Monday, April 30, 2012

CHADEMA WASHINDA KESI YA UBUNGE SUMBAWANGA MJINI

CHADEMA WASHINDA KESI YA UBUNGE SUMBAWANGA MJINI

Matokeo hayo yametenguliwa katika kesi ya pingamizi la ushindi wa Mbunge huyo iliyofunguliwa na mgombea wa CHADEMA,  Mwalimu Norbet Joseph Yamsebo  kufuatia kasoro zilizojitokeza wakati wa uchaguzi wa mwaka 2010 ikiwa ni pamoja na madai ya kutoa rushwa  kwa makundi mbalimbali ambapo watu wengi walijitokeza kutoa ushahidi na kukiri kuwa ni kweli walipokea vitu kama vile fedha, baiskeli, pikipiki, vinywaji, kinanda kwa Kanisa Katoliki n.k. 
Kiti hicho kilichokuwa kikishikiliwa na Aeshi Khalfan Hilaly, CCM, sasa kipo wazi.






CHANZO: http://www.wavuti.com

HABARI NILIZOPATA SASA HIVI KUHUSU  KESI YA KUPINGA  USHINDI WA MBUNGE WA CHADEMA BIHARAMULO MHESHIMIWA MBASSA,  YANASEMA KWAMBA MHESHIMIWA MBASSA AMEIBUKA MSHINDI NA KUTUPILIA MBALI SHAURI LA MGOMBEA WA CCM.

CHADEMA: Wafuasi wetu 15 wameuawa

POLISI WAKANUSHA, WAUNDA TUME KUCHUNGUZA

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetishwa na wimbi la mauaji yanayotishia amani ya nchi kikidai kuwa jumla ya wanachama wake 15 wameuawa katika wilaya ya Igunga peke yake.
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alidai kuwa mauaji hayo yana mkono wa serikali ya CCM, ambayo imeona wazi kuwa upepo wa kisiasa umekiendea vibaya na sasa kinataka kujiimarisha katika utawala kwa kuua watu wanaoipinga.
Akifungua kikao cha Baraza Kuu la chama hicho jijini Dar es Salaam jana, mwenyekiti huyo alifafanua kuwa mbali na kuuawa kwa watu wanne kwa pamoja na juzi kifo cha mwenyekiti wao wa tawi huko Arumeru mkoani Arusha, jumla ya wanachama wake 15 wameuawa katika wilaya ya Igunga peke yake tangu kumalizika kwa uchaguzi mdogo wa jimbo hilo mwaka jana.
“Wapo watu wanadhurika kwa sababu ya kuwa CHADEMA na mfano mzuri ni Mbunge Highnes Kiwia, aliyeshambuliwa na wahuni wa serikali ya CCM. Kule Igunga zaidi ya wanachama wetu 15 waliuawa na lengo la yote haya ni kuwakatisha tamaa wananchi ili wasiiunge mkono CHADEMA,” alisema Mbowe.
Alisema mauaji ya watu wanne yaliyotokea Arusha wiki mbili zilizopita na ya juzi ya mwenyekiti wa tawi wa chama hicho, hayawezi kuepushwa na hujuma za kisiasa kwa kuwaandama watetezi wa haki za wanyonge.
Alisema serikali yoyote inayotumia vyombo vya dola na vijana wake kuua watu, haina uhalali wa kuwa madarakani na kwamba chama hicho kimeamua kwa dhati kupambana na kila aina ya uchafu ndani ya nchi kwa nia ya kuwaokoa Watanzania wanaoangamia.
Mbowe alizidi kuishambulia serikali akisema hatua ya kunyamazia mauaji na kupigwa kwa viongozi na wanachama wa CHADEMA ni kielelezo tosha cha watawala kukata tamaa na ishara ya wazi ya kutapatapa.
Polisi yakanusha, yaunda tume
Kutoka jijini Arusha, Jeshi la Polisi nchini limedai kuwa halina habari juu ya mauaji hayo kuhusishwa na mambo ya kisiasa, lakini limekubali kuunda tume maalumu ya kuchunguza vifo hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Naibu Kamishna wa Polisi, Isaya Mngulu, ilisema kuwa Mkuu wa Jeshi hilo nchini, Inspekta Jenerali, Saidi Mwema, ameunda tume maalumu itakayokuwa chini ya Mngulu na kujumuisha maofisa wa ngazi mbalimbali wa jeshi hilo kwa ajili ya kuongeza nguvu ili kufanikisha uchunguzi wa matukio ya mauaji na vurugu wilayani Arumeru.
Mngulu pasipo kuingia kwa undani kutokana na tuhuma za mauaji hayo kuhusishwa na mambo ya kisiasa, alikiri kuwa matukio hayo yamesababisha hali kuwa tete katika wilaya ya Arumeru, hivyo watalazimika kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na wananchi ili wahusika wote waweze kukamatwa.
Aliwataka wananchi wenye taarifa kuzitoa jeshi hilo na kwa viongozi wa serikali huku akiwahakikishia kuwa hakuna atakayewataja hadharani.
Mchakato wa Katiba, rufaa ya ubunge
Kuhusu mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya, Mbowe alisema wakati Kamati ya Katiba inafanya kazi yake CHADEMA itakuwa njiani kuwaelimisha wananchi ni vitu gani vinapaswa kuwepo na kutokuwepo katika Katiba hiyo.
Alisema wananchi watajadili Katiba kadiri wanavyotaka na siyo kama anavyotaka Rais Jakaya Kikwete na kwamba hata suala la Muungano litajadiliwa.
Akiongelea sababu za kukata rufaa katika jimbo la Arusha mjini Mbowe alisema wamefanya hivyo kwa ajili ya kuweka kumbukumbu ya kusimamia haki, huku akibainisha kwamba hata kama uchaguzi wa jimbo hilo utafanyika leo wana uhakika wa kushinda kwa kiwango kikubwa.
“Tunaamini wapo majaji ambao wana nafasi ya kusimamia haki pasipo kuyumbishwa na wao watafanya kazi hiyo kwa uadilifu kwa ajili ya kuweka kumbukumbu za upatikanaji wa haki sawa; hiyo ndiyo sababu iliyotufanya tukate rufaa katika jimbo la Arusha mjini,” alisema Mbowe.
Akizungumzia mfumko wa bei mbowe alisema hali ni mbaya kwa mfumko kutoka asilimia 19 hadi 24 na kubainisha hali hiyo inachangiwa na watendaji wanaojifikiria wenyewe pasipo kuwaangalia wananchi wanaowatumikia.
“Kama hali itaendelea hivi ni hatari kwa usalama wa nchi kwani matumizi ya serikali peke yake ni shilingi trilioni 12 na ukiangalia kwa umakini wanaochangia hali hii ya matumizi makubwa ni viongozi wanaotumia fursa vibaya,” alisema Mbowe.
Sabodo aishukia serikali
Naye kada maarufu wa CCM na mfanyabiashara maarufu nchini Mustapha Sabodo, aliyealikwa katika mkutano huo, aliishukia serikali ya CCM akidai kuwa viongozi wake hawana shukrani kwa namna alivyojitolea kwa miaka 50 kuisaidia kwa kila njia.
Sabodo alisema hajawahi kupewa hata ‘asante’ na viongozi wa CCM, pamoja na kuipa msaada wa mabilioni ya fedha, hali ambayo imemsikitisha.
“Mimi si mwanasiasa na hata wakati wa uhai wa Baba wa Taifa (Mwalimu Nyerere) nilitaka kupewa uwaziri na baadaye uenyekiti wa benki ya NBC nikakataa kwa sababu mimi ni mfanyabiashara lakini juu ya yote hawajui hata kusema asante kwa niliyowafanyia,” alisema Sabodo.
Sabodo alikiri kuwa CHADEMA imeonyesha kuwa ni chama makini, kinachopigania maslahi ya Watanzania na kuthamini mchango wa kila mtu bila ubaguzi, na kudai kuwa atawafuata marafiki zake akiwemo waziri mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba na kuwaeleza umuhimu wa kuiangalia CHADEMA kama chama kinacholenga kuwakomboa wanyonge. Aliahidi kuzidisha misaada zaidi kwa CHADEMA, na kukumbushia ahadi yake ya kuwapatia jengo la kisasa kwa ajili ya ofisi.
Alisema dhana kuwa chama hicho ni cha kidini ni propaganda za watu walioshindwa kwenda na kasi yake na kutaka kutumia nafasi ya kuwachonganisha wananchi ili wapate kuwatawala milele.
“Wanasema CHADEMA inabagua dini huo ni uongo na ninakuombeni muendelee kupambana CHADEMA hoyeee!” alisema Sabodo huku wajumbe wa baraza kuu wakimshangilia.
Awali katibu mkuu wa CHADEMA Dk. Willibrod Slaa akiuelezea uzalendo wa Mustapha Sabodo, alisema amekuwa muwazi kwa mambo yake licha ya wafanyabiashara wengi kubaki katika mawazo mgando kuwa mtu anayetaka mambo yake yaende sawa ni lazima awe mwanachama waCCM.
Alisema watu wengi wenye uwezo na hata wasomi wamekuwa wakijificha kuzungumzia siasa hususan kwa upande wa upinzani kwa hofu ya kuharibikiwa mambo yao tofauti na Sabodo ambaye ni muwazi kwa kila anachokifanya.
Alisisitiza ufisadi wa Tanzania unatokana na mambo mengi kufanywa gizani kwa kuwa hadharani watu wanaogopa wataumbuliwa.
“Wanatuuliza tunapokea hela za Sabodo tuna uhakika gani kama si za fisadi, sisi tunawaambia huyu hafanyi gizani na kama ana madhambi leo hii kwa namna anavyojitoa kwa CHADEMA asingekuwa na kitu,” alisema Dk. Slaa.

CHANZO - Tanzania Daima

CCM yahofia kung’oka

SASA YATAKA MAWAZIRI WASHTAKIWE

HALI ya upepo mbaya wa kisiasa imedhihirika kukitisha Chama cha Mapinduzi ambacho katika namna isiyokuwa ya kawaida, kimeitaka serikali kuwatimua sio tu mawaziri bali hata makatibu wakuu na wakurugenzi wa wizara zilizotuhumiwa na Bunge kufuja fedha za umma.
Mbali na kuharakisha kuwafukuza, chama hicho pia kimeitaka serikali kuwatimua makatibu wakuu na wakurugenzi wa wizara zote zilizotuhumiwa kuhusika na ubadhirifu na kisha kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya dola kwa hatua za kisheria.
Hatua hiyo isiyokuwa ya kawaida imechukuliwa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi (NEC) wa CCM, Nape Nnauye, ambaye amekiri kwamba hali ya kisiasa kwa upande wa chama hicho ni mbaya.
Akizungumza katika maandamano ya Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao walivamia ofisi za chama hicho jijini Dar es Salaam jana, Nape alisema ili kurudisha imani ya wananchi lazima mawaziri waliotajwa katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), wawajibishwe, na kisha kufikishwa katika vyombo vya dola kwa hatua zaidi za kisheria.
Nnauye alisema haitakuwa jambo la busara kuwatimua mawaziri na kuwaacha makatibu wakuu na wakurugenzi ambao ndiyo watendaji wakuu katika wizara.
“Hatua ya kwanza kwa mawaziri hao ni kuwawajibisha kwa kuwavua madaraka ya uwaziri na hatua nyingine itafuata kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuwachunguza na kuwafikisha mahakamani.
Alisema kuwa suala la kuwahamisha halitakuwepo kama ambavyo imezoeleka, bali ni kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili kuleta heshima katika serikali ya Chama cha Mapinduzi.
“Tunajua wananchi wanasubiri kwa hamu juu ya kuvunja kwa baraza la mawaziri hivyo lazima ifanyike kwa haraka kutokana na mazingira yaliyopo sasa,” alisema Nnauye.
Wanafunzi hao waliandamana wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali wa kuwataka mawaziri waliotuhumiwa wanashtakiwa kama sehemu ya kujivua gamba ndani ya CCM.
Mweyekiti wa shirikisho hilo Assenga Abbakari alisema kama makada wa chama hakuna kurudi nyuma katika hilo na kudai kuwa ni vema wote wakakamatwa na kufilisiwa ili kuwa mfano kwa mawaziri na watendaji wengine wenye tabia ya kutafuna mali ya umma.


CHANZO - Tanzania Daima

TUSIPUUZE WOSIA WA MWALIMU NYERERE - LETICIA NYERERE MP

Ni jambo la kusikitisha kuona nchi yetu inatafunwa wazi wazi.Nasikitika kusema kuwa nadhani baadhi ya watanzania tulipuuza wosia wa baba yetu, baba wa taifa Mwalimu Julius K. Nyerere. Nadhani laana zake zimeanza rasmi. Baada ya kumfahamu na kuishi na mwalimu kwa takribani miaka 12 kama mkwe wake, nilitambua nguvu pekee ya mwalimu ambayo haiazimishwi,Nasikitika baadhi yetu tumeshindwa kumuenzi baba wa taifa na ninachokiona mbele yangu ni laana za mwalimu baada ya kupuuza wosia wake. Watanzania tusishangae yote yanayotusibu, kuna sababu, tupige magoti ,tutubu tumweke mwalimu kwenye maombi yetu, pengine mwenyezi Mungu atatusamehe!.Leticia Nyerere(MP) 

Sunday, April 29, 2012

Hukumu ya kupinga ubunge sumbawanga mjini

Kesho tar 30/04/2012 ndo siku ya hukumu ya kesi kupinga ubunge wa bw Aesh Hilaly Khalfan Wa Sumbawanga mjini, kesi hiyo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya CHADEMA bw Noberth Yamsebo akilalamikia ugubikwaji wa uvunjifu wa sheria ya uchaguzi uliofanywa na bw Aeshi kwa kujihusisha na rushwa na uchakachuzi wa matokeo uliofanywa na msimamizi mkuu wa uchaguzi jimbo bi Sylvia Siriwa. 

Hali ni shwari hapa Sumbawanga, askari wamemwagwa kwa wingi sana. Kila upande kwa maana walalamikaji CHADEMA na walalamikiwa CCM wanajigamba kwa kuibuka kidedea hapo kesho. Wenye kujihakikishia zaidi ni wanaccm kwani wanasema mahakama na dola ni ccm na hivyo wao hawana wasi wasi kwani mbunge wao lazima ashinde, waandishi wa habari nao wamejiandaa vilivyo kuhakikisha wanaripoti vilivyo yote yatakayojili mahakamani, na hasa ikizingatiwa kuwa waandishi wengi wako upande wa bw Aeshi na ndo maana walishindwa kuripoti namna kesi ilivyoendeshwa hadi ushahidi ulivyofungwa kwani kwa kiasi kubwa ilionekana kwao baadhi ya waandishi wa habari ni udhalilishaji kwa bw Aeshi na kwa baadhi ni wale waandishi njaa ambao kwao hawawezi kuripoti bila fedha na ndo maana hiyo kesho bw Aeshi akishida kama wanavyotegemea watajipendekeza kwake na kupata chochote.

Zaidi tu ni kuwa ujumbe unasambazwa na watu wasiojurikana kwa njia ya sms kuwa Tahadhari: Usiende mahakamani J3. Kutakuwa na; Mbunge ni yule yule, askari wanafanya maandalizi, wadai wamelazimishwa ingawa hawapendi, jaji apewa ulinzi makali na jeshi la polisi”

Taarifa za uhakika ni kuwa ujumbe huo polisi wameupata na Jana kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa aliwaita baadhi ya viongozi wa CHADEMA mkoa wa Rukwa akiwepo katibu mh Ozemu Chapita na kuwaeleza kuwa ujumbe huo waupuuze kwani polisi haijihusishi na wala haitakuja jihusisha na siasa za Sumbawanga, na kuhusu askari wengi waliomwagwa hivi karibuni,kamanda huyo alisema hao ni askari wapya wako mbioni kupelekwa mkoa mpya wa Katavi kama vituo vyao vipya vya kazi walivyopangiwa na kuwa muda wowote wataondoka, mwishowe aliwaasa viongozi hao wa CDM wawahamasishe wapenzi na wanachama wao wajitokeze kwa wingi na wasiwe na hofu na usalama wao, zaidi ya yote aliwaahidi kutoa hata gari kwa ajili ya kuwatangazia wananchi kupuuza uzushi huo wa ujumbe uliosambazwa.



CHANZO - JF

TGNP yatoa madai ya Jumla katika Katiba Mpya


MTANDO wa Jinsia Tanzania (TGNP) umetoa maoni ya jumla ambayo wangependa yaingizwe kwenye mchakato wa uundwaji wa Katiba Mpya ya Tanzania. Maoni hayo yalitolewa na TGNP kwenye semina ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika semina hiyo, Mratibu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa TGNP, Bi. Lilian Liundi alisema madaraka katika muhimili wa utawala wa sasa ni makubwa hivyo kushauri yapunguzwe na kuwe na utengano kati ya mihimili mikuu mitatu ya nchi.
Bi. Liundi pia ametaka uwepo wa uwiano sawa wa kijinsia (50/50) huku akitaka mawaziri wasiwe wabunge na uwepo wa utaratibu wa viongozi (wabunge, madiwani) kuwajibishwa katikati ya mihula tofauti na ilivyo sasa.
Aidha mambo mengine ambayo Bi. Liundi ameyatoa kama changamoto na kushauri yaingizwe kwenye mchakato wa Katiba Mpya ni pamoja na kufutwa kwa adhabu, uwepo wa uhuru wa kupinga matokeo ya urais baada ya kutangazwa na ukomo wa uongozi wa wabunge, madiwani na serikali za mitaa.
Amesema siasa za uliberali mamboleo zilizoletwa na mataifa ya nje katika nchi za kiafrika zimesababisha mtafaruku mkubwa katika siasa za kiafrika, hali ambayo imezua migomo na mapambano dhidi ya uporaji wa rasilimali, ubinafsishaji wa huduma za afya na kuzifanya kama bidhaa na uporaji mkubwa wa ardhi na madini.
“Harakati hizi zimesababisha makundi ya kijamii, vyama vya siasa na wanaharakati kuanza kudai mabadiliko ya katiba katika nchi zao. Mfano mzuri ni nchini Kenya 2007,” alisema.
Pamoja na hayo alisema licha ya mchango mkubwa unaotolewa na wanawake nchini Tanzania bado hakuna fursa sawa kimgawanyo wa masuala mbalimbali.
Asilimia 80 ya nguvu kazi vijijini ni wanawake na asilimia 60 yao ni wazalishaji wa chakula. Wanawake ambao hawana ajira ni asilimia 40.3 (2006) ukilinganisha na wanaume ambao walikuwa asilimia 19.2 ( 2006), asilimia 66 ya wanawake wanafanya kazi zisizokuwa na kipato (kazi za huduma)… asilimia 39.5 ya wanawake hawajasoma ukilinganisha na asilimia 25.3 ya wanaume…,”
Awali akitoa mada katika semina hiyo ya wahariri, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya alisema licha ya uwepo wa maendeleo kwa kiasi fulani ukilinganisha na miaka ya nyuma, bado kuna mifumo kandamizi inayoikabili jamii ya kipato cha chini.
Alisema maendeleo ya huduma za jamii katika maeneo mbalimbali kwa kiasi kikubwa yanawanufaisha zaidi wenye nacho (matajiri) na si masikini. “Huduma za jamii zimeongezeka ndiyo lakini wanaonufaika zaidi na huduma hizo ni wachache…ukiangalia utaona Serikali inawajibika zaidi kwa wafadhili na si wananchi wake…,” alisema Bi. Mallya.
Alioneza kwa sasa hata tabaka la wasionacho na walionacho ni kubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma huku jukumu la kuihudumia jamii likirudi kwa familia zenyewe (majumbani) na si Serikali walioiweka madarakani kuwahudumia wananchi wake.
CHANZO - THE HABARI

Kigogo Chadema achinjwa Arusha

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kata ya Usa-River, wilayani Arumeru mkoani Arusha, Msafiri Mbwambo (32) ameuawa kinyama kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana.

Mamia ya wakazi wa Jiji la Arusha na Wilaya ya Arumeru jana, walifurika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, kushuhudia mwili wa Mbwambo ambaye pia, alikuwa fundi ujenzi .

Mbwambo aliuawa na watu wasiojulikana baada ya kupigiwa simu kumwita majira ya saa mbili usiku, wakati akitazama taarifa ya habari eneo la Mji Mwema akiwa na watu wengine.
Katibu wa Chadema wa Wilaya ya Arumeru, Dotnan Ndonde, alisema mara baada ya marehemu kuondoka muda mfupi baadaye, mwili wake uliokotwa eneo la Shule ya Mukidoma, Kusini mwa mji wa Usa-River umbali wa takriban kilomita mbili kutoka alipokuwa.
“Tulimkuta akiwa anavuja damu ilionekana muda si mrefu alikuwa amechinjwa na watu wasiojulikana ambao walikuwa wametoweka,”alisema Ndonde
Mwili wa kada huyo ulichinjwa kuanzia kisogoni na taarifa za uchunguzi wa madaktari jana zilithibitisha kuwa kifo hicho kimetokana na kuchinjwa.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Thobias Andengenye amethibitisha kutokea tukio hilo na kueleza kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi kuwapata wahusika waliofanya unyama huo.
Baadhi ya watu mjini hapa wamekuwa wakihusisha mauaji hayo na vuguvugu za kisiasa hasa baada ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, ambapo Chadema kiliibuka mshindi.
Hata hivyo Kamanda Andengenye amekanusha tetesi hizo na  kuwataka wananchi wasubiri uchunguzi wa polisi .
Chadema wahusisha mauaji na siasa
Mbunge wa Arumeru Mashariki kupitia Chadema, Joshua Nassari na Katibu wa chama hicho Jimbo la Meru, Ndonde, walisema tukio hilo lina harufu za kisiasa.
Ndonde alisema kwa mazingira ya tukio na hali ya kisiasa eneo la  Meru, anashindwa kuyatenganisha mauaji hayo na siasa.
“Wengi wanamjua marehemu alikuwa nguzo ya chama katika mji wa Usa ambapo Chadema tulipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mbunge.  Anapouawa kwa kuchinjwa ghafla wakati vuguvugu la siasa likiendelea, sisi tunaamini ni mambo ya siasa,”alisema Ndonde.
Mbunge Nassari ameeleza kusikitishwa kwake na tukio hilo la kinyama na kusema kuwa bado joto la kisiasa lipo juu wilayani humo na kulitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linawasaka na kuwatia mbaroni wale wote waliofanya unyama huo.
 
Kwa upande wakev aliyekuwa Mbunge Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema alisema ana wasi wasi kuwa mauaji hayo ni mfululizo wa vifo vinavyoendelea kutokea, vikihusisha viongozi wa Chadema kila baada ya chaguzi ndogo.
 
“Tumeshuhudia watu watatu, wote wakiwa wanachama wetu wakiuawa baada ya uchaguzi mdogo wa Igunga na wengine kupotea katika mazingira ya kutatanisha,” alisema Lema.
 
Lema aliongeza kuwa baada ya uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki yamekuwepo matukio ya watu kuuawa, likiwemo lile la wiki iliyopita ambapo watu wanne walikutwa wamenyongwa hadi kufa katika eneo la Tengeru.
 
“Sasa hata wiki haijapita, mwenyekiti wetu wa Usa-River anauawa kwa kuchinjwa kinyama. Tunaomba vyombo husika vifuatilie matukio haya,” alisema Lema.
Marehemu Mbwambo, ameacha mke na watoto watatu.




Matukio mengine ya mauaji 
Tukio la mauaji ya kada huyu limekuja ndani ya siku kumi baada ya mauaji mengine ya kinyama kutokea wilayani humo.
 
Aprili 21 mwaka huu, watu wanne walikutwa wamekufa kwa kunyongwa na watu wasiojulikana pembezoni mwa Mto Nduruma, katika maeneo matatu tofauti wilayani Arumeru.

Miili ya watu hao ambao ni wanaume waliokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 20-40, ilionwa na wakazi wa eneo hilo asubuhi ikiwa imetupwa.

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha  Andengenye alisema polisi wanachunguza tuko hilo na uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa watu hao waliuawa usiku wa kuamkia siku hiyo.

Andengenye alisema miili ya watu wawili iliokotwa  eneo la Daraja la Gomba Estate, mwingine uliokotwa njia panda ya kwenda Mbuguni katika eneo la Chuo cha Mifugo Tengeru na mwili mwingine uliokotwa jirani na eneo la Sekondari ya Tengeru.

“Uchunguzi wa awali unaonesha watu hawa waliuawa kwa kunyongwa kwa kuwa kuna dalili za kuvunjwa shingo,”  alisema Andengenye.



CHANZO - Mwananchi

Saturday, April 28, 2012

LWAKATARE - Kauli ya Dr Slaa si ya kwake ni ya Chama


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimelitahadharisha Jeshi la Polisi kutofanya hila yoyote ya kuhamisha mantiki ya msingi iliyotolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa.
Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama hicho jana, Wilfred Lwakatare, ilisema kauli iliyotolewa na Dk. Slaa Jijini Mwanza, ilikuwa ni msimamo wa chama na wala si ya kwake.
“Tunaona polisi wameshindwa kujibu hoja za msingi ambazo nyingine zinawahusu wao moja kwa moja… ilikuwaje tukio la wabunge wa Chadema washambuliwe na kujeruhiwa kinyama mbele ya polisi wenye silaha,” ilihoji sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa ilisema, agizo la Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, ACP Phillip Kalangi, kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo linafanya uchunguzi wa kauli alizodai ni za uchochezi na kutolewa na Dk. Slaa, ni za vitisho kwa chama hicho.
“Wao polisi wanadai wakijiridhisha Dk. Slaa alitoa kauli hizo, basi watamkamata na kumfungulia mashtaka. Hatuwezi kukubaliana na hilo kabisa,” ilisema.
Kurugenzi ya Ulinzi na Usalama ya Chadema ilisema, inashangazwa na Jeshi la Polisi badala ya kuwakamata na kuwafikisha vyombo vya sheria wale ambao wanafahamika kutenda tukio hilo kwa wabunge wao, wanaitisha mkutano na wanahabari na kutoa vitisho kwa viongozi wa chama.
Aidha, taarifa hiyo iliendelea kusema Chadema inayafuatilia kwa karibu matukio ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na uvunjwaji wa sheria uliofanywa na kuendelea kufanywa kwa makusudi na Jeshi la Polisi dhidi ya raia, na kuwafumbia macho wahusika wake.
“Uvunjaji wa haki za binadamu uliofanywa na polisi ni pamoja na mauaji wakati wa maandamano ya amani jijini Arusha, Januari 5, 2012. Pia mauaji yaliyofanyika Mbarali, Mbeya Januari 13, 2011,” Lwakatare alisema katika taarifa yake.
Pia, taarifa hiyo ilisema, jeshi hilo liliendelea na ukiukaji wake wa haki za binadamu kwa kufanya mauaji mjini Songea, Februari 22 mwaka huu, kwa kuwaua kwa kuwapiga risasi raia wasiokuwa na hatia pamoja na kuharibu mali zao.
Mauaji hayo yalitokana na maandamano ya amani ya wananchi wa mji wa Songea kuonyesha hisia zao dhidi ya uzembe wa vyombo vya dola kushindwa kudhibiti matukio ya mauaji ya mfululizo.
“Lakini kama hiyo haitoshi, Polisi walifanya vurugu huko Tandahimba Aprili 17 na 18 mwaka huu na kuharibu mali za wananchi waliokuwa wakidai haki zao katika malipo ya korosho.”
Hivyo, Chadema wanasema matukio hayo yote ni kielelezo cha uozo na uwajibikaji mbovu uliomo ndani ya Jeshi hilo ambalo badala ya kuwajibika kulinda amani na usalama wa raia na mali zao, limegeuka kuwa mlinzi wa makosa yake yenyewe na ya watawala wanaofanya dhidi ya raia wasiokuwa na hatia.
Lwakatare alisema kwenye taarifa hiyo kuwa ni karibu miaka mitano imepita tangu Chadema ilipotoa tamko juu ya vita dhidi ya ufisadi na mafisadi kwa kutoa orodha ya aibu ya mafisadi (list of shame), lakini Jeshi hilo limekaa kimya bila kutoa kauli yoyote, huku wananchi wakiendelea kuteseka kwa kuathiriwa na vitendo hivyo vya kifisadi.
“Hivyo basi Chadema haitaweza kufumbia macho vitendo hivyo vinavyofanywa na polisi kwa kujitokeza hadharani kutaka kuwalinda na kuwaficha wahalifu,” ilimaliza taarifa hiyo.

CHANZO - Nipashe

Tundu Lissu aibwaga CCM


MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dodoma imetupilia mbali madai ya kupinga matokeo ya ubunge wa jimbo la Singida Mashariki na kutangaza kuwa Tindu Lissu alishinda kihalali katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 30, 2010.
Katika kesi hiyo ya madai iliyoanza kusikilizwa tangu Machi 12, mwaka huu, walalamikaji wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) walitarajia kuleta mashahidi 51 lakini kwa sababu zisizofahamika ni mashahidi 24 tu na vielelezo saba viliwasilishwa kama ushahidi mahakamani hapo.
Katika kesi yao ya msingi walalamikaji walikuwa wakipinga ushindi wa mlalamikiwa namba moja ambaye ni Tundu Antiphas Lissu kuwa mbunge kwa madai kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa sheria za uchaguzi.
Walidai kuwa ukiukwaji huo uliufanya uchaguzi huo kutokuwa huru, wa wazi na haki na hivyo kumfanya mgombea wa CCM asiweze kupata ushindi katika uchaguzi huo.
Lissu ambaye alishinda kwa kupata kura 13,787 na kumzidi mgombea wa CCM Jonathan Njau kwa kura 1,626 alileta mashahidi wanne tu akiwemo yeye mwenyewe.
Akisoma hukumo hiyo, Jaji Moses Mzuna, alizitaja hoja zilizowasilishwa katika mahakama hiyo kuwa ni pamoja na mlalamikiwa kuandaa barua zilizodai kuwa ziliandaliwa na vyama vya siasa vya kambi ya upinzani ambavyo havikuwa na wagombea katika uchaguzi huo.
Hoja zingine ni kuwa na mawakala nje na ndani ya chumba cha kupigia kura zaidi ya sheria inavyoagiza, kutoa hongo ya usafiri na chakula kwa mawakala wa vyama vyote isipokuwa CCM, askari katika baadhi ya vituo waliacha shughuli zao na kwenda kufanya kampeni.
Hata hivyo Jaji Mzuna ambaye alikuwa akisoma hukumu hiyo huku akitoa mifano ya kesi mbalimbali zilizotolewa hukumu na Mahakama Kuu aliweka bayana kwamba mashahidi wote walifika kutoa ushahidi walionekana kujichanganya wakati wa maelezo yao.
Alisisitiza pia kwamba waleta maombi katika kesi hiyo walishindwa kuwaleta mashahidi muhimu ambao wangeweza kutoa ukweli juu ya hali halisi ya kesi hiyo licha ya kufahamika, jambo lililotafsiriwa kuwa huenda walifanya hivyo kwa kuhofia kuharibiwa kesi yao.
“Wao ndiyo waliopaswa kuthibitisha bila kuacha shaka yoyote juu ya dai lao hilo la msingi, kwani walitakiwa kuwaleta waliobaini tuhuma hizo zikitendeka kwani ni jukumu la mleta maombi kuthibitisha,” alifafanua.
Jaji huyo alisema kesi hiyo ilijikita zaidi kwenye kushuku na hivyo walalamikaji kujikuta wakishindwa kuithibitishia mahakama hiyo kikamilifu.
“Jambo la kushangaza ni kwamba mashahidi walioitwa mahakamani hapa walikuwa ni sawa na watu wanaovaa koti kwa kubadili nje ndani na ndani nje huku mawakili wa waombaji wakijigeuza kinyonga kila walipokuwa wakitoa maelezo yao.
Kabla ya kutoa hukumu hiyo Jaji Mzuna alisema ni vema mahakama zisibariki pale inapobaini kuna kila dalili za kuwanyima haki wananchi wa jimbo husika.
Aliamuru walalamikaji kumlipa Lissu gharama alizotumia katika kesi hiyo kwa mujibu wa taratibu za kisheria kuhusu madai ya gharama za kesi hiyo.
Aangua kilio
Lussu na mkewe katika hali isiyokuwa ya kawaida waliangua kilio mara baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo, huku akisema kuwa amesikitishwa na waliomshtaki kwa kile alichosema walijua hawana ushahidi wowote zaidi ya kutunga na kuhisi.
“Nakubaliana na matokeo ya hukumu hii na ni kweli kabisa haki imechukua mkondo wake, kwani waleta maombi hawakuwa na ushahidi wowote zaidi ya kutunga, kuhisi, kufundishana uwongo lakini mengi zaidi nitaongea na wananchi kule kijijini kwatu Ikungi muda mfupi baadaye,” alisema Lissu.
Hukumu hiyo ilipokelewa kwa shangwe kubwa na mamia ya watu, kiasi cha kulazimisha kuwekwa kwa vipaza sauti ili watu waliokosa nafasi ndani kuweza kusikiliza.
Ulinzi mkali wa polisi
Tangu asubuhi jana, askari polisi wengi na wale wa usalama wa taifa walitanda kila kona ya eneo la mahakama hii, kinyume kabisa na hali inavyokuwa siku zote.
Ulinzi huo uliandamana na ukaguzi mkali ambapo kila aliyeingia ndani ya jengo la mahakamana alikaguliwa, huku askari wakilazimika kuwazuia wananchi waliozidi kufurika katika mahakama hiyo kila muda ulivyosonga mbele.
Hata hivyo, haikuweza kuelezwa sababu za msingi za kuimarisha ulinzi huo, ambapo ofisa mmoja wa jeshi la polisi aliyehojiwa kwa sharti la kutotaja jina alisema ni wajibu wao kulinda amani katika matukio mazito kama hilo.

Friday, April 27, 2012

CCM katika hali mbaya Arusha; kigogo mwingine (Bananga) atimkia CHADEMA


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI. TAARIFA KWA VYA HABARI
“Mficha maradhi kifo humfichuwa “

Ni muda mrefu nimeitafakari dhamira yangu na sasa ni wakati muafaka kufikia maamuzi magumu, Nimeamua kuachia nyadhifa zangu zote ndani ya CCM ambazo ni, MJUMBE WA MKUTANO MKUU CCM TAIFA, MJUMBE WA BARAZA LA MKOA UVCCM, NA M/KITI WA KAMATI YA MAHUSIANO YA UVCCM MKOA ARUSHA.

Yaliyonisukuma ni mwelekeo mbaya wa CCM kwa sasa ambao umejiondoa kuwa Chama cha wanyonge na wakulima na sasa ni chama cha kundi la watu wachache na watoto wao ndio sababu yanayoendelea sasa ndani ya CCM yanasikitisha sana.

Usaliti na makundi ndani ya CCM yanatishia kabisa uhai wa chama na tayari yamekwisha angamiza Taifa letu, hata hivyo nafasi ya wa watoto wa wanyonge ndani ya CCM inazidi kuwa finyu, aidha ujipendekeze kwa wakubwa ili upate nafasi ya kutumikia jamii au Chama, wakati nafsi yangu haiko tiyari kusimamia uovu huu sasa nimeamua kusimamia ninachokiamini bila uoga wala unafiki, na mfano Tazameni yanoyoendelea ndani ya UVCCM ARUSHA mikono ya mtoto wa mkubwa unaumaliza umoja huo mkoani hapa.

Lakini pia uzito wa serikali ya CCM kushidwa kuwawajibisha wabadhirifu na wanaotumia vibaya madaraka waliyopewa angalia ubadhirifu mkubwa hivi karibuni uliofanywa na Mawaziri na Watumishi wengine wa Umma, Angalia jinsi Serikali imelichukulia suala la Jairo kwa mzaha, ni hatari kwa Nchi yetu kwamba wakati watoto hawana madawati wako viongozi wakubwa ambao wanashindwa kuchukuliwa hatua kwa wizi wa mabilioni ya fedha.

Sababu ni nyingi sana za kwanini nimeamua kutoka CCM, nikisema niandike zote pengine itanipasa kuandika kitabu hata hivyo ninaamini kuwa nitakuwa na fursa ya kueleza mambo mengi sana kwenye mikutano ya hadhara nitakayofanya na Chama cha kipya CHADEMA.

CHADEMA, nawashukuru kwa kunipokea nawahaidi utumishi na kazi iliyotukuka, nitajifunza kwenu na pia naamini mtajifunza kwangu ili tuweze kwa pamoja kuleta matumaini kwa wanyonge.

Kwa marafiki zangu na wanachama wa CCM, msihuzunike sana kwani ninatangulia kwenda kuwaandalia makao kwani ninajua nanyi pia mko njiani mnakuja, hata hivyo sikuwahi kuwa mwema kama malaika tulipokuwa pamoja CCM naamini kuna mahali niliwakosea kama binadamu naomba msamaha kwenu na undugu wetu ubaki, lakini kama maamuzi yangu ya kwenda Chadema yatakuwa yamewauzunisha poleni sana na muendelee kuchukia kwani hatuwezi kuukwaza utu na faraja ya Mwanadamu kwa kufurahisha nafsi za watu wachache.

Asanteni sana karibuni Chadema.


Ally Bananga.
……………………
27/4/2012.

TUNDU LISSU ASHINDA KESI YA UBUNGE


Habari zilizotufikia zinasema kwamba Mbunge wa Singida Mashariki mheshimiwa Tundu Lissu ameshinda kesi yake ya kupinga matokeo ya ubunge iliyofunguliwa na wanachama wa Chama cha Mapinduzi Shabani Itambu na Paschal Hallu, kesi ambayo hukumu yake imetolewa leo na Jaji Moses Mzuna wa  Mahakama kuu Kanda ya Kilimanjaro. Kesi hiyo ilianza kusikilizwa kwa mara ya kwanza tarehe 12 Machi 2012.
HABARI KAMILI KUWAJIA BAADAE

Kamati Kuu ya Chadema kukutana leo


Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), inakutana leo jijini Dar es Salaam kwa kikao chake cha kawaida.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika, kwa vyombo vya habari jana ilieleza kwamba kikao hicho kitapitia nyaraka za ajenda mbalimbali kwa ajili ya mkutano wa baraza kuu.

Katika taarifa hiyo, Mnyika alisema kikao hicho kitafuatiwa na Mkutano wa Baraza Kuu utakaofanyika Aprili 29.

Alisema pamoja na mambo mengine, Baraza Kuu litaandaa ratiba na maelekezo kamili ya uchaguzi wa kichama ambapo uchaguzi utaanza ngazi za chini za msingi na matawi za chama na mabaraza mwaka 2012 na kuendelea mpaka ngazi ya taifa ya chama na vyombo vyake mwaka 2013.

Alisema mkutano wa baraza kuu utapokea taarifa ya hali ya siasa na kufanya maamuzi muhimu kuhusu mwelekeo wa chama na taifa.

“Mkutano huo utathibitisha mikakati, mpango kazi na bajeti ya chama kwa mwaka 2012/2013 pamoja na kufanya maamuzi muhimu kuhusu hali ya siasa nchini,” alisema.

Aliongeza kuwa “Chadema inaendelea kutoa rai kwa wananchi na wanachama kuendelea kukiwezesha chama kutimiza dhima yake ya kuhakikisha uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa maendeleo endelevu ya Tanzania.” 
CHANZO: NIPASHE

CCM yazidi kubomoka


1,500 WAIKIMBIA BABATI

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimezidi kupoteza nguvu zake sehemu mbalimbali nchini, baada ya waliokuwa viongozi na makada wake ngazi za vijiji na wilaya kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Habari kutoka mikoa ya Manyara, Iringa na Kagera zimesema kuwa wimbi la kukimbia kwa wanachama wa CCM na kujiunga na upinzani limeshika kasi kuliko mwaka wowote tangu kuingia kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Huko Babati zaidi ya wanachama 1,500 wa CCM wakiwamo wenyeviti wa vijiji wilayani Babati wamekihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA, wakati wa mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Kati ya waliojiunga na CHADEMA ni pamoja na Bi. Zamda ambaye ni kada maarufu wa CCM mjini hapa, Wakili Lumambo na wenyeviti wawili wa vijiji vya Mruki na Hala, ambao walijiunga na wanachama wao zaidi ya 100.
Akihutubia mkutano huo, Lissu amewataka wananchi wa Jimbo la Babati Mjini na wengineo kuiga mifano ya waliokataa kuonewa na kunyanyaswa na serikali ya CCM badala yake wachukue hatua ili kuondoa uvundo, wizi na uozo unaoendelea kufanywa na watawala.
“Hatujaweka mkataba wa kuibiwa na serikali ya CCM kwa kipindi cha miaka mitano mitano, kwa hiyo hatuhitaji kusubiri hii miaka mitatu ya uchaguzi iliyobaki. Wakati umefika sasa wa kuchukua hatua, tukianzia na hili suala la mawaziri wanane, na pamoja na umaskini wetu tukiamua kusema kwa pamoja hakuna mtu atakayeweza kutuzuia,” alisema Lissu.
Huko Iringa, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kihesa Mgagao, Kata ya Ngúruwe, wilayani Kilolo, Isdori Kindole na wazee wawili, Tula Dumba (75) na Japhet Ngoda (88) wamejiunga na CHADEMA kutokana na kile walichodai kuwa wameshindwa kupata haki ya kweli kutoka katika chama hicho kupitia uongozi wao wa kijiji hususan diwani wao kutuhumiwa kuhujumu mali za umma.
Wazee hao wamedai kuwa wao waliingia kwenye TANU wakati Rais akiwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, walipata fursa ya kukaa pamoja na kuzungunza juu ya mambo mbalimbali yakiwamo ya chama pamoja na maendeleo ya Watanzania kwa ujumla.
Akindole alisema sababu kubwa iliyomfanya kuhamia CHADEMA ni kuona uongozi wa CCM wa sasa ukiwanyanyasa wananchi kupita kiasi na kunyamazishwa pindi wanapokuwa na maneno ya kushauriana juu ya maendeleo ya kijiji chao.
“Kwa sababu hiyo mimi nimeamua kutoka kwenye Chama cha CCM na kuhamia CHADEMA ili nijaribu kuona msimamo unakwendaje, maana tunanyanyaswa kupita kiasi na tukitaka kulalamika serikali haitusikilizi, na mbunge akija hapa tukilalamika hata yeye hatusikilizi. Mimi nilikuwa na mambo yangu mengi tu nimelalamika mpaka wilayani lakini sikusikilizwa. Tufanyeje wananchi?’’ alisema Japhet.
Kwa upande wake mzee Tula amesema kuwa, wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere kulikuwa na viongozi waliokuwa wamepata mafunzo ya uongozi kwa lengo la kuwasaidia wananchi lakini kwa sasa wananchi wakilalamika viongozi hawatoi msaada wowote zaidi ya kukandamizwa kutokana na viongozi wengi kukosa maadili ya uongozi.
“Hapa nilipo nina miaka 75, mzee kama mimi sikuwa na haja ya kuhama hama chama, lakini ninatafuta msaada, kama CCM kungekuwa na msaada viongozi wasio bora wangekuwa wanaonywa na kufuata maadili ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kweli nisingehama,“ alisema Tula.
Aidha, wazee hao wamesema kuwa, licha ya wao kuhamia CHADEMA, lakini bado wanaiomba serikali kumchukulia hatua mwenyekiti huyo wa Kijiji cha Kihesa Mgagao ambaye pia ni diwani wa kata na mwenyekiti wa CCM, kwani hawatendei haki wazee wa kijiji hicho na wananchi kwa ujumla na uongozi wake ni wa kidikteta.
CHADEMA yashinda viti vinane
Huko Chato, katika Mkoa mpya wa Geita, CHADEMA kimepata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mdogo wa wenyeviti wa serikali za vijiji baada ya kuibwaga CCM kwa kupata vijiji vinane kati ya 11 vilivyokuwa vikishindaniwa.
Uchaguzi huo mdogo wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi na baadhi ya viongozi waliokuwepo awali jimboni humo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vifo  ambao ulifanyika hivi karibuni uliwafanya baadhi ya Wana CCM kujiunga na CHADEMA mara baada ya matokoeo kutangazwa akiwamo aliyekuwa mgombea wa CCM wa Kijiji cha Minkoto.
Nafasi zilizogombewa zilikuwa zikishikiliwa na viongozi wa CCM kabla ya baadhi yao kujiuzulu, kuhamia vyama pinzani na wengine kuhama makazi yao na kwenda maeneo mengine.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari,  msimamizi msaidizi wa uchaguzi huo, Sodio Nyuga alisema CHADEMA kimefanikiwa kutwaa nafasi 8 za vijiji dhidi ya tatu zilizonyakuliwa na CCM .
Hata hivyo, CCM ilijifariji kwa kutwaa uenyekiti katika vitongoji 28 na CHADEMA kikipata nafasi 10, wakati wajumbe wa serikali za mitaa CCM kilijipatia wajumbe 92 na CHADEMA 46.
Katibu wa CHADEMA wa Wilaya ya Chato, Mange Sai, alisema ushindi uliopatikana ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo kwa kuwa baadhi ya vitongoji CHADEMA ilipitisha wagombe pasipo kuwa na upinzani wa chama tawala jambo ambalo linaonyesha wazi kukubalika kwa chama hicho kwa wananchi.
Alisema kuwa CHADEMA kilitegemea kuibuka kidedea katika uchaguzi huo mdogo kutokana na wapiga kura kuchoshwa na ahadi mbalimbali za serikali ya CCM ambazo zimekuwa hazina utekelezaji na badala yake baadhi ya viongozi wamekuwa wakijinufaisha kwa maslahi yao binafsi huku wakiwaacha wananchi wakitaabika.


CHANZO - Tanzania Daima

Polisi watishia kumkamata Dk Slaa

JESHI la Polisi mkoani Mwanza limesema kuwa litamchukulia hatua za kisheria Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibroad Slaa ikiwemo kumkamata kutokana na kauli zake za uchochezi alizozitoa katika mkutano wake wa hadhara mwishoni mwa wiki iliyopita.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Philipo Kalangi alisema kauli zilizotolewa na Dk Slaa ni za uchochezi ambazo zinaweza kuharibu amani ya nchi.


Mwishoni wa wiki iliyopita katika mkutano wake wa hadhara kwenye Viwanja vya Sahara, Dk Slaa alitoa wiki moja kwa Jeshi la Polisi mkoani hapa kuwakamata wale wote waliohusika na vurugu katika uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Kirumba uliofanyika mwanzoni mwa mwezi huu.


Ilidaiwa kuwa vurugu hizo ambazo zinahusishwa na wafuasi wa CCM, zilisababisha kujeruhiwa vibaya kwa wabunge wa Chadema, Samson Kiwia wa Ilemela na Salvatory Mchemli wa Ukerewe.


Katika mkutano wake, Dk Slaa alisema kama Jeshi la Polisi halitawakamata watuhumiwa na kuwachukulia hatua za kisheria ndani ya siku saba, basi yeye mwenyewe atachukua jukumu la kuwahamasisha wananchi wa Mwanza kuwakamata vijana hao.


Kamanda Kalangi alisema Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi na kusema kuwa kauli za Dk Slaa haziwezi kulilazimisha jeshi lake kufanya kazi kwa matakwa yake.


“Ofisi yangu inafanya kazi yake bila kushurutishwa, mpaka hivi sasa watu 18 wamekwisha kamatwa na kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo ila kuna baadhi ya watu ambao wapo nje kwa dhamana kutokana na kutokuwepo na maelezo ya kujitosheleza,” alisema Kalangi.
 
Alisema hawezi kuwashikilia watu ambao hawana maelezo yoyote na kinachotakiwa ni wananchi kujitokeza na kuandikisha maelezo ambayo yatawaweka hatiani watuhumiwa.


Katika hatua nyingine: Aliyekuwa mgombea wa udiwani kwa tiketi ya CCM, Jackson Masamaki amesema kwamba ametoa maelezo yake Polisi kuhusiana na tukio hilo la wabunge kukatwa mapanga.
 
Alisema hakuhusika kabisa na tukio hilo na hawezi kushiriki unyama huo, akitoa mfano wa Mbunge Machemli kwamba ni ndugu yake.
Baba, watoto wadaiwa kuua mama
Jeshi la Polisi mkoani hapa linawashikilia baba na watoto wake wawili wa kiume kwa madai ya kumuua mama yao.
 
Kamanda Kalangi alidai kuwa mnamo Aprili 24, mwaka huu saa 5:00 usiku katika Kijiji cha Kisesa B, mama huyo, Scolastica Mjangera (58) alikutwa nyumbani kwake akiwa ameuawa baada ya kupigwa na kitu kizito kichwani.


Alisema katika tukio hilo, mume wa marehemu aliyetambuliwa kwa jina la Mgeka Ngapi (75) pamoja na watoto wake wawili John Mgeka (25) na Ndaki Mgeka (18) wanashikiliwa.
 
Kamanda Kalangi alisema taarifa za awali zinaeleza kuwa kabla ya kifo hicho kulikuwa na mgogoro wa kugawana fedha zilizotokana na kuuzwa kwa shamba la marehemu.
 
Alisema marehemu aliuza shamba lake kwa Sh5 milioni ambalo linadaiwa kuwa ni la urithi kutoka kwa wazazi wake. Kamanda huyo alidai kwamba baada ya kupokea fedha hizo, aliwagawia kila mmoja kiasi cha Sh200,000 ambazo walizikataa.


Alisema kuwa baada ya kutokea kwa mzozo katika nyumba hiyo, marehemu alitoa taarifa katika ofisi za Serikali ya Kijiji na kabla kuamuliwa kwa ugomvi huo, marehemu akakutwa ameuawa.


CHANZO - MWANANCHI

Thursday, April 26, 2012

MAKALA : Kura ya kutokuwa na Imani na Waziri Mkuu ni kura dhidi ya Rais na Chama tawala!

Binafsi naweza kusema kwamba, nikiangalia kiufundi naweza kusema kuwa kama kuna sababu kubwa na ya msingi ya kuvunja baraza la mawaziri siyo shinikizo la wanasiasa, wananchi au watu wengine bali KUSHINDWA KUWAJIBIKA kwa pamoja. Kwenye serikali kuna nadharia ya "collective responsibility" kwamba mawaziri wote wanafanya kazi kwa pamoja kwa ridhaa ya Rais.

Ikumbukwe kuwa katika nchi yetu chombo kikuu cha kumshauri rais juu ya utendaji wa mambo mbalimbali ya serikali na majukumu yake siyo Bunge, au vyama vya siasa bali ni Baraza la Mawaziri. Katiba yetu inaliweka hili wazi kwa maneno yafuatayo Ibara ya 54:3 "Bila ya kuathiri masharti yaliyomo katika ibara ya 37(1) ya Katiba hii, Baraza la Mawaziri litakuwa ndicho chombo kikuu cha kumshauri Rais juu ya mambo yote yanayohusika na utekelezaji wa madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii, na litamsaidia na kumshauri Rais juu ya jambo lolote litakalowasilishwa kwenye Baraza hilo kwa mujibu wa maagizo maalum au maagizo ya jumla yatakayotolewa na Rais."

Na kutokana na uzito huu - kwamba ndicho chombo cha kuaminiwa na rais kumpa ushauri - katiba inaweka kinga kamili (absolute immunity) kwa baraza hilo linapotoa ushauri kwa Rais. Inasemwa "Suala kama ushauri wowote, na ni ushauri gani, ulitolewa na Baraza la Mawaziri kwa Rais, halitachunguzwa katika mahakama yoyote." Kwa maneno mengine mawaziri wanaweza kutoa ushauri pasi ya hofu kuwa mambo waliyoshauri yanaweza kutumiwa dhidi yao mahakamani au hata kuchunguzwa!

Sasa dhana hii ya kuwajibika kwa pamoja kwa baraza la mawaziri kimsingi inaenda sambamba na hoja ya kutokuwa na imani na waziri mkuu (serikali). Kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu siyo kura dhidi ya mtu binafsi! Ni kura dhidi ya serikali na inapopigwa serikali nzima lazima ivunjwe na siyo tu kuvunjwa lakini serikali nzima inatakiwa kujiuzulu na kuitisha uchaguzi mpya. Wikipedia inaelezea hili hivi (kwa sisi tunaofuata mfumo wa Westminster) "if a vote of no confidence is passed in parliament, the government is responsible collectively, and thus the entire government resigns. The consequence will be that a new government will be formed, or parliament will dissolve and a general election will be called" Huwezi kuwa na kura ya kutokuwa na imani na serikali na Rais akabakia! Huwezi kuwa na kura ya kutokuwa na imani na serikali na Bunge likabakia! If one falls, the other must follow!

Nadhani ni makosa kufikiria kuwa kura hii ni dhidi ya Pinda kama Waziri Mkuu; mtazamo huu siyo sahihi. Pinda ni Waziri Mkuu wa Serikali iliyoko madarakani. Yeye kama Waziri anafanya kazi kwa mujibu wa Katiba lakini akitekeleza majukumu yake chini ya Rais. Bahati mbaya sana Waziri Mkuu wetu siyo mtendaji (a non-executive Prime Minister) yaani siyo anayeunda serikali. Waziri Mkuu wetu japo anapitishwa na Bunge hawajibiki kwa Bunge moja kwa moja! Ibara ya 53:1 ya Katiba iko wazi katika hili "Bila ya kuathiri masharti ya Katiba hii, Waziri Mkuu atawajibika kwa Rais kuhusu utekelezaji wa madaraka yake." Hii ina maana ya kwamba, Waziri Mkuu akiboronga kama yeye chombo cha kumwajibisha ni kilichomteua yaani Rais!

Na kifungu kinachofuatia kinaiweka dhana hii ya "kuwajibika kwa pamoja" kwenye Katiba yetu. Kifungu hicho kinasema "Serikali ya Jamhuri ya Muungano, chini ya mamlaka ya Rais, ndiyo itakuwa na uwezo wa kufanya maamuzi juu ya sera ya Serikali kwa jumla, na Mawaziri, chini ya uongozi wa Waziri Mkuu, watawajibika kwa pamoja Bungeni kuhusu utekelezaji wa shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano." Ni muhimu kutambua kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano mkuu wake siyo Waziri Mkuu! Waziri Mkuu ndiye "kiongozi wa shughuli za serikali Bungeni". Hata hivyo, katiba pia inampa madaraka Waziri ya kusimamia shughuli za kila siku za serikali kwenye ibara ya 52:1 ya Katiba yetu. Hata hivyo madaraka hayo yanafungwa na kifungu hicho cha 53:1

Ibara ya 33:2 ya Katiba yetu inasema hivi kuhusu madaraka ya rais kuwa "Rais atakuwa Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu." Ni vizuri kuona tofauti ya "kiongozi" inavyotumiwa kwa Waziri Mkuu na kwa rais. Waziri Mkuu nimeonesha anaitwa "kiongozi wa shughuli za serikali Bungeni" yaani "leader of Government business in the National Assembly" lakini rais ni "Head of Government". Hii ina maana gani basi?

Hii ina maana ya kwamba, kama serikali inapwaya, kama serikali haitekelezi kazi zake vizuri na kama inaonekana kuwa serikali imechafuliwa sana basi mtu sahihi na wa kwanza kulaumiwa ni Rais! Waziri Mkuu anaweza kulaumiwa kama kule bungeni mawaziri walikuwa wanagongana au walikuwa hawawajibiki kwa pamoja. Lakini kama ni suala la serikali nzima kuwa na matatizo basi mtu sahihi wa kubebeshwa lawama ni Mkuu wa Serikali (head of government) yaani rais.

Sasa, kwa vile serikali ni moja ni vigumu kutenganisha kuwajibika kwa Waziri Mkuu na kuwajibika kwa rais. Ikumbukwe ni Rais ndiye anayemteua Waziri Mkuu akiwa na uhuru kamili (absolute freedom) na hulipendekeza jina hilo kwa Bunge. Waziri Mkuu mkuu anasimamia utekelezaji wa serikali kwa niaba ya Rais. Sasa Katiba yetu haijaweka utaratibu wa kumpigia rais kura ya kutokuwa na imani lakini imeweka utaratibu dhidi ya Waziri Mkuu. Kwa msingi wa kuoanisha uhusiano ulipo kati yaWaziri Mkuu na Rais ni wazi kuwa kumpigia kura Waziri Mkuu ni kupigia kura serikali; na kuipigia serikali ni kumpigia kura Rais ambaye ndiye MKUU WA SERIKALI. Huwezi - narudia tena - kujipanga kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu halafu ukasema una imani na Rais! Huwezi kumnyoshea mkono Waziri Mkuu kuhusu utendaji mbovu wa seriakli bila wakati huo huo kumnyoshea mkono Rais ambaye ndiye aliyemteua Waziri Mkuu huyo lakini vilevile ndiye mkuu wa serikali hiyo.

Mmoja akiondolewa na mwingine ni lazima afuate ndio maana rais anapokufa au kuacha urais kwa sababu zilizoanishwa Kikatiba Waziri mkuu naye anapoteza nafasi yake na baraza la mawaziri linavunjika! Ni sauti na mwangwi! Chini ya Ibara ya 36 Rais ndiye anauamuzi wa mwisho wa nani anatumikia serikali hii kwani ana uwezo wa kumfukuza mtu yeyote kwenye utumishi wa umma. Siyo Waziri Mkuu.

Lakini huwezi pia kunyoshea kidole Waziri Mkuu na rais bila kunyoshea kidole chama cha Waziri Mkuu na Rais. Ikumbukwe kuwa Rais wa Tanzania anachaguliwa na wananchi lakini sharti la msingi chini ya Ibara ya 39:1c. Ibara hiyo inasema mojawapo ya sifa za mtu kuwa Rais ni kuwa ni lazima awe "ni mwanachama, na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa". Kimsingi Rais ni lazima atoke kwenye chama. Katika suala letu rais wetu anatokana na Chama cha Mapinduzi - ndiyo mwanachama wake na ndicho kilichompendekeza. Kuinyoshea mkono serikali ni kunyoshea mkono chama kilichounda serikali hiyo.

Lakini pia tuangalie kwa namna nyingine kidogo; Bunge linapomnyoshea mkono Waziri Mkuu ina maana linaonesha halina imani na serikali - ndio maana inaitwa kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu - na hivyo halina imani na Rais. Bunge linapokosa imani na Rais ambaye anamteua Waziri Mkuu lenyewe pia linajikuta matatani kwani Rais ni sehemu ya Bunge! Ibara ya 62:1 iko wazi kuhusu hili "Kutakuwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano ambalo
litakuwa na sehemu mbili, yaani Rais na Wabunge" Hivyo, Bunge linaponyoshea kidole sehemu yake mojawapo - yaani rais - Bunge linajinyoshea lenyewe kidole; kutokuwa na imani na Waziri Mkuu ni kutokuwa na imani na Rais na kutokuwa na imani na rais ni kutokuwa na imani na sehemu ya bunge; Waziri Mkuu akilazimishwa kujiuzulu Rais naye ni LAZIMA ajiuzulu! Na Rais akijiuzulu Bunge lazima livunjwe! Wote wanawajibika kwa pamoja per excellence! 

Lakini pia tunaweza kuliona hili vizuri - Waziri Mkuu anapendekezwa na rais, na anapitishwa na Bunge. Sasa Bunge linapomgeuka Rais, Bunge linageuka uamuzi wake lenyewe. Ikumbukwe kuwa Pinda alipendekezwa na Rais, jina lake likaletwa Bungeni, Wabunge wakaulizwa na kuunga mkono uteuzi huo wa rais na sasa wanataka kuukataa. Sasa, hawawezi kuukataa na wao wakabakia! Naomba niweke tofauti kidogo ambayo ningependa ieleweke. Ni vizuri sana kuweka shinikizo Waziri Mkuu ajiuzulu au mawaziri wajiuzulu. Wabunge wanaweza kuweka shinikizo hilo kwa kutumia Bunge. Lakini wanapokaa na kuwa tayari kupiga kura ya kutokuwa na imani wamevuka kutoka kwenye shinikizo kwenda kwenye suala la kisheria ambalo lina matokeo; kupiga kura ya kutokuwa na imani ni Waziri Mkuu ni kupiga kura ya kutokuwa na imani na serikali (Rais) na kutokuwa imani na Rais (ambaye ni sehemu ya Bunge) ni kujishtaki lenyewe!

Ni sawa sawa na mtu kunyoshea kidole mtu kwenye kioo na kumtishia kumkata kichwa kwa panga. Well, ukitaka kumkata mtu wa kwenye kioo weka panga shingoni mwake, ukimkata yeye na wewe hubakii! hivyo, naunga mkono kabisa kura ya kutokuwa na imani na serikali lakini kama nilivyosema kwenye mada nyingine naamini watu wengi hawajui kuwa huwezi kuwa na kura ya kutokuwa na imani nusu - yaani ukaishia kwa Waziri Mkuu. Ni LAZIMA ili liende moja kwa moja kwa Rais, na kwa Bunge.

Ni matumaini yangu - na maombi yangu -kuwa Spika Makinda atakubali hoja hii na kuitisha kikao cha Bunge cha dharura chini ya kifungu cha 27:4 cha Kanuni za Bunge kuwa "Endapo manufaa ya Taifa yatahitaji kuwa Bunge lisikutane tarehe ile iliyowekwa kwa Mkutano utakaofuata, bali likutane tarehe ya mbele zaidi au ya nyuma zaidi, basi Spika anaweza, baada ya kushauriana na Kamati ya Uongozi, kuliita Bunge likutane tarehe hiyo ya mbele zaidi au nyuma zaidi." Ninaamini kama matakwa ya Katiba yametimizwa (taarifa ya asilimia 20 ya wabunge kutaka hoja hiyo iletwe) basi Spika NI LAZIMA aitishe kikao maalum cha Bunge mapema zaidi.

Ni matumaini yangu vile vile kuwa Rais Kikwete hatovunja baraza la mawaziri sasa hivi au kufanya mabadiliko yoyote kwa sababu ya hoja ya kina Zitto kwa sababu mabadiliko hayo sasa YAMECHELEWA MNO kiasi cha kupoteza umaana. Sasa hivi hoja iliyopo mbele ya taifa ni kuwa wananchi hawana imani na serikali yao na Rais Kikwete hawezi kupata imani hiyo kwa kufanya mabadiliko isipokuwa kwa Waziri Mkuu wake kupigiwa kura hiyo. Hivyo, ninaamini kabisa kuwa rais akubaliane na Spika ili Bunge liitishwe mapema kabisa iwezekanavyo ili Serikali yake ijaribiwe na wawakilishi wa wananchi na awe tayari kwa matokeo yoyote yale.

Hata hivyo, naamini pia kwa rais kukubali hili ni LAZIMA AWEKE WAZI kwa Wabunge wote kuwa Kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu ni kura ya kutokuwa na imani na serikali yake na ni kura ya kutokuwa imani na yeye na kuwa yuko tayari kabisa wabunge wawe uhuru kabisa katika kura ya SIRI kupiga kura hiyo na kuwa endapo wabunge hawana Imani na Waziri Mkuu na wakaonesha hivyo kwa kura basi Waziri Mkuu ataondolewa lakini siyo hapo tu na yeyemwenyewe atajiuzulu na kuvunja Bunge ili nchi ianze upya. Ikumbukwe huwezi kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu lakini ukataka kubakia ama na Rais au na Bunge.

Hakuna mabadiliko nusu! Tumeamua kuvua nguo, tuyaoge.


Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com

Mawaziri tumbo joto


WAKATI Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), amesema kuwa hakutumwa na Rais Jakaya Kikwete wala mtu yeyote, kuibua hoja ya kutaka Bunge lipige kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, mawaziri wengi sasa wanahaha kujaribu kujinasua na ‘fagio’ la mabadiliko ya uongozi.
Mawaziri walio katika wakati mgumu kuliko wengine wote ni wale waliotajwa na wabunge kuhusika na tuhuma za ufisadi na ubadhirifu wa mabilioni ya fedha za umma katika wizara zao.
Habari za uhakika kutoka serikalini, zimebainisha kuwa hofu ya mawaziri hao imekuja baada ya kuthibitika kuwa Rais Jakaya Kikwete atafanya mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri wakati wowote, ambapo inaelezwa kuwa atapunguza pia idadi ya wizara.
Taarifa zimesema kuwa baadhi ya mawaziri wameanza kukusanya vitu vyao, zikiwamo nyaraka na kuvihamishia majumbani mwao ama sehemu nyingine wanazoziamini kuwa salama.
Chanzo chetu cha kuaminika kutoka serikalini kimesema kuwa, hata baadhi ya mawaziri ambao hawakutuhumiwa moja kwa moja, wamekuwa wakikutana na wale wote wanaoaminika kuwa ‘watu wa karibu’ na Rais Kikwete, kwa nia ya kutaka wasaidiwe kubaki katika nafasi zao.
Hata hivyo, mmoja wa mawaziri aliyetajwa kuanza kuhamisha vifaa vyake alipoulizwa alikana kufanya hivyo na kwamba alikuwa mkoani kikazi.
Alipoelezwa namna ambavyo juzi alifika ofisini na kuondoka na rundo la vitu katika mkoba wake, waziri huyo kwanza alinyamaza, kabla ya kudai kuwa alifanya hivyo si kwa lengo la kuhama, bali ni kawaida yake kufanya kazi za ofisi nyumbani kwake.
“Si kweli, na hilo unalosema ni jambo la kawaida kwangu na hata dereva wangu anajua kuwa mara nyingi nachukua nyaraka zangu na kwenda kufanya kazi nyumbani.
“ Hata nikiwa ndani ya gari, badala ya kulala, huwa niko ‘bize’ na kufanya hiki ama kile. Kwa hiyo isichukuliwe kuwa nahamisha kitu,” alisema waziri huyo.
Zitto akana kutumwa
Akizungumza jana asubuhi katika kituo kimoja cha runinga, Zitto katika tuhuma za kutumwa na Kikwete, alisema yeye binafsi alisukumwa na taswira ya mabadiliko iliyoko kwa Watanzania wengi wanaotaka kuona hatua zikichukuliwa dhidi ya watendaji wabovu.
“Mimi nimetumwa na wananchi na ndiyo maana naishauri na kuisimamia serikali kama Katiba ya nchi inavyosema. Sasa kusema nimetumwa na Rais Kikwete, sidhani kama anaweza kufanya hivyo kwa lengo la kumwaibisha waziri mkuu wake,” alisema Zitto.
Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, alibainisha kuwa, viongozi wengi wanashindwa kusoma taswira hiyo ya watu kutaka mabadiliko.
Alifafanua kuwa alishangazwa na hatua ya waziri mkuu kuhitimisha Bunge pasipo kusema chochote kuhusiana na baadhi ya mawaziri wanaotakiwa kung’oka baada ya wizara zao kutajwa kwenye ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusika na ufujaji na matumizi mabaya ya fedha.
“Kwa kweli nilikuwa ‘disappointed’ na hatua ya waziri mkuu kuhitimisha Bunge bila kusema chochote, na hata nje mimi na Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), tulimfuata na kumuuliza alimaaninisha nini? Na tulimfahamisha hatua yetu ya kuendelea na mchakato wa kutaka Bunge lipige kura za kutokuwa na imani naye,” alisema.
Alisema kwa miaka minne ripoti za CAG zimetoa mapendekezo ya kutaka watendaji wabovu wachukuliwe hatua lakini hazikufanyiwa kazi licha ya wabunge kupiga kelele.
Zitto aliongeza kuwa wazo hilo si lake binafsi wala chama chake cha CHADEMA, bali ni la Watanzania wote wenye mapenzi mema kupitia kwa wawakilishi wao bungeni na kwamba ndiyo maana aliweza kukusanya saini za wabunge 75 kutoka vyama vyote isipokuwa UDP.
Aliongeza kuwa tayari wamewasilisha hoja yao kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, wakimtaka aitishe Bunge la dharura baada ya siku 14 ili kujadili na kupata muafaka.
“Mawaziri hawa si kwamba wengine wametajwa moja kwa moja kwenye ripoti hizo, isipokuwa wameshindwa kuwawajibisha watendaji wabovu wa chini yao na hivyo wao wanapaswa kung’oka kama sehemu ya uwajibikaji,” alisema.
Alisema kuwa Bunge halina mamlaka ya kumwajibisha waziri mmoja mmoja, hivyo njia pekee waliyonayo ni kwa waziri mkuu, kama walivyoamua kufikia hatua ya kukusanya saini ili wapige kura za kutokuwa na imani naye aondoke ama awachukulie hatua mawaziri husika.
“Tuliwapa muda mawaziri kuanzia Alhamisi hadi Jumapili ili wapime, wajiwajibishe wenyewe ama wamtose waziri mkuu, hivyo kwa kuwa hawakufanya hivyo basi sisi tunaendelea na mchakato wetu wa kumwajibisha Pinda,” alisema.
Aidha, Zitto amesema wabunge wote wa upinzani na wale wa CCM waliotia saini fomu ya kutaka waziri mkuu apigiwe kura ya kutokuwa na imani naye, wataungana na kufanya mikutano mikubwa kuhamasisha wananchi kuamua ikiwa Spika Anne Makinda atapuuza hoja yao.
Filikunjombe: Siogopi kufa
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, ameapa kuwa yuko tayari kufa kwa ajili ya kutetea Watanzania wanyonge na kwamba haogopi vitisho uchwara vinavyotolewa na baadhi ya watu.
Alisema kamwe hawezi kukaa kimya akitazama namna Watanzania wanavyoporwa haki zao na viongozi wachache wenye uroho wa madaraka.
“Hatuwezi kufumbia macho wizi huu unaoliangamiza taifa kwa hofu kuwa ni chama changu. Ubunge wangu ni kwa manufaa ya Wana Ludewa na Watanzania wote, hivyo, wanaonishambulia wao ndio maadui wa CCM na Watanzania,” alisema mbunge huyo.
Alipuuza madai kuwa hatua yake ya kuungana na wapinzani katika suala la kutia saini kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu ni hatua za kukihama chama chake.
“Huo ni ujinga. Sina wazo la kukihama chama changu, nakipenda na nitaendelea kuwa mwanachama tu, labda wanifukuze,” alisema.
Wanaharakati waja juu
Nao Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umesema kuendelea kwa ufisadi nchini ni aibu kwa serikali iliyoko madarakani, na umedai kutonyamazia aina yoyote ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za miradi ya wananchi zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Katika taarifa yao jana, TGNP wamesema wanataka mawaziri na watumishi wa serikali wanaotuhumiwa kutumia vibaya fedha za umma kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Ili kuonesha dhana ya uwajibikaji na utawala bora unaozingatia misingi ya haki za binadamu, tunaitaka serikali kuwawajibisha mara moja mawaziri, manaibu waziri na watendaji wakuu wa serikali na mashirika ya umma ambao wametajwa kuhusika na matumizi mabaya ya fedha za umma au kushindwa kusimamia rasilimali za taifa.
“Rais awafute kazi watendaji wanaotumia vibaya fedha za umma na kuwaongezea wananchi umaskini, ili liwe fundisho kwa watendaji wa serikali wenye tabia kama hiyo na wachukuliwe hatua za kisheria’ imesema taarifa hiyo iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji,” Anna Kikwa.


CHANZO - Tanzania Daima