ujasiri aliochukua katika kuhakikisha Watanzania wanatafuta haki na ujasiri kwa kukata minyororo ya watesi.

“Mama ulikuwa mwoga kwenye kampeni katika hatua za awali, lakini baadaye ulipata ujasiri kama mgombea mwenyewe. Asante sana kwa kuondoa woga; asante kwa kuongoza familia, na sasa tuendelee na mapambano.” alihimiza Mbowe

Kabla ya Mbowe kusimama, neno la kuwashukuru watu waliofika nyumbani lilitolewa na Regina akasema familia, hasa Lowassa mwenyewe, ilikuwa inasubiri kwa hamu siku ya kumshukuru Mungu na Watanzania kwa mazuri mengi aliyowatendea.

Hafla hiyo ya shukrani ilianzia kwa ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Azania Front, Dar es Salaam. Lilichagizwa na nyimbo kadhaa za shukrani zilizopendekezwa na Lowassa mwenyewe, na kuimbwa na washiriki wote, wakiwamo wa madhehebu mengine ya dini.

Miongoni mwa washiriki wa hafla hiyo ni baadhi ya wanachama wapya wa UKAWA waliojiengua CCM mwaka jana, wakiwamo Hamisi Mgeja, Mgana Msindai, Lawrence Masha, John Guninita, na wengine.

Ilihudhuriwa pia na wanasiasa, viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali, vijana na wazee, matajiri na watu wa kawaida kutoka sehemu mbalimbali.

“Tumepata mengi mazuri, tunaweza kusafiri kwenda Monduli na kurudi si sababu tuna magari mazuri kuliko wengine; tunaweza kusafiri kwa ndege na tukarudi salama, lakini hata wakati mwingine unasikia mtu anakupigia simu kukusalimu au kukuandikia ujumbe mzuri wa faraja, haya yote ni sababu ya Mungu na tukaona leo tufike Kanisani kusema Mungu asante kwa mema yote uliyotujalia,” alisema Regina akiwa amejawa tabasamu muda wote, huku akishangiliwa.

Wajukuu wa Lowassa walijumuika kumwimbia babu yao wimbo kutoka miongoni mwa tenzi za Injili zilizoandaliwa kwa ajili hiyo, huku wakiongozwa na mpiga kinanda.

Baada ya wajukuu, Masha alitumbuiza washiriki kwa wimbo wa Kiingereza “Amazing Grace,” akatuzwa kiasi cha Tsh. 50,000 ambacho, hata hivyo, alikigawa kwa wajukuu wa Lowassa.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, Lowassa alikuwa mgombea urais mwenye mvuto kuliko wote, lakini aliibuka mshindi wa pili katika matokeo yenye utata, akiwa nyuma ya John Magufuli.

Taarifa za chini chini zinasema kuwa matokeo hayo yalipikwa. Tume ya Uchaguzi ilitangaza kuwa Lowassa alipata kura 6,072,848 ikiwa ni asilimia 39.97 ya kura zote, huku Magufuli akipewa kura 8,882,935 ikiwa ni asilimia 58.46 ya kura zote.

MwanaHalisiOnline

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA KUHUSU HATMA YA MSAADA WA FEDHA ZA MCC KWA SERIKALI YA TANZANIA


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA

KUHUSU

HATMA YA MSAADA WA FEDHA ZA MCC KWA SERIKALI YA TANZANIA

Mnamo Desemba 16, mwaka jana, Bodi ya MCC katika kikao chake iliazimia kuahirisha msaada wa USD Mil. 472.8, uliokuwa umekusudiwa kwa ajili ya Tanzania kwa mwaka 2016, ambao ulilenga kusaidia sekta ya nishati ya umeme, hususan maeneo ya vijijini, pia katika kuunganisha wateja wapya na mabadiliko ya kimuundo ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO) ili lifanye kazi na kutoa huduma kwa ufanisi katika sehemu za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji.

Fedha hizo pia zilikusudiwa kusaidia kuanza kwa mpango mkubwa wa kuboresha sekta ya umeme nchini 2014-2024.

Sababu zilizotumiwa na MCC kuahirisha msaada huo zilikuwa ni pamoja na;

1. Mkwamo wa Uchaguzi wa Rais na Wawakilishi Zanzibar na

2. Matumizi mabaya ya Sheria ya Makosa ya Mtandao hususan

kuhusiana na uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

wa 2015.

Taarifa zilizopo ni kwamba Bodi ya MCC inakutana tena Machi 28, mwaka huu, ambapo pamoja na masuala mengine pia itajadili mchakato wa msaada kwa Serikali ya Tanzania.

Bodi hiyo ya MCC inakutana katika wakati ambapo hakuna hatua zozote za maana zimechukuliwa na Serikali ya Tanzania kurekebisha sababu zile mbili ambazo ziliisukuma bodi hiyo kuahirisha msaada ule mwaka jana.

Sheria ya Makosa ya Mtandao na nyingine zinazofanana na hizo zinazolenga kufifisha uhuru wa habari na kupashana taarifa bado ziko vile vile na hivi karibuni zimetumika hata kufuta kabisa Gazeti la Mawio na kutisha vyombo vingine vya habari pamoja na wanahabari wanaotekeleza wajibu wao kwa jamii.

Hali ya mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar imezidi kuwa tete zaidi baada ya Serikali ya CCM kukanyaga demokrasia na kulazimisha kurudia uchaguzi bila msingi wowote unaotokana na uhalali wa kisheria au kisiasa wa kufanya hivyo.

Hivyo basi, wakati Bodi hiyo inakutana kuamua masuala kadhaa ikiwa pamoja na kuhusu hatma ya msaada huo kwa Tanzania, tunapenda kusema yafuatayo katika hatua ya sasa;

Kwa kuwa hadi sasa Serikali haijaonesha nia yoyote ya kupeleka bungeni marekebisho ya sheria mbovu zilizotungwa kwa makusudi kuua uhuru wa habari na maoni/mawazo mabadala, ikiwemo ile ya Makosa ya Mtandao.

Kwa kuwa Serikali badala ya kuziondoa sheria hizo mbovu, imezidi kuzitumia kutisha watu, wakiwemo waandishi wa habari, vyombo vya habari ina sasa imekwenda hatua kubwa zaidi hata ya KUFUTA chombo cha habari (Gazeti la Mawio).

Kwa kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano chini ya Rais Magufuli imeamua kupuuza kabisa maoni ya Watanzania waliotaka imalize mgogoro wa kisiasa nchini Zanzibar kwa kumtangaza mshindi halali aliyepatikana katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka jana.

Kwa kuwa Serikali ya Tanzania, kinyume kabisa na misingi ya uhalali wa kisheria na kisiasa imeamua kusigina demokrasia huko Visiwani na kulazimisha kurudia uchaguzi ambao tayari ulishafanyika.

Kwa sababu Serikali ya Tanzania haijatambua umuhimu wa sheria zinazotenda haki, kuzingatia demokrasia na utawala bora kuwa ni misingi imara ya amani na utulivu wa kweli, maendeleo chanya na ustawi wa jamii;

Tunaamini kuwa Bodi ya MCC itaungana na Ubalozi wa Marekani pamoja na Mabalozi wa Nchi za Jumuiya ya Ulaya nchini Tanzania, Kulaani kilichofanyika Zanzibar.

Kuendelea kutoa wito kwa Serikali kufuta au kuzifanyia marekebisho sheria zinazolenga kuua uhuru wa habari na maoni kwa ujumla.

Kuitikia wito wa kuendelea kuahirisha mchakato wa msaada huo kwa Serikali ya Tanzania hadi hapo Serikali hii itakapoona umuhimu wa kuwa na mwafaka wa kitaifa kuamua hatma ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla wake, yenye amani na utulivu unaosimama katika misingi ya demokrasia na uongozi bora unaozingatia sheria zinazotenda haki.

Pamoja na mambo mengine, bodi hiyo izingatie na kujiridisha iwapo Serikali ya Tanzania imeamua kutambua umuhimu wa misingi hiyo katika kuondoa chembechembe za udikteta zinazoanza kuonekana kutoka kwa utawala wa awamu ya tano.

Itakumbukwa kuwa Bodi ya MCC ilipoamua kuahirisha mchakato wa kuipatia fedha Serikali ya Tanzania, mwaka jana, CHADEMA tulitoa kauli kuwa kuchelewa kupatikana kwa fedha za MCC si tu kunachafua jina la nchi na hadhi yake katika medani za kimataifa, bali kutaathiri kwa kiasi kikubwa miradi yote iliyo chini ya ufadhili wa MCC.

Kuhusu Sheria ya Makosa ya Mtandao


Tulisema pia kuwa Sheria ya makosa ya mtandao (Cyber Crime Act 2015) ni sheria mbaya sana inayokinzana na kukua kwa technolojia ya habari na mawasiliano ambapo watawala chini ya utawala wa CCM, walilenga kwa makusudi kuua uhuru wa kupeana taarifa na kupashana habari.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa sheria hiyo ilipitishwa usiku wa manane kwa ubabe wa wabunge wa CCM na hata tulipomtaka Rais Jakaya Kikwete kwa maslahi mapana ya taifa asiisaini, aliisaini kibabe akijua anaandaa mazingira gani ya ‘kihalifu’ dhidi ya uhuru wa kutafuta, kupokea na kusambaza taarifa, wakilenga kudhibiti kijinai uchaguzi mkuu uliopita.

Sheria hiyo ilitumika kuhalalisha ‘uvamizi’ wa vituo vya CHADEMA vilivyokuwa vikitumika kukusanya matokeo ya kura za rais na wabunge na hadi leo vijana zaidi ya 161, wakiwemo wanafunzi, wana kesi za “kubumba” mahakamani, huku CCM wakiwa na vituo vilivyokuwa vikifanya kazi hiyo hiyo na Jeshi la Polisi halikudhubutu kuvizuia achilia mbali kuwakamata waliokuwemo na kuwafungulia kesi.

Ni sheria hiyo hiyo ilitumika kuficha dhana ovu iliyotumika kuhalalisha kuvamia Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilichokuwa kikiratibu watazamaji wa uchaguzi wa ndani kwa kibali cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Tulitoa rai kwa Rais John magufuli kuchukua hatua za kiuongozi kuifanyia marekebisho makubwa Sheria ya Makosa ya Mtandao kupitia bungeni, pia kumuagiza DPP kuzifuta kesi ambazo watu wamebambikiwa kutokana na sheria hiyo mbovu.

Kuhusu Zanzibar

Tulimtaka Rais Magufuli aingilie kati na kumaliza mgogoro wa kisiasa uliokuwa unaiweka Zanzibar katika hali tete ambapo wito wetu ulisisitiza kuhakikisha kuwa mshindi halali aliyepatikana katika uchaguzi mkuu mwaka jana natangazwa badala ya kuiacha nchi katika sintofahamu na kulazimisha uchaguzi wa marudio bila kuwepo na uhalali wowote wa kisheria wala kisiasa kufanya hivyo.

Imetolewa leo Jumatatu, Machi 28, 2016 na;

Idara ya Habari na Mawasiliano

CHADEMA

Wednesday, March 23, 2016

Haikuwa kazi rahisi Umeya Dar

HAIKUWA kazi rahisi kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kukiangusha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam,anaandika Happyness Lidwino.
Wafuasi na wanachama wa Ukawa leo mapema walifika katika Ukumbi wa Kareemje kushugudia uchaguzi wa Meya.
Ulinzi ulikuwa mkali getini huku wananchi wakizuiwa kuingia ukumbuni, viongozi na wajumbe waliotakiwa kupiga kura waliingia kwa kukaguliwa na polisi.
Mara baada ya wajumbe wa pande zote kuwasili ukumbini humo, mkutano ulifunguliwa saa 4:37 asubuhi na kura zilianza kupigwa huku Edward Lowassa, aliyekuwa mgombea wa urais kupitia Ukawa akishuhudia tukio hilo.
Mara baada ya wajumbe kumaliza kupiga kura kabla ya kuhesabiwa, wajumbe wa CCM walianza walinyanyuka na kutoka nje.
Hali hiyo iliwashangaza wengi waliokuwa ukumbini humo, walipofika nje ya ukumbi walianza kuzomewa na wafuasi wa Ukawa.
Safari hiyo ikahitimishwa kwa Isaya Mwita Charles (Chadema) kutwaa nafasi hiyo kwa kura 84 na kumbwaga mpinzani wake Yusuph Omary Yenga (CCM) aliyepata kura 67.
Safari ya mafanikio ya Ukawa katika Jiji la Dar es Salaam ilitawaliwa na vuta nikuvute. Kulikuwa na michezo michafu.
Jeshi la Polisi pamoja na Halmashuri ya Jiji la Dar es Salaam vililaumiwa kwa madai ya kushiriki katika hujuma zilizokuwa zikifanywa na CCM kutaka kushinda kwa hila nafasi hiyo.
Jumla ya wajumbe wa mkutano wa kumchagua Meya wa Jiji ni 163. Kwa upande wa Kinondoni kulikuwa na wajumbe 58; CCM wakiwa 20 na Ukawa 38. Temeke jumla ya wajumbe 49, CCM wakiwa 31 na Ukawa 18 na Ilala jumla ya wajumbe 54 huku CCM wakiwa 23 Ukawa 31.
Umoja na mshikamano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF) ndio umeiangusha CCM.
Safari ya Ukawa kusaka nafasi ya Umeya katika Jiji la Dar es Salaam ilianza tarehe 23 Januari wakati Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilipoitisha uchaguzi huo kwa mara ya kwanza.
Kwa mara ya kwanza uchaguzi huo uliitishwa tarehe 23 Januari na kusindwa kufanyika kutokana na kuwepo kwa mvutano wa wajumbe halali wa uchagzi huo.
Mzozo huo uliibuka baada ya CCM kuingiza wajumbe kutoka Zanzibar na kutaka kuwa sehemu ya wapiga kura, hatua hiyo iligomewa na Ukawa na kusababisha kuanza kwa mnyukano.
Hatua hiyo ilimlazimu Sarah Yohana, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kughairisha uchaguzi huo ambapo alipanga kufanyika tarehe 8 Februari mwaka huu.
Licha ya Sarah kuitisha uchaguzi huo tarehe 8 Februari mwaka huu, Sarah alighairisha uchaguzi huo kwa madai ya kuwepo kwa zuio la mahakama
lililopelekwa katika Mahakama ya Kisutu Februari 5 na mwanachama wa CCM.
Sarah kwa nafasi yake, aliitisha uchaguzi huo tarehe tarehe 27 Februari mwaka huu na baada ya taratibu zote kufuatwa, alisimama na kughairisha uchaguzi huo kwa madai ya kuwepo kwa zuio kutoka mahakamani jambo ambalo liliibua vurugu.
Wabunge, madiwani kukamatwa
Tuhuma ziliibuka kwa wajumbe wa Ukawa kwamba walishiriki kumshambulia Terresia Mmbando, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kughairishwa kwa uchaguzi huo wa tarehe 27 Februari mwaka huu.
Tuhuma hizo zilisababisha baadhi ya wabunge na madiwani wa Ukawa kukamatwa na Jeshi la Polisi na baadaye kufikishwa mahakama kujibu tuhuma hizo.
Kundi la kwanza kukamatwa lilikuwa ni Halima Mdee, Mbunge wa Jimbo la Kawe, Mwita Waitara ambaye ni Mbunge wa Ukonga na madiwani watatu na kisha kufikishwa katika Mahakama ya Kisutu.
Jeshi la Polisi kisha lilimkamata Saed Kubenea, Mbunge wa Ubunge kwa tuhuma zile zile za kumshambulia Mmbando, watuhumiwa wote wapo nje kwa dhamana.
Hatua ya vuta nikuvute iliyofanywa na jiji ilionywa na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema-Taifa kwamba ina madhara na kwamba, hawatoomba ila watachukua nafasi hiyo.
George Simbachawene, Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) alichoshwa na hali hiyo ambapo alimtaka Sarah kuitisha uchaguzi huo kabla ya tarehe 23 mwezi huu.
Katika hali ya kuonesha kuelemewa, Rais John Magufuli alishauri ‘walioshindwa washindwe na walioshinda washinde.”Mafanikio ya Ukawa leo katika Jiji la Dar es Salaam alianza siku nyingi.

Sunday, March 20, 2016

TAMKO LA KULAANI KUTEKWA KWA MWANAHABARI BI SALMA SAID

TAMKO LA KULAANI KUTEKWA KWA MWANAHABARI BI SALMA SAID

Waziri kivuli wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Mh Joseph Mbilinyi

Tanzania na dunia nzima inaelewa kuwa marudio ya uchaguzi wa Zanzibar ni batili. Na kwa kuwa uchaguzi huu ni batili, watawala yaani Chama cha Mapinduzi kimeingia katika historia ya kipekee duniani kwa kuwanyima haki wananchi wake.

Matukio mbalimbali yanayoendelea Zanzibar ikiwemo matumizi ya nguvu, vitisho na hata vitendo vya kikatili dhidi ya wanaosimamia haki, vinaendelea kuitia Serikali ya CCM doa si kwa taifa letu tupekee bali pia kwa dunia nzima.

Tukio la kutekwa kwa mwanahabari Bi Salma Said wa Deutsche Welle (DW) kimezua maswali makubwa lakini hofu kubwa kwa wananchi, familia yake na wadau hasa wanahabari wa ndani ya nchi na jumuia za kimataifa. Ni dhahiri kuwa kutekwa kwa Bi. Salma Said kunatokana na kazi yake ya uanahabari na ndio maana ushahidi wa awali ambao umepatikana kwa njia ya ujumbe wa sauti ukiwa na sauti inayoaminika kuwa ni yake, unaelezea wazi kutekwa kwake kunatokana na yeye kuripoti dosari zinazoendelea hasa katika uchaguzi batili wa marudio ya Zanzibar.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inalaani kwa nguvu zote kitendo cha utekaji wa mwanahabari huyu kutokana na kazi yake. Aidha, tunaitaka Serikali kuhakikisha kuwa mama, dada, rafiki na ndugu yetu Bi Salma Said anapatikana akiwa salama.
Tunaendelea kuamini kuwa kuchelewa kupatikana kwa Bi Salma Said na ukimya wa vyombo vya Serikali na Usalama ni matokeo ya uminyaji wa demokrasia kwa wale wasiofanya kazi kwa mashinikizo ya Chama tawala.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, itaitisha maandamano makubwa nchini ili kushinikiza upatikanaji wa haraka wa Bi Salma Said lakini pia kupaza sauti kwa ulimwengu kuwa Tanzania si mahali salama kwa wanahabari.

Kwa niaba ya Kambi ya Upinzani Bungeni, tunaungana na watanzania wote hasa familia ya Bi Salma Said na watu wote wenye mapenzi mema kumuombea heri Bi Salma na kuamini kuwa atapatikana akiwa Salama Salmin na kuwatia hatiani watekaji wake.

Imetolewa na,
Joseph O. Mbilinyi (MB)
Waziri Kivuli wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo.
19/03/2016

Friday, March 18, 2016

Uchaguzi wa Meya Dar waota mbawa

UCHAGUZI wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam bado ni kitendawili licha ya Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kuwa na idadi kubwa ya wajumbe kuliko Chama Cha Mapinduzi (CCM) lakini bado hawaishi vikwazo, anaandika Happyness Lidwino.

Wajumbe halali walioshiriki katika uchaguzi wa mameya wa Halmashauri za Manispaa Jijini ni 163 huku CCM wakiwa 76 na Ukawa 87, kwa hivyo Ukawa kuwazidi CCM wajumbe 11.

Akizungumza na waandishi leo Jijini Mwita Waitara Mwenyekiti wa Mkoa wa Dar es Salaam Kuu ‘’The Great Dar’’ amesema wanashangazwa na mbinu zinazotumiwa na CCM kwa kuwashirikisha watumishi wa serikali katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema CCM wanafanya kila mbinu ili kulipoka Jiji licha ya kuwa na idadi ndogo ya wapiga kura. Mbinu hizo pia wamemshirikisha Willson Kabwe Mkurugenzi wa Jiji kuvunja sheria katika majukumu yake.

Mbinu nyingine waliyoitumia ni kuwaandaa wanachama feki wa CCM wakiongozwa na wakili Elias Nawela kufungua kesi ya madai huku wakitaka wajumbe 9 toka Zanzibar na 11 kutoka mikoa mingine kushiriki uchaguzi wa meya.

Waitara amesema, kesi hiyo yenye jarada namba 39 ya mwaka 2016 wameshaomba kujiunga na kesi hiyo huku wakiwa na mawakili wa kutosha ambapo inatarajiwa kusomwa Machi 21 mwaka huu katika Mahakama ya Kisutu.

‘’CCM haina ujanja kwa sasa kwani tunapambana nao, na hatutakubali wajumbe wasiohusika kupiga kura wakati ni kinyume cha sheria ya Serikali za Mitaa za mwaka 1982 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2006,’’ amesema Waitara.

‘’Juzi tumepokea barua kutoka kwa Mkurugenzi ya mwaliko wa ushiriki katika uchaguzi wa meya wa Jiji lakini ndani ya barua hiyo kuna kitu hatujakubaliana nacho. Barua inaeleza uchaguzi utafanyika Machi 22 mwaka huu ukumbi wa Kareemjee lakini wanaotakiwa kuingia ni wajumbe tu,.

Wananchi na wafuasi wa vyama hawataruhusiwa kushuhudia ucha guzi huo. Tunajua hizo ni mbinu za CCM kwa kuwa kuna uovu umepagwa kufanyika siku hiyo.

Kufuatia hali hiyo Waitara amesema Ukawa umemwandikia barua Mkurugenzi huyo ya kutokubaliana na matakwa yake ya kuzuia wafuasi wa vyama kuingia ukumbini wakati wa uchaguzi kwani ni uvunjifu wa sheria na kwamba hawatakubali, bali watawapigania na kuhakikisha wananchi wanaingia ukumbini.

Aidha, kuhusu kesi iliyopo mahakamani watahakikisha sheria inafutwa hata kama uchaguzi utapelekwa mbele lakini hawatakubali kuruhusu mamluki wa CCM kuingia ukumbini kwani wao hawatashiriki uchaguzi huo.

Wednesday, March 16, 2016

Katibu mpya Chadema: Nilibuni kaulimbiu 'Mabadiliko - Lowassa'

Wakati wengi wakizidi kuhoji uwezo wa Katibu Mkuu mpya wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, kutokana na kutokuwa na jina kubwa katika uwanja wa siasa, mbali na elimu aliyonayo, kipaji chake na uwezo binafsi, vimezidi kufichuka.

Mwishoni mwa wiki, Chadema ilimteua Dk. Mashinji kuwa Katibu Mkuu mpya kushika nafasi ya Dk. Wilbroad Slaa aliyejiuzulu nafasi hiyo Julai 30, mwaka jana kwa kile akichodai kuwa ni utaratibu kutofuatwa wa kumkaribisha Edward Lowassa, aliyehamia katika chama hicho kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kisha kuteuliwa kuwa mgombea urais kupitia chama hicho akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Hata hivyo, wakati wengi wakihoji uwezo wake, imefahamika kuwa Dk. Mashinji kwa kushirikiana na kamati yake, ndiyo waliobuni kaulimbiu (slogan), ya `Lowassa Mabadiliko, Mabadiliko Lowassa,' ambayo ilitumika katika kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana na kuwa kivutio kikubwa.

Akihutubia mamia ya wananchi wa Jiji la Mwanza katika viwanja vya Furahisha, Katibu Mkuu huyo, alisema: "Katika mkakati wetu kama kamati ya wataalam, tulileta kauli ya Mabadiliko Lowassa, Lowassa Mabadiliko, wameiiga, lakini hawawezi kuwa kama sisi, tunamaanisha mabadiliko tunayoyazungumzia na tutayatekeleza kimkakati na kimfumo zaidi."

Mbali na hilo, kati hiyo ya ndiyo iliyofanikisha maafikiano tisa ya Ukawa pamoja na suala zima la chama kipi kipewe nafasi ya kusimamisha umeya katika umoja huo.

Kauli hiyo ambayo hadi sasa inatumika kwenye vikao vya ndani, nje na mikutano ya hadhara vya Chadema, alishirikiana na Kamati ya Wataalam ya Ukawa ambayo imekuwa ikibuni na kushauri mambo mbalimbali ya uendeshaji wa umoja huo.

Katika umoja huo unaohusisha vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD, kamati ya wataalam iliongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu na Makamu wa Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania, Dk. Rodrick Kabangila na Makamu akiwa Dk. Mashinji na Katibu alitoka CUF.

AELEZA SAFARI YAKE NA DK. MASHINJI
Dk. Kabangila, alisema alikutana na Dk. Mashinji Chuo Kikuu cha Makerere, nchini Uganda, akiwa mwaka wa tatu naye wa pili, wakishirikiana kwenye uongozi wa Umoja wa Wanafunzi wa Tanzania wanaosoma chuoni humo.

Baada ya kurudi nchini walikutana tena Muhimbili na kuendelea kushirikiana ikiwamo kuandika majarida mbalimbali ambayo walimpelekea Mbowe kwa ajili ya utekelezaji.

Anasema mwaka 2011, baada ya kujiondoa katika Chama cha Madaktari nchini, baada ya kuona mgongano mkubwa na kutoeleweka katika wanayoyapigania, aliingia kwenye siasa na kwa pamoja waliwekwa kwenye Kamati ya Afya ya Chadema, yeye akiwa mwenyekiti na Mashinji akiwa makamu mwenyekiti.

Alisema baada ya kufanya vizuri kwenye kamati hiyo, walipewa Kamati ya Maandalizi ya Ilani ya Chadema, nako alikuwa mwenyekiti na mwenzake makamu.

AMFAGILIA DK. MASHINJI
Alisema Dk. Mashinji ni mtu sahihi kwa Chadema kwani ni makini, mwandishi mzuri, anasoma kwa makini machapisho mbalimbali, amesimamia miradi mikubwa ya mabilioni ya fedha na ilileta matokeo chanya, anaijua neno kwa neno katiba na ilani ambayo alishiriki kuiandika na anajua inavyoweza kutekelezwa na miongozo mingi wameiandaa pamoja.

AMPONDA DK. KIGWANGALLA
Dk. Kabangila, alimshangaa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. Hamis Kingwangala, ambaye amendika kwenye ukurasa wake wa Facebook akimponda Dk. Mashinji, na kwamba wakati wa mgomo wa mwaka 2005 alikuwa ni mwanafunzi aliye katika mafunzo ya vitendo (internship) na kwamba mgomo huo uligawanyika katika maeneo matatu ya wanafunzi wanaofaya mafunzo kwa vitendo, daraja la kati na wakongwe, na kwamba Dk. Mashinji alikuwa katika daraja la juu na alisimamia masuala ya ngazi hiyo.

Alisema katika mgomo wa mwaka 2011, walikuwa na Dk. Kigwangalla, yeye (Kabangila) akiwa ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Madaktari Tanzania na Makamu wa Rais, na walishirikiana wote na Dk. Mashinji kwa kuwa ni miongoni mwa watu waliokuwa na misimamo thabiti, mtendaji makini na mfuatiaji wa mambo.

"Namshangaa sana Dk. Kingwangalla, sijui ni siasa inamlevya au baada ya kuwa waziri anasahau kabisa jinsi walivyopambana kuboresha sekta ya afya na maslahi ya madaktari nchini, unapokuwa mtaalam unapaswa kupinga kitaalam na siyo kusema mambo kirahisi rahisi na pasipokuwa na taarifa kamili, kwa sasa inaonekana amesahau kabisa udugu wa kitaaluma tuliofundishwa na tunapaswa kuuhubiri. Ukweli anaujua ila anajilazimisha kutoujua," alisema.

Tuesday, March 15, 2016

TUKIO LA KUMTAMBULISHA RASMI KATIBU MKUU WA CHADEMA VICENT MASHINJI LILILOFANYIKA MWANZA










Lowassa analea amani ya nchi

KIMSINGI, kuna tofauti kubwa kati ya binadamu mmoja na mwingine kwenye mambo mengi. Hii ifahamike hivi, anaandika Adam Mwambapa.

Kama ilivyo kwangu na kwako, ndivyo ilivyompendeza Mwenyezi Mungu kwamba, binadamu tuwe sawa kwa mwonekano na maneno au pengine hata matendo; wakati kiundani ni tofauti kabisa.

Ni ukweli usiopingika nikisema, hata mapacha waliozaliwa siku moja na saa moja, isipokuwa kwa kupishana sekunde tu. Pia na wao hawako sawasawa kwa kila kitu.

Yule ni yule na huyu ni huyu. Waingereza wanatumia neno zuri sana, kuwakilisha utofauti wa kitu kimoja na kingine wakisema ‘unigue’.

Ndilo neno linaloonesha upekee wa mtu, na ndilo linaloleta tofauti kati ya mtu mmoja na mwingine. Hata kama kimtazamo wako na mwonekano, vitu viwili utaviona ni kama viko sawa hivi.

Kwa Rais Dk. John Magufuli pia na kwa aliyekuwa mshindani wake wa jirani, katika mbio au kinyang’anyiro cha urais, kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana, Edward Lowassa; pia wana utofauti mkubwa na hawafanani.

Hata kama walikuwa na nguvu zinazokaribia kuwa sawa, wote wakitumia maneno ya kuleta mabadiliko, ingawa Magufuli aliiga, hawako sawa kwa mambomengi.

Lakini kuna tofauti ya ndani ambayo nguvu na mamlaka yao, kamwe haviwezi kuwa sawa. Kama nitakavyofafanua.

Kuna vitu vinajulikana zaidi kwa jina la ‘nafsi’ na kingine kinajulikana kwa jina la ‘nafasi’, asilani vitu hivi havifanani na vina maana tofauti pia. Ingawa, katika hali ya ubinadamu, wapo wanaovichanganya kwa kuvielezea maana yake iko sawa na vinafanana. Ukweli havifanani kabisa.

Wakati tafsiri nzuri ya ‘nafsi’ ni ‘hakika’. Tafsiri ya ‘nafasi’ ni ‘kujaaliwa’ au ‘Iliyojaaliwa/imejaaliwa. Kwa maana hiyo basi, ukiyachanganya, ukisema ‘nafsi nafasi’ maana yake ni ‘baraka’.

Na ukisema, ‘nafasi nafsi’ ni ‘neema’. Kwa maana ya kwamba, nafasi inachukua tafsiri ya neno lingine na kuwa eneo, wakati huo nafsi inaweza kuchukua tafsiri nyingine inayoweza kueleweka kama mtu.

Pengine niseme hivi, huenda nitaeleweka vizuri, katika kitu chochote ni lazima kuanze na vitu hivi viwili.

Ikiwa ilianza kuweko ‘nafasi’ kabla ya ‘nafsi’ kuwepo, basi nafasi ndicho kitu cha kwanza na ndipo nafsi hufuata baadaye. Vivyo hivyo, ikiwa kama nafsi ilianza kuweko mahali, basi nafasi ndiyo huja baada ya nafsi kuwepo.

Ni wachache sana wasiojua au kuelewa kuwa, kabla ya Dk. Magufuli kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya urais, Lowassa, tayari alikuwa kwenye eneo hilo.

Na alikuwa amechukua fomu na hivyo akatangulia kuwako na kuwa sehemu ya nafsi akiisubiri nafasi tu kupata alichokuwa akikihitaji; na baadaye ndipo akaingia Rais Magufuli kuchukua fomu.

Kilichofuata wengi wanafahamu fika kwamba, baadaye Lowassa aliingia kwenye mchujo mkali. Au wa kutopendwa na pengine kuhofiwa, na jina lake likafanyiwa figisu-figisu na kuondolewa.

Hali iliyompa nafasi Dk. Magufuli kuwa chaguo la Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuteuliwa kuipeperusha bendera ya CCM kwa nafasi ya urais, akiwabwaga wagombea wateuliwa wenzake.

Neema aliyoipata Dk. Magufuli, ndiyo naizungumzia kama ‘nafasi’ au ‘eneo’ kwa jinsi nilivyofafanua.

Ukilijua hilo, nakusihi ulijue na hili. Ni wachache sana mpaka hivi leo wanaoendelea kuamini wanapoiona amani ikiwa imetawala hapa nchini kiasi cha kutosha, wasijue imefikaje hapo ilipo na hata kudumu.

Wakati ilitazamiwa na ilishabashiriwa kuwepo na vita na machafuko mara baada tu ya uchaguzi mkuu kumalizika na kumpata rais.

Kwa wasioelewa au kama wanaelewa ila hawataki kuamini, amani hii imeletwa na kitu kinachoitwa ‘nafsi’. Ile iliyotangulia kuwako kabla ya kuja ‘nafasi’ iliyokuja baadaye.

Pamoja na kwamba nilisema kuwa, ‘nafasi’ na ‘nafsi’ havifanani, vinatofautiana na wala haviko sawa. Ila lazima vitu hivi viwili vishirikiane.

Kama ‘nafasi’ haiitaki ‘nafsi’ ni vigumu hali ya amani kupatikana na kuwepo eneo husika, muhimu ni kushirikiana na kuelewana kwa ukaribu kutokana na ule umuhimu wa utendaji wa kila kimojawapo.

Ili kuwepo au kuleta machafuko hapa nchini. Ni mpaka pale ‘nafsi’ itakapoanza kuona hakuna haja ya kuwapo na ‘nafasi’.

Au ‘nafasi’ itakapoona hakuna tena haja ya kushirikiana kwa lolote na ‘nafsi’, katika kuleta maendeleo na ufanisi wa pamoja. Likitokea hili ni hakika vita itatokea na machafuko kuibuka, jambo ambalo mpaka sasa naamini kuwa limeshikwa na ‘nafsi’ ambayo ingali inaheshimu uwepo wa ‘nafasi’.

Kwa tafsiri na maana hiyohiyo, nikimzungumzia Rais Magufuli, nasema kuwa ni mtu ambaye amepata nafasi ya urais kwa neema, nafasi ambayo haikuwa ya kwake.

Neema ilianza pale ambapo, yeye binafsi hakuwa na wazo la kuchukua fomu ya kutaka kugombea nafasi nyeti kama hiyo.

Nafasi ile, wapo waliotengewa na waliokusudiwa. Kwa ajabu ya wengi, majina yale ambayo kwa mujibu wa aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mngeja; yalikuja yakiwa mfukoni mwa kiongozi mmojawapo aliyetaka watu wake wapewe nafasi.

Jambo ambalo wajumbe wengi walipingana nalo na lilileta mzozo mkubwa na hatimaye majina yale kukosa nafasi. Ndipo kwa nasibu, nafasi ikampata na kumwangukia rais wa sasa.

Kwa maelezo hayo, baraka za kiuongozi ni lazima na kwa vyovyote, zitaandamana au zitakuwa na ‘nafsi’.

Na ‘nafasi’ itabaki kuwa na neema tu na kwa kuendeleza utulivu na amani ni mpaka pale ambapo ‘nafasi’ itaona kuwa ni vyema kutenda au kushirikiana na ‘nafsi’ ili mambo yaweze kwenda na kusonga; nje ya hapo ni mambo kwenda kinyume na matarajio.

Ieleweke kuwa amani iliyopo na inayoendelea kuwepo hapa nchini, licha ya kwamba Mungu ndiye mleta amani na hali ya utulivu, lakini mara zote haji yeye ili watu tumshuhudie.

Daima hutumia watu tuliona nao na tunaoishi nao siku zote, na sasa amemtumia Lowassa kuleta amani kwa ile hali ya kukataa namna yoyote ya maandamano.

Kwa wale ambao pengine hawakukubaliana na uchaguzi ulivyokuwa na figis-figisu zozote zilizojitokeza wakati wote wa zoezi lile, pamoja na kwamba inadhaniwa serikali iliagiza magari mengi ya kivita, yakiwemo mengi ya kubeba maji ya washawasha.

Yote hayo hayana nafasi kwa wakati huu, maana hali ni shwari.

MwanaHalisi

Katibu mpya Chadema alikuwa 'kichwa' Ukawa.

Licha ya Katibu Mkuu mpya wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji, kutokuwa na jina kubwa katika ulingo wa siasa na wengi kumwona mgeni, ndiye aliyekuwa 'kichwa' (think tank) wa Ukawa, imefahamika.

Juzi, Chadema ilimteua Dk. Mashinji kuwa Katibu Mkuu mpya kushika nafasi ya Dk. Willibrod Slaa, aliyejiuzulu nafasi hiyo Julai 30, mwaka jana, kwa kile akichokieleza kuwa ni utaratibu kutofuatwa wa kumkaribisha Edward Lowassa, aliyehamia katika chama hicho kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hata hivyo, uteuzi wake umepokelewa kwa mtazamo tofauti kutokana na kutokuwa na jina kubwa katika ulingo wa siasa, lakini imefahamika kuwa ni mmoja wa watu waliofanikisha mipango mikakati ya Ukawa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kupata mafanikio makubwa, baada ya kuwa na wabunge 113 bungeni ikiwa ni wale wakuchaguliwa na viti maalumu.

Idadi hiyo ni kubwa zaidi kupatikana tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa kwanza unaojumuisha vyama vingi mwaka 1995.

Katika mafanikio hayo, Dk. Mashinji alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Sera na Wanataaluma wa Ukawa na ndio walioandaa Ilani ya Chadema katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Akielezea uwezo wake na anavyomfahamu, Mwenyekiti wa Kamati ya Sera na Wanataaluma wa Ukawa, Dk. Rodrick Kabangira, ambaye amefanya kazi kwa karibu na Dk. Mashinji, alisema ni mtendaji mwenye malengo ya kimkakati na kufuatilia kwa karibu anayoyatenda.

"Nilifahamiana naye mwaka 2011 tulipokuwa tunaandika majarida mbalimbali ambayo tuliyawasilisha Chadema kama la namna ya kuboresha sekta ya afya na baadaye kuandika ilani, lakini katika Kamati ya Ufundi ya Ukawa, tumefanya kazi pamoja. Namfahamu vizuri ni mtu sahihi kwa Chadema katika kuelekea mwaka 2020," alisema.

Alisema wakati wa kampeni za uchaguzi, alikuwa mzungumzaji wa namna Sera na Ilani ya Chadema inavyoweza kutekelezwa kwa kuwa anaijua kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho na kwamba kwa mwonekano ni mpole na anayezungumza taratibu, lakini anatoa neno zito.

AMWAGA SERA FURAHISHA
Akihutubia mamia ya wananchi wa Mwanza katika viwanja vya Furahisha jana, Dk. Mashinji alisema ataongoza kimkakati zaidi kwa kuwa na mabadiliko ya kimfumo ndani na nje ya chama kwa kujenga matawi ya chama katika kila eneo.

"Naagiza kila kata kuwe na kamati za ufuatiliaji palipo na diwani na ambako hakuna ili kuhakikisha masuala ya wananchi yanafuatiliwa kwa karibu katika sekta mbalimbali kama elimu, maji na mengine. Madiwani wafanye kazi, hatukuwapeleka kuuza sura bali kusimamia kwa karibu maslahi ya wananchi," alisema

Aidha, aliagiza wabunge wote wa Ukawa kugeuza suala la Katiba Mpya ni agenda ya kudumu kwa kila dakika wanazopata ndani ya Bunge na kwamba kikosi cha kimkakati ndani ya chama kitaimarishwa katika utekelezaji wa shughuli zinazolenga kutetea maslahi ya wananchi.

Dk. Mashinji alisema ni lazima maeneo yanayoongozwa na Ukawa, ustawi wa wananchi uonekane na kwamba mambo yatakayosimamiwa ni mabadiliko ya wananchi ili washike hatamu ya chama na viongozi washirikiane nao.

Lingine ni kujiandaa kwenda kwa kasi kwani kwenda pole pole jua litazama na giza kuingia na kushindwa kusonga mbele kufikia malengo ya kuchukua dola m,waka 2020.

ATAJA VIPAUMBELE VYAKE
Dk. Mashinji ameweka wazi vipaumbele vitano ambavyo ataanza navyo baada ya kuingia ofisini katika kuhakikisha Chadema inafanikiwa kushika dola katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, ikiwamo kukipeleka chama hadi kwa wananchi wa kawaida.

Akizungumza jana na Nipashe, aliwashukuru wajumbe wa Baraza Kuu waliompigia kura za ndiyo kwa asilimia 100 huku alitaja vipaumbele hivyo kuwa ni utekelezaji wa ilani ya Chadema katika halmashauri wanazoongoza, kupinga rushwa na makundi yanayotaka kumea, Katiba Mpya na kusimamia mabadiliko ndani na nje ya chama.

Alisema wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu kaulimbiu kubwa ya chama hicho ilikuwa mabadiliko ambayo hayajahitimishwa kwa kushindwa uchaguzi bali yametajwa katika ilani na yatatekelezwa kwa vitendo.

"Baraza Kuu na wengine bado tuna jukumu la kuwasimamia na kuwatetea Watanzania. Tusiogope licha ya watu kunakili mambo yetu na kutaka kuyatekeleza, hawawezi kutufikia sisi ambao ndio tunajua utekelezaji wake, twendeni katika kiini cha tatizo," alisema.

Dk. Mashinji ambaye aliambiwa uteuzi wake na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, wakiwa hotelini, alitaja kingine ni kukisogeza chama kwa wananchi zaidi kwani kufanya operesheni mbalimbali na mikakati ya kichama kwa kuwa mtaji mkubwa wa chama ni watu.

"Msingi wa chama uko chini, mtaji wa chama ni watu na siyo vipeperushi, magari. Hezekiah Wenje akishinda kesi si yeye ni Wananyamagana wameshinda, hivyo ni lazima tuwafikie wannachi huko waliko ili 2020 tuweze kushinda uchaguzi,"alisisitiza.

Alisema kazi iliyoko mbele yake si nyepesi, lakini watafikaje Ikulu itajulikana baada ya kufika mtoni, na kuwataka wanachama na viongozi kutoogopa polisi na vyombo vingine vya dola vinavyotumika kuwanyanyasa.

Kipaumbele kingine ni kusimamia mabadiliko ya Katiba Mpya ambayo yalianza kwa kuhakikisha mifumo iliyopo inabadilika kwa kuwa imekuwa chanzo kikubwa cha kuwanyima haki za msingi na ukuaji wa uchumi wa Watanzania.

"Hatuwezi kupiga hatua kubwa kimaendeleo kwa katiba tuliyonayo au iliyopendekezwa na Bunge Maalumu. Tuna matatizo nyeti ya kitaifa ambayo chanzo chake kikubwa ni mfumo. Ukiangalia suala la rushwa utabaini shida ni mfumo uliopo na ambao tunahitaji kuubadili kwa kutumia Katiba Mpya, hivyo nikiiingia ofisini litakuwa kipaumbele," alisema.

Aliongeza kuwa: "Lengo letu ni nguvu ya umma, tuiwezeshe kutambua haki zao mfano mgogoro mkubwa baina ya wenyeviti na mameya wa halmashauri ni wakuu wa wilaya na mkoa kuingilia utendaji wa halmashauri kwa kuwa kuna mifumo ya kikoloni kwa Katiba Mpya tutaiondoa."

Dk. Mashinji alisema lingine ni kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chadema 2015, ambayo alishiriki kuiandaa tangu mwanzo na anajua inavyoweza kutekelezwa kivitendo katika halmashauri zinazoongozwa na Chadema katika kuleta maendeleo endelevu ya wananchi.
Katibu huyo ambaye ni Daktari wa Binadamu, alisema pia ni lazima kuwa pamoja katika ujenzi wa chama na kushika hatamu, huku akitumia mfano wa maji ambayo huenda pamoja na yanapofika kwenye maporomoko hushuka pamoja.

Jambo lingine ni kupinga rushwa na makundi ambayo yameanza kumea ndani ya chama, ili kuendelea kukitofautisha chama hicho na kingine na kudhihirishia umma kuwa wamejipanga kushuka dola ifikapo 2020.

WABUNGE CHADEMA WAMZUNGUMZIA
Mbunge wa Moshi Mjini, Jaffary Michael, alisema chama kimepata mtu sahihi kwa wakati sahihi kwa kuwa moja kwa moja inakwenda kuvunja propaganda zilizopandikizwa kuwa ni chama cha Kaskazini.

Alisema ataleta mawazo mapya ndani ya chama kuliko kuendelea na watu wale wale wenye mawazo yale yale na akipewa ushirikiano ataweza kuvaa viatu vya Dk. Slaa, kwa kusimamia maono yake ambayo alitumia muda wake mwingi katika ujenzi wa chama imara.
Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro, alisema uwezo wa mwenyekiti wa taifa kuficha siri ni ushahidi tosha kuwa chama kinasiri na intelejensia ya hali ya juu na kina sifa za kushika dola kwa mwaka 2020.

Alisema Dk. Mashinji si mgeni katika utendaji serikalini na harakati mbalimbali ikiwamo kutetea maslahi ya madaktari na sekta ya afya ambayo inakabiliwa na matatizo mengi hadi sasa, hivyo kwa kumtumia wataweza kunyonya ujuzi na kuupeleka katika halmashauri zinazoongzwa na Chadema.

Naye Mwalimu alisema siku zote duniani hakuna mbadala wa mtu kwa kuwa kila mmoja ana uwezo, uimara na udhaifu wake, kinachotakiwa ni kutekeleza majukumu kwa viwango vinavyotakiwa.

"Nimeshika nafasi ya kaimu katibu, haikuwa kazi rahisi kwa kuwa nafadi hii ni nyeti sana, kila mtu anakuangalia wewe, lakini naamini bosi mpya tuliyempata ni mtu imara, anaijua Chadema siyo kwa kuisoma, bali kushiriki ikiwamo kuandika ilani na machapisho mbalimbali," alibainisha.

Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Kiwelu, alisema kwa kiongozi huyo anaiona Chadema mpya kwa kuwa ni mtu mwenye uwezo na anafahamu anachokitenda.

Awali, akizungumza wakati wa kumuombea kura kwa Baraza Kuu, Mbowe, alisema ameona Dk. Mashinji anastahili kuendeleza guruduma la chama hicho kwa kuwa ni mtu makini, mwenye maono na anayejua atendalo.

Mjumbe wa Kamati Kuu, Lowassa, alisema Mbowe amedhihirishia umma kuwa uamuzi wake ulikuwa makini sana kwa kuwa ameleta mtu kijana na shupavu hasa katika nyakati za mabadiliko.

"Tumekupa imani kubwa, chama kinachofuata kuongoza nchi ni Chadema, lengo letu ni kukamata dola na rafiki yetu wa kweli ni kutuwezesha kufika Ikulu 2020," alisema.

WADAU WAPONGEZA
Uteuzi wa Dk. Mashinji kuwa Katibu Mkuu wa Chadema umepokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wanasiasa na wasomi nchini.
Baadhi ya makundi hayo, wameeleza kuwa Chadema imemteua mtu ambaye alikuwa hafahamiki kwa wananchi, hivyo imekuwa ‘surprise’ kwa wanachama wao, kwa kuwa walikuwa wanatarajia kusikia jina kubwa.

Mtaalamu na mchambuzi wa masuala ya siasa, Abdulhakim Atiki, alisema pamoja na kuwa Mashinji hafahamiki kwa wananchi, lakini alikuwa ni mmojawapo wa wanachama walioshiriki katika kutengeneza Ilani ya Ukawa wakati wa uchaguzi mkuu.

Alisema ni kijana mwenye uwezo wa kuongoza Chadema kama makatibu wakuu wengine waliotangulia.

Alisema tangu kuondoka kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Aman Kabourou, aliyetokea Kanda ya Ziwa, hakukuwa na katibu mkuu mwingine aliyetokea upande huo, hadi alipoteuliwa Mashinji.

“Nadhani Chadema wamezingatia ukanda zaidi, tena ukizingatia wakati wa uchaguzi mkuu maeneo ya Kanda ya Ziwa hawakufanya vizuri, hivyo wamemteua Mashinji ili kujiimarisha zaidi,” alisema.

Naye mwanazuoni kutoka Chuo cha Diplomasia, Israel Sosthenes, alisema hamfahamu Dk. Mashinji vizuri, lakini Chadema hadi kumteua kushika nafasi hiyo ya juu watakuwa wako sahihi na uhakikia na mtu huyo.

Alisema katibu mkuu ndiye mtendaji mkuu katika usimamizi wa chama, na kwamba ni mapema kumzungumzia kama ataweza au la.
Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Anna Mghwira, alisema hakuwa anamfahamu Dk. Mashinji, na kwamba amemfahamu mara baada ya kuteuliwa.

Alisema Chadema ni chama kikubwa nchini, hivyo hakiwezi kumtemteua mtu kushika nafasi hiyo kubwa ndani ya chama kama uwezo wake ni mdogo.

Naye Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Siasa ya Sayansi, Dk. Bashiru Ally, alisema hamfahamu Dk. Mashinji utendaji wake kiundani, kwa kuwa ni mara ya kwanza kumsikia.

Alisema anawafahamu viongozi wakuu wote wa Chadema, alisema Dk. Mashinji hakuwahi kumwona kumwona wala kumsikia akishiriki katika masuala ya chama, alisema kama aliwahi kushiriki itakuwa ngazi za chini.

Alisema uteuzi wake unaweza kuwa na faida ndani ya Chadema, kwa kuwa ni mtu ambaye hana mambo mengi kama walivyo viongozi wengine wakubwa ndani ya chama hicho.

Aliongeza kuwa, Dk. Mashinji ni jina jipya pia, ni kijana ambaye anaweza kumudu kazi ya ukatibu mkuu wa chama.


Nipashe

Sunday, March 13, 2016

Dk. Vicent Mashinji ndiye Katibu Mkuu Chadema

DAKTARI Vicent Mashinji ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu mpya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kupitishwa na Baraza Kuu la Chadema, katika kikao chake kilichokaa jijini Mwanza, anaandika Mwandishi Wetu.

Katika Kikao hicho cha Baraza Kuu, Freeman Mbowe alitangaza jina la Dk. Mashinji na kuungwa mkono na wajumbe wa baraza hilo, hivyo anajaza nafasi iliyoachwa na Dk. Willibrod Slaa, aliyejienguwa ukatibu mkuu wa chama hicho.

Jina la Dk. Machinji halikuwa miongoni mwa wanachama wa Chadema ambao walikuwa wanatarajiwa kumrithi Dk. Slaa kwani waliokuwa wanatabiriwa kukatia kiti hicho ni Salum Ally Mwalimu, Frederick Sumaye, Benson Kigaila, John Mnyika, Dk. Marcus Albanie na Prof. Mwesiga Baregu.

Nafasi ya Katibu wa Chadema ilikuwa wazi tangu Dk. Slaa alipoondoka Chadema muda mfupi baada ya chama hicho kumpitisha Edward Lowassa aliyetokea CCM kuwa mgombea urais wa chama hicho na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Wasifu wa Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Vincent B. Mashinji

Professional experience

Clinical Advisor & TB/HIV lead

UMSOM-IHV

July 2008 – Present

ART Program Doctor/IMA team lead

IMA Worldhealth

August 2006 – June 2008 (1 year 10 months)

Medical Officer/Anaesthesiology

Regency Medical Centre

October 2005 – August 2006 (10 months)

Medical Officer

Muhimbili National Hospital

August 2003 – October 2005 (2 years 2 months)

Research Assistant

Freelance

November 2002 – August 2003 (9 months)

Intern Docor

Muhimbili National Hospital

September 2001 – October 2002 (1 year 1 month)

Education history

Open University of Tanzania

PhD

August 2010 – Present

AMREF/UCLA Anderson School

MDI Certificate

April 2010 – April 2010

Blekinge Institute of Technology

MBA

September 2007 – March 2010 (2 years 6 months)

UMSOM-IHV

IPEP Certificate

May 2008 – May 2008

Evin School of Management

Certificate in CSR

October 2005 – October 2005

Muhimbili University College of Health Sciences

MMed/Anaesthesiology

September 2003 – April 2005 (1 year 7 months)

Muhimbili University College of Health Sciences

Certificate in Research Methodology

September 2004 – September 2004

Makerere University

MBChB

October 1995 – July 2001 (5 years 9 months)

Mzumbe High School

ACSEE

July 1992 – June 1994 (1 year 11 months)

St. Pius X Seminary, Makoko

GCSEE

January 1988 – October 1991 (3 years 9 months)

Iligamba Primary School

Leaving Certificate/Primary School

January 1981 – October 1987 (6 years 9 months)


MwanaHalisiOnline

DR VICENT MASHINJI NDIYE KATIBU MKUU MPYA CHADEMA

Katibu Mkuu wa CHADEMA Dkt. Vicent Mashinji akiwa anatoa shukrani baada ya uteuzi.

Saturday, March 12, 2016

Mbowe atoboa siri ya Lowassa

FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema-Taifa amesema, Edward Lowassa, aliyekuwa mgombea wa chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kuungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hakutoa hata senti moja alipojiunga na chama hicho, anaandika Happyness Lidwino.


Mbowe amezungumza hayo kwenye Mkutano wa Baraza Kuu la Chadema linaloendelea kwa sasa Jijini Mwanza.

Amesema kuwa, pamoja na kuwepo kwa kauli nyingi kwamba, Lowassa alimmwaga pesa kabla ya kujiunga na chama hicho, ukweli unabaki kuwa hakutoa pesa yoyote kama ilivyokuwa ikidaiwa.

“Watoto wangu walikuwa wanakula sana maharage, sasa siku moja wakala nyama, jirani akasema umeona Lowassa kaja Chadema,” am esema Mbowe.

Akizungumzia migogoro ya kichama iliyokuwa imejitokeza kwenye uchaguzi uliopita Oktoba 25 mwaka huu Mbowe amesema, kuna kila sababu kushughulikia migogoro hiyo kwa haraka.

“Migogoro mingi ndani ya Chadema imepelekea kuanguka kwa chama, hivyo itashugulikiwa kwa haraka,” amesema na kuongeza;

“Uchaguzi mkuu wa chama ni Oktoba 2018.”

Amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba, harakati za kisiasa hasa kukikuza chama ni gharama kubwa jambo ambalo chama kinajitahidi linakabiliana nalo.

Amesema kwamba, pamoja na mambo yote ndani ya chama hicho lakini suala la rushwa haliwezi kuvumiliwa hata mara moja.

Akifafanua kauli hiyo amesema kwamba, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeishi kwa kulea rushwa na kwamba, hali hiyo ndio imekifikisha hapo kilipo sasa.

Amesema, hali hiyo inaelekea kuingia Chadema jambo ambalo linaweza kusababisha kupasuka kwa chama hicho endapo halitashuhulikiwa.

“Jambo ambalo hatutalivumia ndani ya Chadema ni swala la rushwa kwani rushwa linagawa taifa, sasa swala la rushwa lililelewa na CCM na sasa inataka kuingia Chadema,” amesema.

“Kuna majimbo kama Iringa, Rukwa, Arusha Chadema waliachiwa kwa asilimia mia moja na Ukawa lakini kwanini wameshindwa kuchukua ushindi wa kutosha katika majimbo hayo?” amehoji.

Akizungumzia changamoto za Ukawa Mbowe amekiri kuwepo na kwamba, hakuna sababu ya kuzikwepa.

“Changamoto zilizopo ndani ya Ukawa hakuna haja ya kuzikimbia bali ni kupambana nazo,” amesema.

Akizungumzia umoja wa kimataifa amesema kwamba, Chadema hakikubaliani na mtu yoyote anayetaka ama kushabikia kauli za kuligawa taifa.

“Nawashauri tunapokuwa popote lazima tukatae nchi yetu kugawa vipande vipande. Hatukotayari kufanya kosa kama hilo wala kushabikia kuligawa taifa ,” amesema.

MwanaHalisiOnline

Thursday, March 10, 2016

Waitara: Ukawa hatutalala umeya Dar hadi kieleweke.

Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara, amesema Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wanaendelea kupambana dhidi ya mbinu chafu zinazotumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kumpata Meya wa Jiji la Dar es Salaam.

Alizitaja mbinu hizo kuwa ni kuahirisha uchaguzi huo mara tatu bila sababu za msingi ikiwamo kisingizio cha zuio la Mahakama kwa ajili ya uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari 26 ambalo limebainika kuwa halikuwa halali.

Waitara aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kivule mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kuwashukuru wananchi hao kwa kumchangua kwa kura nyingi, hivyo kuwa miongoni mwa wabunge 10 nchini waliopata kura nyingi.

Alisema iwapo juhudi zao za kumpata meya wa Jiji la Dar es Salaam zitafanikiwa, kazi ya kwanza itakuwa ni kuhakikisha wanafuta sheria ya kuwazuia bodaboda wasiingie mjini na kutumbua jipu la mradi wa mabasi yaendayo haraka (Darts) kusuasua.

“Hatuwezi kuachia nafasi hiyo kwani CCM wakiipata utekelezaji wa majukumu ya kuleta maendeleo kwa jamii kupitia Ukawa utakuwa mgumu, hivyo lazima tuvuke vikwazo vyote,” alisema.

Alisema nafasi ya meya wa Jiji ni muhimu kwa kuwa ndiyo nafasi pekee inayoratibu itifaki za viongozi wa nchi, hivyo CCM hawapendi mpinzani apewe jukumu hilo na ndiyo sababu wanatafuta kila sababu kupunguza kasi ya Ukawa.

Aliongeza kuwa itakuwa ndoto kwa CCM kushinda kwa kura kwenye uchaguzi wa meya wa Jiji kwa kuwa ina wajumbe 76 wakati Ukawa ina wajumbe 87, hivyo ipo tofauti ya wajumbe 11.

Aidha, Waitara ambaye pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kivule, alisema wananchi wakiona Mbunge wa upinzania anapigiwa makofi na chama tawala wafahamu ni msaliti na anapaswa kufukuzwa.

“Nyote mtakuwa mashahidi, nilivyokamatwa na polisi kisha kuwekwa lupango kwenye sakafu aliyolala Masamaki, lakini nilipofika mahakamani nilijidhamini mwenyewe, kiukweli sijampiga RAC (Katibu Tawala wa Mkoa),” alisema.

Mmoja wa wakazi hao, Juma Hamis, alisema wanashukuru kupata taarifa kutoka kwa mbunge wao, lakini wao wanahitaji maendeleo ya kuboreshewa miundombinu ya barabara, maji na umeme.

“Tumechoka na ahadi za wanasiasa, tunahitaji vitendo kuliko maneno,” alisema.

CHANZO: NIPASHE

Sunday, March 6, 2016

MAAZIMIO YA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CHAMA ILIYOKUTANA MACHI 1, 2006, JIJINI DAR ES SALAAM

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO



TAARIFA KWA UMMA KUHUSU
MAAZIMIO YA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CHAMA ILIYOKUTANA MACHI 1, 2006, JIJINI DAR ES SALAAM


Kamati Kuu ya Chama imesema kuwa tangu utawala wa awamu ya tano chini ya Serikali ya CCM ikiongozwa na Rais John Magufuli uingie madarakani, misingi ya uongozi bora na demokrasia ya vyama vingi imeyumba, kiasi cha kuiingiza nchi katika sintofahamu kubwa ya kisiasa, kiuchumi na kiutawala na kutishia mstakabali wa nchi.

Akitoa maazimio ya kikao cha Kamati Kuu, mbele ya waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe ametaja masuala kadhaa ambayo yameanza kuharibu sifa Tanzania kwa kuvunja misingi ya demokrasia kuwa ni pamoja na ‘uhuni’ wa kisiasa unaofanywa na Serikali, vyombo vya dola kwa kushirikiana na CCM kupora haki ya wananchi katika uchaguzi wa mameya na wenyeviti wa halmashauri hasa maeneo ambako vyama vinavyounda UKAWA vimeshinda.

Katika muktadha huo, Mwenyekiti Mbowe amesema kuwa Kamati Kuu katika kikao chake hicho kilichoketi Machi 1, mwaka huu, imazimia kwa kauli moja kuwa Chadema haitaendelea tena ‘kuomba’ haki ya kufanyika uchaguzi na hatimaye kuongoza Jiji la Dar es Salaam kupitia Meya na Naibu wake, wanaotokana na UKAWA, bali itaidai haki hiyo, ambayo imepatikana kutokana na mapenzi ya wananchi wa jiji hilo kwa vyama vinavyounda UKAWA.

Mwenyekiti Mbowe amewaambia waandishi wa habari kuwa Kamati Kuu katika kikao hicho cha siku moja, ilijadili na kutafakari kwa kina, pamoja na masuala mengine, mambo yafuatayo:

1. Hali ya kisiasa nchini.

2. Kutathmini uhai na nguvu ya chama.

Kwa kuanzia, Mwenyekiti Mbowe amesema kuwa kwa Mamlaka ya Kikatiba, ibara ya 6.1.3 inayopewa nguvu na ibara ya 7.5.1, Chama kimeamua kuimarisha uongozi wa kichama mkoani Dar es Salaam, kwa kuanzisha Kamati Maalum itakayosimamia eneo linalojulikana Dar es Salaam Kuu (Greater Dar es Salaam) ambayo pamoja na mambo mengine, wajibu wa awali itahusika katika kuratibu upatikanaji wa haraka wa kikatiba, kisheria na kikanuni wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti Mbowe, Kamati hiyo Maalum itakayokuwa chini ya Uenyekiti wa Mwita Waitara (Mb), Makamu Mwenyekiti Bernard Mwakyembe (Diwani) na Katibu Henry Kilewo ikiwa na wajumbe 25, pia itahusika katika mambo mengine yanayohusu uimarishaji wa chama na usimamizi wa shughuli zote zinazohusu utendaji wa wawakilishi wa chama katika vyombo vya serikali hususan katika eneo la Dar es Salaam Kuu.

Suala jingine lililodhihirisha kuyumba kwa misingi ya uongozi bora na demokrasia ya vyama vingi ni uchaguzi wa Zanzibar ambao Mwenyekiti Mbowe amesema kuwa washindi halali wa nafasi ya Rais na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamenyimwa haki yao hali ambayo hadi sasa imesababisha sintofahamu kubwa ya kisiasa, kiuchumi na kiutawala Zanzibar, akisisitiza kuwa msimamo wa Chama cha CUF ndiyo msimamo wa CHADEMA kuhusu hali tete inayoendelea visiwani humo.

Aidha, Mwenyekiti Mbowe ameongeza masuala mengine ambayo yameiharibia sifa nchi katika kusimamia misingi ya demokrasia na uongozi bora, kuwa ni pamoja na namna Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na vyombo vya dola vilivyosimamia Uchaguzi Mkuu na kutumika kupora haki ya wananchi ya kuchagua na kupata viongozi wanaowataka.

Suala jingine ni juhudi za makusudi zinavyofanywa na watawala wa awamu ya tano kudhibiti mhimili wa Bunge usitekeleze wajibu wake wa kikatiba wa kuisimamia serikali, akitolea mifano kadhaa ikiwemo kuzuia TBC kurusha vikao vya bunge moja kwa moja, Serikali ya CCM kuingilia uundwaji wa uongozi wa Kamati za Bunge zinazosimamia fedha za umma (PAC na LAAC).

“Pia serikali hii hii ya CCM imeingilia mhimili wa bunge na kudhibiti uundwaji wa Kamati mbalimbali za bunge kwa kutumia visivyo au nje ya taaluma, uzoefu na uwezo wao wabunge wa kutoka vyama vyote ambao walionesha ujasiri wa kuikosoa Serikali katika mabunge yaliyopita…jambo ambalo kwa upande wa Kamati za PAC na LAAC tumekataa CCM watuamulie kinyume na sheria na kanuni za bunge.

“Jeshi la Polisi kwa maelekezo ya Serikali limeendelea kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya upinzani, ilihali CCM, viongozi wao, wanachama na wafuasi wao wakifanya maandamano na mikutano maeneo mbalimbali ya nchi bila kuzuia na polisi. Yote haya yanafanyika, Magufuli anajua, Majaliwa anajua.
“Viongozi wetu, wanachama, wafuasi na hata mashabiki wa vyama vya upinzani wanafunguliwa mashtaka yasiyokuwa na msingi pale wanapodai haki za kikatiba za kutekeleza wajibu wao wa kisiasa katika mazingira huru yenye uhakika. Wameamua hata kudhibiti kwa kuvitisha na hata kuvifuta vyombo vya habari ambavyo vinatimiza wajibu kikamilifu kwa jamii na havifungamani na CCM moja kwa moja. Yote haya yanafanyika Magufuli anajua, Majaliwa anajua,” amesema Mwenyekiti Mbowe na kuongeza;

“Ni vyema kuelewa kuwa hatua ya misingi ya utawala bora na demokrasia ya vyama vingi ambayo kama nchi tulikuwa tumeifikia kiasi cha Tanzania kujipambanua miongoni mwa nchi za Afrika hasa Kusini mwa Sahara yalikuwa ni matokeo ya mapambano ya zaidi ya miaka 20 kupigania demokrasia katika taifa hili. Leo watu wanataka nchi iongozwe kwa kauli za mtu au watu badala ya misingi ya katiba, sheria na taratibu ambazo nchi imejiwekea.”

Mwenyekiti Mbowe amehitimisha kwa kusema, Kamati Kuu imeazimia kwamba namna ya kukabiliana na hila, njama, mipango ovu ya CCM dhidi ya wapinzani, hali ya kisiasa nchini kwa kina pamoja na Mkakati wa Chama wa Miaka 5 ijayo, itajadiliwa na kufanyiwa maamuzi katika kikao cha Baraza Kuu kitakachofanyika jijini Mwanza, Machi 12 mwaka huu ambalo pia litaweka dira na mwelekezo wa chama kuelekea mwaka 2020.

Imetolewa leo Machi 5, 2016 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

Chadema waja na mkakati mpya wa umeya Dar

Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), iliyojifungia kwa siku moja, imeazimia iundwe ngazi ya uongozi ya chama itakayojulikana kama ‘Dar es Salaam Kuu’ ili kuijenga, kuitetea na kuilinda demokrasia inayodaiwa kuelekea kuporwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema chombo hicho kimeundwa kwa mujibu wa katiba ya chama chao (Chadema).

Alisema chombo hicho ambacho kitakuwa na wajumbe 25 wakiwamo wabunge wa kuchaguliwa na wa viti maalumu, mameya, madiwani na wenyeviti; kitakuwa na kazi ya kuongeza nguvu ya usimamizi, udhibiti na uratibu wa chama.

Alisema mwenyekiti wa chombo hicho atakuwa Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara; makamu atakuwa Diwani wa Temeke, Bernard Mwakyembe; Katibu, Henry Kileo; na mweka hazina atakuwa Susan Lyimo.

Alisema katika mchakato wa uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, kumejengeka utamaduni wa kushtukizana bila ya kuwa na ushauriano juu ya lini uchaguzi huo unafanyika.

Madiwani wengi katika Jiji la Dar es Salaam wanatoka Chadema na Chama cha Wananchi (CUF), ambavyo hushirikiana kupitia muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

"Tumeona (CCM) hawana nia njema. Kwa hiyo hatutashiriki uchaguzi wa kushtukizana. Kanuni ipo wazi… inasema notisi ni siku saba ili nasi tujiandae," alisema.

Uchaguzi wa kumpata Meya wa Jiji la Dar es Salaam umekuwa ukiahirishwa mara kwa mara kutokana na sababu kadhaa, ikiwamo kile kinachoelezwa na madiwani wa Ukawa kuwa ni mizengwe inayosababishwa na CCM inaoenekana kutokuwa tayari jiji hilo kuwa chini ya upinzani.

Katika hatua nyingine, Mbowe ambaye pia ni Mkuu wa Kambi Ramsi ya Upinzani Bungeni, alisema katika miezi mine ya utawala wake, Serikali ya Rais John Magufuli imeyumba kwa kiasi kikubwa katika kusimamia misingi ya utawala bora.

Alitolea mfano kuhusu hali ya kisiasa visiwani Zanzibar, akisema washindi halali waliochaguliwa na wananchi kupitia sanduku la kura hawajapewa haki yao ya kuongoza.

“Waliochaguliwa kihalali Zanzibar hawajapewa fursa kama wananchi walivyoamua na vile vyama vinavyoshiriki uchaguzi wa marudio (utakaofanyika Machi 20) ni wakala wa CCM,” alisema.

Aidha, alisema wameshangazwa na kitendo cha kuzuiwa sehemu kubwa ya urushwaji wa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge kupitia Televisheni ya Taifa (TBC), ambayo ni mali ya umma.

Mbowe alisema serikali imeingilia uundwaji wa uongozi wa kamati za kusimamia fedha za umma bungeni ambazo kwa kawaida hutakiwa kuongozwa na kambi ya upinzani.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Ukawa walipa jiji siku 7

Wabunge na madiwani kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wameandamana hadi ofisi za Jiji wakitaka waambiwe tarehe ya uchaguzi wa umeya wa Dar es Salaam ndani ya siku saba.

Wakiwa kwenye ofisi hizo jana, wawakilishi hao wa wananchi walisema waliamua kwenda kwa njia ya kistaarabu, lakini wasipoambiwa tarehe ya uchaguzi huo watakwenda kwa njia ambayo wanaijua wao.

Akizungumza kwa niaba ya madiwani hao, Mbunge wa Jimbo la Ukonga (Chadema), Waitara Mwita, alisema maandamano yao yalikuwa ya amani kutaka kukutana na Mkurugenzi wa Jiji ili kujua hatma ya uchaguzi huo.

Alisema Jiji linatakiwa kutangangaza tarehe ya uchaguzi huo ndani ya siku saba na endapo hawatafanya hivyo wanachama wa Ukawa watajua cha kufanya.

“Bajeti ya Jiji la Dar es Salaam imepitishwa bila kushirikishwa madiwani wa Ukawa," alisema Waitara ambaye mapema wiki hii alifikishwa mahakamani pamoja na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee wakituhumiwa kumpiga msimamizi wa uchaguzi huo, kikao kilipoahirishwa mwishoni mwa wiki iliyopita.

"Meya wetu tukimpitisha lazima tutaiondoa hiyo bajeti iliyopitishwa bila kuwashirikisha madiwani wetu.”

Aidha, Mwita alisema sheria inatamka kuwa Meya anapaswa kuwa amepatikana ndani ya siku 90 tangu tarehe ya uchaguzi, lakini CCM kwa maslahi wanayoyajua wao wamekuwa wakiupiga danadana uchaguzi huo.
Mdee alisema hakukuwa na sababu za msingi zilizosababisha uchaguzi huo usifanyike Jumamosi iliyopita.

Mdee alisema kuchelewa kwa uchaguzi huo kumekuwa na madhara makubwa kwa wanancho kwani miradi mingi imesimama.

“Tunamtaka Mkurugenzi atueleze ni lini anatarajia kuitisha uchaguzi... sisi tunataka uchaguzi uitishwe ndani ya siku saba na taratibu zote za matakwa ya kisheria zimeshakiukwa na watu wasioitakia mema nchi hii,” alisema Mdee.

“Kwa sasa tumeambiwa Mkurugenzi hayupo, tumeelezwa ana vikao na sisi tunamsubiri aje alimalize hili suala la umeya wa Jiji.

"Kipindi hiki cha kuelekea bajeti halmashauri zote zinatakiwa kuwa na bajeti na bajeti ya jiji itatengenezwa na nani na kwa maslahi ya nani wakati sisi hatupo?”

Mdee alisema kuna uchafu mkubwa ndai ya Jiji ikiwemo uuzwaji wa Shirika la Uda.

Uchaguzi huo uliokuwa umepangwa kufanyika wiki iliyopita, uligeuka kuwa kama sinema baada ya kuibuka kwa vurugu za kurushiana makonde kati ya wafuasi wa Ukawa na Polisi kufuatia kuahirishwa baada ya zuio la muda Mahakama lilowekwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Zuio hilo la Febriari 5, lililowekwa na Susan Massawe na Saad Khimji dhidi ya Mkurugenzi wa Jiji na Jiji la Dar es Salaam, lilidaiwa kutolewa na Hakimu Mkazi Mkuu Mahakama ya Kisutu, Waliarwande Lema.

Lema amekanusha kutia amri ya kuzia uchaguzi wa Jumamosi iliyopita, uliahirishwa na kufuatiwa na vurugu zilizowakisha Waitara na Mdee katika mahakama hiyo kwa tuhuma za jinai.

Mbowe afura umeya Dar

FREEMAN Mbowe, mwenyekiti mwenza wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) amesema kuwa, umoja huo kamwe hautaomba Umeya wa Jiji la Dar es Salaam bali watadai,anaandika Happyness Lidwino.

Amesema, Jeshi la Polisi linafanya hujuma kwa kuzuia mikutano pamoja na kukamata wabunge pia madiwani wa Ukawa na kwamba, hiyo ni mikakati ya kukisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushinda uchaguzi wa umeya Dar es Salaam.

Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema-Taifa amesema umoja huo haupo tayari kushiriki uchaguzi wa Meya kwa kushtukiza akidai kuwepo kwa mkakati huo.

Amesema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho na kwamba, mara zote wamekuwa wakitaarifiwa kwa kushitukiza ili wasipate muda wa kujiandaa.

“Sasa tumechoka kuwabembeleza, mara zote huwa tunafanya kwa kuheshimu maamuzi yao hata kama wanavunja katiba,” amesema Mbowe na kuongeza;

“Jana wabunge na madiwani wetu walienda kwa Mkurugenzi wa Jiji kwa lengo la kutaka kujua tarehe ya uchaguzi, lakini hatukupata, kwa kuwa tumeshaomba hawataki sasa tutakachoamua tusilaumiane. Tumechoka kudai haki kwa kubembeleza na sasa hatutaomba tena.”

“Tunakosa imani na viongozi wa kiserikali na Jeshi la Polisi kwa ujumla juu ya utendaji wake na kutokana na yanayoendelea yakiwemo ya viongozi wetu wa chama kukamatwa tunapata wasiwasi inawezekana polisi ni vibaraka wa (CCM),”amesema Mbowe.

Akieleza baadhi ya maazimio ya Kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichokaliwa tarehe 1 Machi mwaka huu amesema, kilitafakari utendaji wa Rais John Magufuli na kubaini kuwa, serikali yake inavunja misingi ya utawala bora ikiwemo na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kushindwa kusimamia majukumu yake.

Kamati Kuu pia iliazimia kuunda uongozi wa chama kutoka katika wilaya zote za kichama ambazo zinaunda Mkoa wa Dar es Salaam ambapo uongozi utakuwa na wajumbe 25 ambao ni wabunge na viti maalumu wilaya zote, mameya, Mratibu Kanda ya Pwani pamoja na baadhi ya madiwani.

” Tumefanya hivyo kwa makusudi ili kuweza kupanda na uchafu wote unaotendeka katika mikoa yetu ya kichama kwani jiji zima tumelishikilia sisi hao walioteuliwa ndio wataongoza jiji hili tulilolipa jina la Great Dar,” amesema Mbowe.

Amesema chama kinaandaa mkutano mkubwa utakaofanyikia Mwanza ambao utashirikisha viongozi wa nchi nzima pamoja na wabunge kwaajili ya kujadili hali ya chama na jinsi ya kujipanga kwa uchaguzi wa mwaka 2030.Mkutano unatarajiwa kuanza tarehe 13 Machi mwaka huu.

MwanaHalisiOnline

Tuesday, March 1, 2016

Mbowe amshitaki Magufuli kwa maaskofu

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amemshitaki Rais John Magufuli mbele ya maaskofu kadhaa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Mbowe amedai kuwa Serikali yake ya Awamu ya Tano imekuwa ikiwatimua watumishi mbalimbali wa umma bila kuwapa nafasi ya kuwasikiliza kupitia kampeni ya kupambana na ufisadi, inayotambulishwa kwa kaulimbiu ya ‘utumbuaji majipu’.

Akizungumza jana katika ibada maalumu ya shukrani kwa kumaliza uchaguzi mkuu salama, iliyofanyika kwenye Usharika wa Nshara wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT na kuhudhuriwa na Mkuu wa KKKT, Askofu Dk. Frederick Shoo, na maaskofu wastaafu Dk. Erasto Kweka na Dk. Martin Shao, Mbowe alisema (wapinzani) hawaridhishwi na hatua ya serikali ya Rais Magufuli kuendeleza timuatimua na kuwasimamisha kazi watumishi wa umma 160 tangu aingie madarakani bila kuwapa nafasi ya kuwasikiliza.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema wapinzani wako tayari kuipongeza serikali wakati wowote inapofanya mambo mazuri kwa manufaa ya taifa, lakini kwa sharti kwamba mara zote iwe inahakikisha sheria za nchi zinasimamiwa, mali na rasilimali za umma zinalindwa na kila kitu kinafanyika kwa kuzingatia taratibu zilizopo.

"Kutokana na hali ya sintofahamu kutamalaki katika taifa kwa sasa, hakuna mtumishi wa umma aliye na amani kutokana na mfumo unaoitwa kutumbua majipu. Tunasikia watumishi wa umma wakifukuzwa kazi bila kusikilizwa.

“Mpaka sasa kuna watumishi 160 wamefukuzwa na wengine kusimmishwa. Lakini pia zaidi ya taasisi na idara za serikali zipatazo 20 hazina uongozi…hii si sahihi,” alisema.

Katika ibada hiyo, Mbowe alikuwa ameongozana na wabunge 16 na makada wengine mbalimbali wa Chadema, alitoa sadaka ya Sh. milioni 279 kwa ajili ya kusaidia ukarabati na upanuzi wa jengo la Bethel lililoko Hai.

"Sisi tunamshukuru Mungu leo kwa kuwa tuko salama ndiyo maana tunatoa sadaka. Sadaka yetu tunaielekeza kwenye upanuzi na ukarabati wa jengo hili la Betheli la Usharika wa Nshara. Kwa hiyo, nawaomba sana viongozi wa dini na Watanzania kuliombea taifa kutokana na hali inayoendelea," alisema Mbowe.

Kiongozi huyo ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema wabunge 42 wa Chadema wamemuunga mkono kwa kuchangia kanisa hilo Sh. milioni 131.5; mwanasiasa mkongwe na mfanyabiashara, Philemon Ndesamburo alimchangia Sh. milioni 50; marafiki zake wa Arusha Sh. milioni 49.9; Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Edwin Mtei Sh. milioni mbili; makada wengine wa Chadema Sh. milioni 15 na Kamati ya Maandalizi Sh. milioni 41.

Katika hatua nyingine, Mbowe alitumia nafasi hiyo pia kuzungumzia mgogoro wa uchaguzi wa kumpata Meya wa Jiji la Dar es Salaam kwa kuitupia lawama CCM kwa madai kuwa ndio wanaokwamisha kwa maslahi yao.

Alisema jambo hilo pia linasikitisha kwa sababu sasa ni miezi minne imepita huku haki ya wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kuwa na Meya wao ikiendelea kuminywa kutokana na CCM kutoheshimu demokrasia na kutaka waendelee kuongoza licha ya wananchi kufanya uamuzi wao kupitia sanduku la kura katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.

Chadema na Chama cha Wananchi (CUF) vinavyoshirikiana kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ndivyo vyenye idadi kubwa ya madiwani kulinganisha na CCM, hivyo kwa mujibu wa Mbowe, CCM wamebaini kuwa hawawezi kushinda na sasa wanajitahidi kadri wawezavyo kukwamisha uchaguzi huo.

ASKOFU SHOO AZUNGUMZIA UTUNZAJI MAZINGIRA
Awali, akihubiri katika ibada hiyo, Askofu Dk. Shoo alielezea kusikitishwa kwake na uharibifu wa mazingira unaoendelea nchini.
Alisema takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya eneo la ardhi liko katika hatari ya kugeuka jangwa na dalili zake ni kuongezeka kwa joto duniani na mabadiliko ya tabia nchi.

"Bado hatujawa mawakili wema wa mazingira. Ukame, mafuriko, kupotea kwa rutuba na ubora wa ardhi na mabadiliko ya tabia nchi ni matokeo ya sheria za mazingira kutosimamiwa ipasavyo kukabiliana na hali hii. Sheria ziko nyingi, lakini hakuna utayari wa moja kwa moja wa kuwajibika katika kuzitekeleza," alisema Askofu Shoo.

Akifafanua Zaidi, kuhusu uharibifu huo, Dk. Shoo alisema zaidi ya hekta 400,000 za misitu huteketea kila mwaka, ndiyo maana kanisa limeamua kujikita katika kutoa elimu na kupiga kelele ili mamlaka zinazohusika zichukue hatua.

PICHA ZA TUKIO LA KUWEKWA NDANI HALIMA MDEE

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee akiwasili katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam leo kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tuhuma za shambulio, mbunge huyo alikosa dhamana na anashikiliwa na Jeshi la Polisi. (Picha na Francis Dande)
Halima Mdee (katikati) akiwa na mbunge wa Bunda, Ester Bulaya (wa pili kushoto) pamoja na wafuasi wa Chadema wakati akielekea mahabusu.
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee akisindikizwa na Ofisa wa Polisi aliyeshika faili kuelekea mahabusu baada ya kukosa dhamana katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam leo.
Mwanasheria wa Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Prof. Abdallah Safari akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, baada ya mbunge huyo kukosa dhamana.